Kikosi cha Yanga kinatazamiwa kusafiri kwa ndege leo Ijumaa kutoka Dar es Salaam kuelekea jijini Arusha kwa ajili ya mchezo wa nusu fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho FA dhidi ya Ihefu utakaochezwa Jumapili Mei 19 mwaka huu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa.
Yanga imetinga hatua hiyo kwa kuichapa Tabora United mabao 3-0 katika hatua ya robo fainali huku Ihefu FC ikiiondosha Mashujaa kwa penalti 4-3 baada ya dakika 90 kukamilika kwa suluhu.
Katibu wa Matawi ya Yanga Mkoa wa Arusha, Maulid Rashid amesema wanatazamia kikosi cha timu yao kuingia jijini hapa leo Ijumaa tayari kwa ajili ya mchezo huo.
Amesema mashabiki na wanachama wa Yanga wamejipanga kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kuipokea timu hiyo ambapo kutakuwa na msafara wa mabasi madogo nane aina ya Coaster.
“Mwitikio ni mkubwa mashabiki wengi kutoka Mto wa Mbu, Longido hapa Arusha mjini na maeneo mengine tayari wamethibitisha kesho kwenda kuwapokea mashujaa wetu,” amesema Maulid.
Ameongeza kuwa msafara wa kuelekea KIA utaanza saa 3:00 asubuhi ambapo pia ametumia fursa hiyo kuwataka mashabiki wa Yanga wanaoishi maeneo ambayo msafara utapita kama Kingori, Kikatiti, Maji ya Chai, Usa, Tengeru, Shangarai, Kwa Mrefu, Ngulelo, Kimandolu, Sekei, Philips na Sanawari kujitokeza kwa wingi.
Maulid ametumia fursa hiyo kuweka wazi kuwa hana wasiwasi na mchezo wa Jumapili kwani anaamini baada ya kutetea ubingwa wa Ligi pia wanakwenda kumgeuza Ihefu kama daraja la kwenda kutetea ubingwa wa Kombe la FA.
Yanga ambayo ndio bingwa mtetezi wa michuano hiyo, safari yake msimu huu kutetea ubingwa wake ilianzia kwenye ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Hausing FC, kisha ikaichapa Polisi Tanzania 5-0. Baadaye ikashinda 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji FC kabla ya kuiondosha Tabora United kwa mabao 3-0. Katika mechi hizo nne imefunga mabao 15 na kuruhusu moja pekee huku mshambuliaji wa kikosi hicho Clement Mzize ndiye kinara wa michuano hiyo akifunga mabao matano.
Kwa upande wa Ihefu, matokeo yao hadi kufika nusu fainali yalikuwa hivi; Ihefu 3-0 Rospa, Ihefu 2-0 Mbuni, KMC 0-3 Ihefu, Ihefu 0-0 Mashujaa (Ihefu ikashinda kwa penalti 4-3). Kumbuka timu zote hizo zilianzia raundi ya pili.
Mshindi wa mchezo huo atacheza fainali dhidi ya mshindi wa nusu fainali ya kwanza kati ya Azam dhidi ya Coastal Union watakaopambana kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza. Fainali itachezwa Juni 2 mwaka huu.