Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga na hesabu kali kwa Medeama leo

Yanga Caf Mks Yanga na hesabu kali kwa Medeama leo

Wed, 20 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

 Yanga imeshauriwa kushambulia kwa tahadhari ili kuhakikisha inapata bao la mapema na kutumia kila nafasi itakayopata leo kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mechi ya nne ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi dhidi ya Medeama.

Timu hizo zinarudiana jijini Dar es Salaam, wakati zikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bao 1-1 nchini Ghana, Desemba 8 mwaka huu.

Mechi ya leo ni ya nne kwa timu hizo ambazo mwaka 2016 katika mechi ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika zilikutana kwenye uwanja huo na Yanga kulazimishwa sare ya bao 1-1 kabla ya kukubali kipigo cha mabao 3-1 ugenini.

Yanga itacheza kufa au kupoikihitaji pointi tatu ambazo zitaamua hatima ya kurejesha matumaini ya kumaliza nafasi mbili za juu kwenye kundi D ambalo bado liko wazi kwa kila timu baada ya mechi tatu ambalo linaongozwa na Al Ahly ya Misri yenye alama tano, CR Belouizdad yenye pointi nne sawa na Medeama iliyo nafasi ya tatu huku Yanga ikiwa mkiani na pointi mbili ilizovuna baada ya sare na Ahly nyumbani na nyingine na Medeama ugenini.

Kama itashinda itafikisha pointi tano, ikisubiri kumalizana na wababe Al Ahly ugenini na Belouizdad nyumbani mechi zitakazopigwa mwakani kuanzia Februari wakitakiwa kushinda ili kumaliza makundi na pointi 11 ambazo zitawapeleka robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza.

Jana kocha Miguel Gamondi alisisitiza jukumu lao ni moja tu katika mchezo huo - kupata ushindi na huo ni mchezo wao muhimu. Alisema: “Tumefanya kila kitu kuhakikisha kuwa tunapata ushindi kwenye mchezo huu, mazoezini na wachezaji, tumeshamaliza maandalizi, tunafahamu kuwa jukumu letu ni moja tu kuhakikisha tunapata ushindi kwa kuwa huu ni mchezo muhimu kwetu.”

Wachambuzi wa soka nchini wamesema kwa namna mechi ya kwanza ya Yanga na Medeama ilivyokuwa kitu cha kwanza inachopaswa kufanya Yanga ni kucheza kwa nidhamu na kujitahidi kutumia vyema nafasi zitakazopatikana.

Wamekwenda mbali zaidi na kubainisha kwamba, Medeama ni timu inayocheza soka la kasi na la nguvu jambo ambalo Yanga inapaswa kujipanga zaidi kukabiliana nalo, lakini ikiwa inatumia sana dakika 15 za kipindi cha kwanza kushambulia.

Hata hivyo, rekodi zinaonyesha Medeama inafungika kirahisi kipindi cha pili, katika mechi zake nane za kimataifa za karibuni, nyavu zake zimetikiswa zaidi kipindi cha pili.

Katika mechi hizo, imefungwa mabao 10, matatu pekee ikiruhusu kipindi cha kwanza dakika ya 36, 39 na 27 na kipindi cha pili imefungwa mabao saba dakika ya 66, 75, 88, 70, 88, 73 na 48 ikiwamo mmoja la penalti.

Timu hiyo pia imefunga zaidi kipindi cha pili, katika mabao manane iliyoandika kwenye mechi hizo, matatu tu imefunga kipindi cha kwanza dakika ya 27, 24 na 22 na matano kipindi cha pili dakika ya 45, 90, 50, 66 na 69, mawili yakiwa kwa penalti.

>>> inaendelea uk.27

Kinara wake wa kufunga ni Sawah J  ambaye amefunga matatu, mengine yamefungwa na Molotey D, Mamudu K, Babil n k, Abdulai N na Asmah K.

Katika mechi hizo nane, saba ni za Ligi ya Mabingwa na moja ya dunia ya kirafiki ikitoka sare ya bao 1-1 na Yanga, imeshinda 2-1 dhidi ya CR Balouizdad, 3-1 dhidi ya Horoya na bao 1-0 dhidi ya Remo Stars.

Imefungwa mara nne, kwa matokeo ya 3-0 dhidi ya Al Ahly, 2-1 dhidi ya Horoya, bao 1-0 dhidi ya Remo Stars na matokeo kama hayo dhidi ya Kara.

 Eneo ambalo Medeama imekuwa hatari zaidi ni katika mistari ya pembeni ambapo imekuwa hodari kupita huko kutokana na ubora na mabeki wake wa pembeni Kwadwo Amoako na Mamadu Kamaradin ambao muda mwingi hupanda na kuongeza nguvu kwa mawinga Daniel Lomotey na Derrick Fordjour ambao wana kasi sana.

Yanga inatakiwa kuwa imara zaidi kwenye maeneo hayo na kuwadhibiti wachezaji wa Medeama kutofanya mikimbio sahihi.

Sehemu nyingine ambayo Medeama imetega silaha yake ya maana ni eneo la ushambuliaji wa kati ambapo anacheza straika aliyefunga bao la timu hiyo kwenye mechi ya kwanza, Jonathan Sowah raia wa Ghana.

Mwamba huyu amekuwa na nguvu, kasi na ubora mkubwa wa kucheka na nyavu hata kwenye mechi ya kwanza aliwasumbua Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca na Dickson Job hivyo anatakiwa kuchungwa zaidi.

Mchezaji wa zamani wa Yanga, Said Maulid ‘SMG’, alisema Yanga inatakiwa kuiheshimu Medeama na kucheza kwa tahadhari kubwa huku ikitafuta bao la mapema bila kuwaza inacheza kwenye uwanja wake wa nyumbani.

“Medeama sio timu ya kubeza. Tuliona walivyocheza mechi ya kwanza, wana kasi, nguvu na morali ya juu jambo ambalo Yanga wanatakiwa kuliheshimu na kuwa tayari kukabiliana nalo lakini wakati wakifanya hivyo wanahitajika kuhakikisha wanapata bao mapema ili kupunguza presha,” alisema SMG.

Kocha wa zamani wa Yanga, Kenny Mwaisabula ‘Mzazi’, alisema Yanga isiingie uwanjani kwa kuwabeza Medeama kwani nao wanahitaji ushindi na wana timu bora.

“Yanga iingie ikijua Medeama nao wanaitaka mechi hii, waende wakijua watakutana na watu wagumu hivyo wacheze kwa nguvu zote huku wakitumia vyema faida ya mashabiki na uwanja wa nyumbani. Naamini itakuwa mechi nzuri na yenye ushindani na naona Yanga ina nafasi kubwa ya kupata ushindi,” alisema Mwaisabula.

Yanga itakuwa na faida ya kurejea kwa beki wake wa kushoto, Joyce Lomalisa aliyeikosa mechi ya mkondo wa kwanza kutokana na majeraha madogo aliyoyapata lakini pia mastaa wake wote tegemeo ambao baadhi yao walipumzishwa kwenye mechi iliyopita ya ligi dhidi ya Mtibwa Sugar akiwemo Stephene Aziz Ki, Pacome Zouzou, Djigui Diarra watakuwepo kuhakikisha jeshi la kocha mwenye misimamo, Miguel Gamondi linapata ushindi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live