Nafasi ya Yanga kusajili mshambuliaji inaweza kubaki kwa kumsajili Simon Msuva pekee na endapo itatoa sababu za kutosha zitakazowaridhisha Shirikisho la Soka Afrika (CAF) wanaoweza kumchomeka kwa faini.
Yanga dirisha la usajili sambamba na Azam na Singida Fountain Gate lilishafungwa ambapo kama Yanga itamsajili Msuva anaweza kuingia endapo tu watatoa sababu, huku pia hatua ya mshambuliaji huyo kuwa huru ikiwarahisishia kwa kuwa bado dirisha la ndani la usajili halijafungwa.
Usajili wa ndani utafungwa Agosti 31 saa 6:00 usiku Msuva anaweza kuingia kabla ya muda huo kumalizika.
Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salum Madadi amesema kuwa kwasasa ni Simba pekee ambao ndio wanaweza kufanya usajili huku klabu zingine muda wao umemalizika na labda kuwe na sababu kubwa itakayowaridhisha CAF.
“Simba pekee ndio wanaweza kusajili sasa bila kikwazo, na sababu zao ni mbili kwanza ni kutokana na hatua yao ya kuanzia hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika na sababu ya pili ni hiyo ya ushiriki wao wa Super Cup,”alisema Madadi ambaye kocha wa zamani wa Taifa Stars.
“Klabu zingine zinaweza kusajili lakini hapo wanaweza kukutana na malipo ya adhabu lakini kikubwa hapa ni kama hiyo klabu itatoa sababu nzito ambayo CAF itawaridhisha na kuwapa hiyo nafasi.
“Unajua hizo klabu tatu za Yanga, Singida na Azam wao wanacheza wiki hii na ndio maana nasema lazima kuwe na sababu kubwa itakayowapa mashiko CAF na kuwapa hiyo nafasi ya kusajili,” liongeza mzawa huyo ambaye ni msomi na anayeheshimika katika soka la kimataifa.