Kama kuna msimu ambao Yanga imetawala soka la Tanzania basi ni huu wa 2022/23. Ubingwa wa Ligi Kuu kibindoni tayari huku ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Afrika ukisubiri.
Yanga wako fainali ya mashindano ya CAF kwa mara ya kwanza katika historia. Hii ina maana kwamba shabiki wa Yanga wa kipindi hiki anashuhudia na kufurahia kitu ambacho hakuna shabiki wa kizazi chochote wa klabu hiyo aliyekishuhudia na kufurahia.
Licha ya kwamba Yanga ndiyo klabu ya kwanza Tanzania kufika robo fainali ya mashindano ya CAF, ilipofanya hivyo mara mbili mfululizo 1969 na 1970 kwenye Klabu Bingwa Afrika, lakini haikuweza tena kufika hatua hiyo achilia mbali kuvuka.
Itoshe tu kusema kwamba huu ulikuwa msimu wa Yanga Afrika. Hata hivyo, kuna kitu cha kihistoria ndani ya mafanikio haya ambacho watu wengi hawakijui.
Kama historia ina nafasi yoyote katika mafanikio, basi historia ya Yanga itakuwa imecheza nafasi yake msimu huu.
Wahenga walisema jina baya hapewi mwana. Hii ni kwa sababu jina ni kielelezo cha mtu; haiba na hulka. Mwanao ukimuita tabu yumkini atataabika.
Katika miaka yake ya mwanzo mwanzo kabisa Yanga ilijiita Italiana ikijifananisha na timu ya taifa ya Italia iliyobeba ubingwa wa dunia mara mbili mfululizo, 1934 na 1938.
Timu hiyo iliongozwa na nahodha Giuseppe Meazza ambaye alikuwa pia nahodha wa klabu ya Inter Milan ya Italia. Kwa heshima ya nahodha huyo klabu hiyo inalitumia jina lake kuuita uwanja wao wa nyumbani wanaoutumia kwa pamoja na majirani zao, AC Milan.
Kwa hiyo unaweza ukasema mafanikio ya Yanga msimu huu ni mwendelezo wa mafanikio ya mashujaa wao, Italia. Ikumbukwe kwamba msimu huu Italia imeingiza timu tatu kwenye fainali zote tatu za mashindano ya klabu barani Ulaya. Inter Milan - Ligi ya Mabingwa, AS Roma - Europa League na Fiorentina Europa Conference League.
Kama ilivyoelezwa hapo juu, wakati Yanga inaanzishwa miaka ya katikati ya 1930, Italia ndiyo walikuwa wafalme wa soka duniani. Walishinda Kombe la Dunia mara mbili mfululizo 1934 na 1938. Kwa kufanya hivyo Italia ikawa nchi ya kwanza kutetea ubingwa wa Kombe la Dunia.
Kwa heshima ya Italia, Yanga ambayo ilianzishwa mwaka 1935, ikajiita Italiana. Naam, Yanga ilijiita Italiana 1936 ikijifananisha na mabingwa hao wa dunia.
Jina hilo lilidumu hadi vilipozuka Vita vya Pili ya Dunia 1939 na kupotea kidogo kidogo. Ni hivyo Vita vya Dunia pia ndivyo vilivyoondoa ufalme wa Italia kwenye soka la dunia. Hii ni kwa sababu Kombe la Dunia halikurudi tena hadi 1950, na liliporudi likaikuta Italia ikiwa dhooful hali. Kikosi chake bora kuwahi kutokea kiliteketea mwaka mmoja kabla, 1949, kwenye ajali ya ndege iliyoitwa Superga air disaster.
Ajali hiyo ilitokea Mei 4, 1949 pale ndege iliyobeba kikosa cha klabu ya Torino ilipopata ajali na kuua watu wote 31 waliokuwemo ndani. Watu hao walikuwa wachezaji wa kikosi bora zaidi cha klabu ya Torino kuwahi kutokea.
Kikosi hicho ambacho kilibatizwa jina la Grande Torino (Torino babu kubwa au Torino Dume kwa Kiswahili cha mtaani, ndicho kilichounda timu ya taifa ya Italia 'Azzuri' katika nyakati hizo. Torino ikapotea, Azzuri ikapotea na ufalme ukapotea.
Miaka mingi baadaye unapoona Italia inatawala tena soka la Ulaya usishangae pia kuona Yanga ikitawala soka la Afrika. Yanga na Italia zote ni Italiana.
Hata nahodha mwenye mafanikio zaidi katika historia ya Yanga aliitwa Cannavaro akifananishwa na nahodha wa Italia aliyeiongoza nchi hiyo kutwaa Kombe la Dunia 2006. Yanga na Italia zimekuwa na uhusiano huo tangu na tangu.
Baada ya anguko kufuatia Vita vya Pili vya Dunia na ajali ya Superga, Italia walirudi tena kwa kishindo na kufika fainali ya Kombe la Dunia 1970.
Walipoteza fainali mbele ya Brazil yenye Pele, lakini hayakuwa mafanikio madogo kwa Italia. Itakumbukwa kuwa mwaka huo Yanga ilifika robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika na kutolewa kwa tabu na Asante Kotoko ya Ghana.
Nasema kwa tabu kwa sababu ilibidi zichezwe mechi tatu ili kuamua mshindi. Mechi ya kwanza Dar es Salaam iliisha kwa sare ya 1-1. Mechi ya pili Accra ikaisha kwa sare ya 1-1. Wakati huo hakukuwa na penalti, hivyo ikaamuliwa mechi ya tatu ikachezwe uwanja huru. Ikaenda kufanyika Ethiopia, Yanga ikafungwa 2-0. Italia huzuni, Yanga huzuni.
Italia wakarudi tena kwa kishindo Kombe la Dunia 1982 na kulitwaa. Na huo ndiyo mwaka wa kwanza kwa Yanga kutwaa ubingwa wa ligi tangu 1974. Italia walirudi na Yanga wakarudi. Ukifuatilia mwenendo wa soka la Italia unafanana sana na mwenendo wa soka la Yanga, kila wakati. Kwa mfano msimu huu timu tatu za Italia zimeingia fainali ya mashindano ya klabu Ulaya.
Mara ya mwisho Italia kupata mafanikio kama ya msimu huu ilikuwa msimu wa 1993/94. AC Milan fainali ya Ligi ya Mabingwa, Parma fainali ya Kombe la Washindi na Inter Milan fainali ya Kombe la UEFA.
Msimu huo pia ulikuwa wa mafanikio makubwa kwa Yanga kwani ilishinda ubingwa wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati jijini Kampala, Uganda.
Kwa kufanya hivyo, Yanga ikawa timu ya kwanza ya Tanzania kushinda kombe la kimataifa kwenye ardhi ya ugenini. Pia Italia ilitawala soka la Ulaya msimu wa 1997/98 kwa timu tatu kufika fainali mbili za mashindano ya Ulaya Juventus fainali ya Ligi ya Mabingwa, Inter na Lazio fainali ya Kombe la UEFA.
Msimu huo pia Yanga ilitawala kwa kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Kwa kufanya hivyo, Yanga ikawa timu ya kwanza kufikia hatua hiyo kutoka ukanda wa Cecafa. Ni msimu wa Yanga, ni msimu wa Italia. Ni msimu wa Italiana.