Kikosi cha timu ya Yanga SC, leo kimefanya mazoezi ya gym ikiwa ni muendelezo wa maandalizi kabla ya usiku wa leo kusafiri kwenda Algeria kucheza mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad.
Mchezo huo wa Kundi D, unatarajiwa kuchezwa Novemba 24, mwaka huu nchini Algeria majira ya saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Baada ya hayo mazoezi, kikosi hicho kikiwa na nyota ambao hawapo kwenye majukumu ya timu zao za taifa, kinatarajiwa kusafiri leo usiku kwa kutumia Ndege ya Shirika la Uturuki kuelekea Algeria, ambapo msafara utapitia nchini Uturuki kabla ya kutua Algeria kesho Jumanne saa 10 jioni.
Wakati kundi la kwanza likiondoka usiku wa leo, kundi la pili litaondoka Jumatano ya Novemba 22, baada ya kumaliza majukumu yao katika mchezo wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, utakaochezwa kesho Jumanne Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, dhidi ya Morocco.
Khalid Aucho ambaye yupo na kikosi cha Uganda, Djigui Diarra (Mali) na Stephane Aziz Ki (Burkina Faso), wao wataungana na timu moja kwa moja huko Algeria baada ya kumaliza majukumu yao katika timu zao za taifa.