Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga na rekodi zake tamu CAFCL

Yanga Bilioni 2 CAF Yanga na rekodi zake tamu CAFCL

Mon, 26 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Yanga imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara kwanza kwenye historia ya klabu hiyo, baada ya kuichapa CR Belouizdad mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Mkapa.

Yanga imekuwa timu ya kwanza Tanzania kufuzu hatua hiyo muhimu na kuweka rekodi yake, lakini ya Tanzania kwa timu zake kufuzu kwenye robo fainali ya michuano ya Caf kwa miaka sita mfululizo.

Kiwango cha Yanga kimekuwa kwa kasi kwa miaka ya hivi karibuni baada ya kushindwa kuvuka malengo yao ya kufika hatua ya makundi msimu uliopita, sasa imefanya makubwa zaidi ya malengo waliyokuwa wameweka.

Kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi ambaye alikuwa hapewi nafasi ya kufanya makubwa kwenye timu hiyo, amekuwa na mafanikio zaidi ya Nasreddine Nabi ambaye alishindwa kuifikisha timu hiyo makundi ambayo lilikuwa lengo, lakini akaipeleka fainali ya Kombe la Shirikisho.

Rekodi mpya

Yanga imefuzu robo fainali ya michuano ya CAF kwa mara ya pili mfululizo bila kusubiri mchezo wa mwisho wa kundi, msimu uliopita ilipata nafasi ya kwenda hatua hiyo ya Kombe la Shirikisho baada ya kuichapa US Monastir mabao 2-0 na kumaliza mchezo wa mwisho dhidi ya TP Mazembe bila kitu cha kupoteza, msimu huu imefanya jambo hilohilo inakwenda kumaliza na Al Ahly ikiwa haina kitu cha kupoteza kwenye mchezo wa mwisho bali kutafuta nafasi ya kwanza kwenye kundi tu.

Mabao mengi

Yanga imeweka rekodi mpya kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu huu ikiwa hadi sasa ndiyo imefunga mabao mengi zaidi kuliko timu nyingine zote kwenye hatua hii ya makundi kabla ya mchezo wa mwisho, Yanga imefunga mabao tisa kutoka kundi D, huku kiungo wake Pacome Zouzoua akiwa ndiye mchezaji aliyefunga mengi, baada ya kutupia matatu akiwa anashika nafasi ya pili kwenye ufungaji wa jumla moja nyuma ya Sankara William Karamoko aliyekuwa Asec Mimosas ambaye kwa sasa hayupo kwenye soka Afrika.

Mshambuliaji wa Yanga, Kennedy Musonda anashika nafasi ya pili kwa pasi za mabao yaani asisiti, akiwa nazo mbili.

Pia timu hiyo imekuwa ya kwanza kuwa na pointi nane na kufuzu kwenda robo ikiwa ndiyo timu yenye pointi chache zaidi kufanikiwa kwenda robo msimu huu.

Al Ahly imefuzu pamoja na Petro de Luanda zimefuzu zikiwa na pointi tisa, Asec Mimosas 11, Mamelodi 10, TP Mazembe 10.

Tanzania pekee

Kwenye michuano ya mwaka huu, nchi kadhaa zilifanikiwa kuingiza timu mbili kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini Tanzania peke yake ndiyo timu zake mbili zina nafasi ya kwenda robo fainali, huku mataifa mengine yakitoa timu moja moja.

Endapo Simba ikiichapa Jwaneng Galaxy kwenye mchezo wa mwisho itafikisha pointi tisa na kufuzu kama Yanga, lakini hakuna taifa lingine ambalo lina nafasi ya kuingiza timu mbili kwenye hatua hiyo hadi sasa.

Timu sita ambazo zimeshafuzu robo hadi sasa ni TP Mazembe ya DR Congo, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Petro de Luanda ya Angola, Al Ahly ya Misri na Asec Mimosas ya Ivory Coast.

Timu zinazoweza kufuzu na kutimiza idadi ya nane zinazotakiwa hatua hiyo ni Simba ya Tanzania, Al Hilal ya Sudan, Esperance ya Tunisia, Wydad Casablanca ya Morocoo na Jweneng Galaxy ya Botswana.

Daraja la tatu latawala robo fainali

Kabla ya kupangwa kwa hatua ya makundi, timu ziligawanywa kwenye madaraja manne kutokana na mafanikio yao kwenye michuano ya Caf kwa miaka iliyopita.

Daraja la kwanza ni lile ambalo timu zake ni bora zaidi kwenye michuano hiyo ambalo lilikuwa na vigogo kama Al Ahly, Wydad, Esperance na Mamelodi, huku daraja la pili likiwa na CR Belouizdad, Pyramids, Simba na Petro de Luanda, daraja la tatu zilikuwa TP Mazembe, Al Hilal, ASEC Mimosas na Yanga, huku la nne likiwa na Étoile du Sahel, Jwaneng Galaxy, FC Nouadhibou na Medeama.

Daraja la tatu ambalo lilikuwa linaonekana la kawaida ndiyo pekee hadi sasa limeshapeleka timu tatu TP Mazembe, Yanga na Asec zikiwa zimeshakwenda robo, lakini pia timu yake moja Al Hilal ikiwa na nafasi nayo ya kufuzu.

Daraja la kwanza, la pili na la tatu yamepeleka timu mojamoja Mamelodi na Al Ahly na Petro de Luanda.

Kutengeneza nafasi

Bado kiungo wa Yanga, Pacome anaingia tena kwenye kipengele hiki akiwa ametengeneza nafasi 15, ikiwa ni moja mbele ya Aziz Ki ambaye ametengeneza nafasi 14 hadi mchezo wa juzi unamalizika.

Mchezaji anayefuata kwa kutengeneza nafasi nyingi katika hatua ya makundi ni Mohamed Chibi wa Pyramids ambaye amelingana na Pacome akiwa na nazo 15.

Nidhamu

Wakati Simba ikiwa inashika nafasi ya kwanza kwa timu zilizopewa kadi nyingi za njano kwenye michuano hiyo hadi sasa baada ya mastaa wake kulambwa kadi 14 na kiungo wake Sadio Kanoute akiwa kinara kwa kupewa nne, Yanga imeonekana kuwa na nidhamu nzuri baada ya kukusanya kadi za njano nne tu na kushika nafasi ya 15 kati ya timu 16.

Chukua hii…

Mabao matatu ambayo Yanga imefunga kwenye mchezo uliopita, yamefungwa na wachezaji watatu ambao walikuwa kwenye fainali za Afcon 2023, Mudathir Yahaya (Tanzania), Kennedy Musonda (Zambia), Aziz Ki ( Burkina Faso)

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: