Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga na kocha wa makipa Dodoma Jiji

Yanga Ushindi Pic Data Yanga na kocha wa makipa Dodoma Jiji

Fri, 19 Mar 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

SIKU mbili alizokuwa amepewa kocha wa makipa wa timu ya Dodoma Jiji, Mfaume Athumani zilikuwa zinaisha usiku wa kuamkia leo Alhamisi ambapo ilikuwa ni jibu moja tu.

Jibu la kwamba Mfaume ameshapewa barua ya kuruhusiwa kujiunga na ‘chama la wananchi’ Yanga ili kuungana na benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Kocha Juma Mwambusi.

Ipo hivi, Mfaume ambaye aliwahi kuwa kipa wa Yanga, alichomolewa kwenye kikosi cha timu ya Dodoma Jiji kabla ya mchezo wake dhidi ya Kagera Sugar Ijumaa wiki iliyopita akakutana na mabosi wa Jangwani.

Akizungumzia hilo, Mfaume alithibitisha na kusema kwamba ishu kubwa ambayo ilimfanya asisaini dili la kuwa miongoni mwa benchi jipya la Yanga ni barua ya mabosi wake wa sasa Dodoma Jiji.

‘‘Nilikuwa Dar kweli nikakutana na viongozi wa Yanga ambapo lengo ni kuwa kocha wa makipa wa timu ile, ila bado nina mkataba hadi mwishoni mwa msimu na timu yangu ya sasa Dodoma Jiji, hivyo ili nisaini ilitakiwa barua kutoka kwa timu yangu,” alisema.

Mfaume ambaye alirudi jijini Dodoma juzi Jumanne kwa ajili ya kufuatilia uwezekano wa kupewa barua kutoka kwa mabosi wa timu hiyo iliyopo chini ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, alisema alipewa siku mbili za kukamilisha au kubaki ndani ya timu hiyo.

‘‘Ndio nimerudi Dodoma kufuatilia uwezekano wa kupata ruhusa kwa timu yangu ambapo nina siku mbili tu za kufanikisha au kama haitawezekana nitabaki kuitumikia timu hadi mwishoni mwa msimu,’’ alisisitiza mkongwe huyo.

Imeandikwa na Matereka Jalilu

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz