Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi ametamka kwamba kwa hali ilivyo ndani ya kikosi hicho atatua Tunisia kibabe sana na wataanza vizuri mechi za Kombe Shirikisho siku 10 zijazo.
Yanga itaanzia hatua hiyo ya makundi ya Shirikisho ugenini dhidi ya US Monastir ya Tunisia Februari 12 kabla ya kukiwasha na TP Mazembe Jijini Dar es Salaam Februari 19. Timu nyingine iliyopo kwenye kundi la Yanga ni Real Bamako ya Mali.
Juzi usiku uongozi wa Yanga uliingia mkataba maalum kwa ajili ya mechi zao sita za Shirikisho Afrika hatua ya makundi na kampuni ya Haier wa Sh 1.5 bilioni. Nabi alisema fedha hizo zitaongeza wepesi katika safari zao tatu za mechi za ugenini haswa ile ya kwanza nchini kwao Tunisia ambapo Mwanaspoti linajua wanaondoka wiki ijayo.
"Tafsiri ya udhamini wa namna hii unaipata katika kusimamia timu inakuwa katika maisha bora,"alisema Nabi ambaye amewapa Yanga mataji manne tangu atue. "Ujio wa fedha kama hizi ungekuwa hauna maana kama timu ingekuwa inaishi maisha magumu, lakini ni tofauti hapa Yanga timu imekuwa ikipata maisha bora sana ya kimaandalizi.
"Tunaposafiri kwenda mechi yoyote nje tumekuwa tukiishi maisha kulingana na programu tuliyojipangia na ndio maana sasa tumeanza kufanikiwa zaidi na najua tutafanya vizuri msimu huu kwenye makundi.
"Huwa tunakutana na timu zinalala viwanja vya ndege lakini kwetu ni tofauti hata tunapofika sehemu na tunatakiwa kusubiri kuunganisha ndege huwa wachezaji wanapata nafasi bora ya kupumzika hotelini.
"Mimi nafahamu Kuna gharama kubwa sana katika kuilea timu ya namna hii, ukiacha kununua wachezaji kwa gharama kubwa lakini pia kuna kazi ya kuhakikisha wachezaji kama hawa wanatunzwa vizuri,"alisema Kocha huyo ambaye amempa Mamadou Doumbia mechi tano aonyeshe ubora wake.
"Mchezaji akishamaliza kusajiliwa na kulipwa stahiki zake anakuja kukutana na matunzo Bora na malipo yake kwa wakati hii inatosha kumfanya mchezaji ajitume uwanjani," alisema na kuongeza kuwa wachezaji wamefurahishwa na jezi mpya.
"Mimi sivai jezi hizi za wachezaji lakini siku ambayo wachezaji walikwenda kupiga picha za matangazo,waliporudi walisimulia juu ya ubora wa hizi jezi, nafikiri walikuwa sahihi kusifia hii ni jezi nyingine Bora ambayo imetengenezwa hapa Yanga lakini pia kibiashara ni jambo zuri."
AZIZ KI DAK 40
Nabi amesema ana muda mfupi wa kupandisha ubora wa Stephane Aziz KI ambaye kwa sasa katika mechi ngumu anahimili kucheza kwa umahiri dakika 40 tu.
"Amecheza vizuri,kuna kitu amefanya nakubali lakini bado hajawa katika ubora ambao nautaka na mimi kocha nikafurahi kama walivyofurahi mashabiki,"alisema Nabi ambaye ni kocha wa zamani wa El Merreikh mwenye uraia wa Ubelgiji.
"Ile ni mechi ndogo sana (dhidi ya Rhino), tutakapokuja kucheza mechi ya ushindani mkubwa dakika nyingi sana Azizi anaweza kucheza ni 40 kwasasa ili acheze kwa ubora mkubwa,"alisema
Aidha Nabi alisema watatumia siku 10 zilizobaki kabla ya mchezo wa Monastir kuhakikisha wanaendelea kupandisha ubora wake kabla ya mchezo huo mgumu. "Tunakwenda kucheza mechi ngumu sana dhidi ya Monastir, kuna kazi nilikwambia wiki iliyopita ambayo tunaifanya kuhakikisha Azizi na wengine ambao viwango vyao vipo chini tunavipandisha.
"Tuna siku 10 zimebaki kabla ya mechi hiyo ngumu lakini hapa kati pia tutakuwa na mechi ngumu dhidi ya Namungo ya ligi tutatumia hizi siku kuhakikisha tunaongeza ubora wake."