Wakati saa kadhaa zikisalia kabla ya mchezo wa Mkondo wa Pili wa Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya USM Alger, Kocha Msaidizi wa Young Africans, Cedric Kaze amechimba mkwara mzito kuwa wanataka medali ya ubingwa wa mashindano na sio vinginevyo.
Young Africans leo Jumamosi (Juni 03) wanatarajia kushuka kwenye Uwanja wa 5 July 1962 kuvaana na USM Alger katika mchezo wa fainali ya pili inaotarajiwa kupigwa majira ya saa nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Young African wanaingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo wa kwanza kwa kipigo cha mabao 2-1, walichoipata kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es salaam Jumapili iliyopita.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya kikosi chao, Kaze alisema: “Tunafahamu kuwa mpaka sasa tuna nafasi ya kushinda medali ya michuano hii kwa matokeo yoyote ambayo tutayapata katika mchezo huu, lakini hatutaki kupata medali ya mshindi wa pili.
“Tumekaa na wachezaji na tunaamini tuna nafasi ya kushinda ubingwa wa mashindano haya na kuvaa medali ya dhahabu. Tumekaa chini na wachezaji wetu nao wametuhakikishia kuwa wapo tayari kupambana.”