Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga kuendeleza walipoishia

3534db9dfe31b6a39f10be0a3faa9eee Yanga kuendeleza walipoishia

Tue, 20 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

BAADA ya Yanga kuichapa Biashara United kwa bao 1-0, Kaimu Kocha Mkuu wa timu hiyo, Juma Mwambusi amesema sasa nguvu zote wanahamishia katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Gwambina FC utakaopigwa leo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 1:00 usiku.

Vinara hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara wenye pointi 54 kileleni, wanaingia katika mchezo huo kuwakabili Gwambina FC wanaoshika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi hiyo yenye timu 18, wakiwa wamejikusanyia pointi 30 baada ya kucheza mchezo 24.

Yanga itashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kutoka suluhu tasa katika mchezo wa raundi ya kwanza uliopigwa katika Uwanja wa Gwambina, Misungwi jijini Mwanza, hivyo leo watataka kuondoka na pointi zote tatu ili kujiimarisha kileleni.

Akizungumza na HabariLEO jana, Mwambusi alisema maandalizi ya mchezo huo yamekamilika na kikosi chake kipo vizuri, wachezaji wana morali ya juu hata wale ambao waliokosekana katika mchezo uliopita dhidi ya Biashara United wameungana na timu kwa ajili ya kuzisaka pointi tatu.

“Malengo yetu ni ubingwa wa Ligi Kuu, hivyo tutaingia uwanjani tukiwa na lengo moja tu la kuondoka na pointi tatu ambazo zitatuwezesha kutanua wigo wa pointi kileleni mwa msimamo.”

“Ushindi wa mchezo wetu uliopita umerudisha morali kikosini, nimewaambia vijana wangu wasahau yaliyopita tuendelee kuangalia michezo iliyo mbele yetu,” alisema Mwambusi.

Naye Kocha Mkuu wa Gwambina, Mohamed Badru alisema wataingia katika mchezo huo kwa tahadhari kubwa baada ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya KMC.

Alisema atautumia mchezo huo dhidi ya Yanga kurudisha morali katika kikosi chake.

“Nimeyafanyia kazi makosa yaliyojitokeza katika mchezo wetu dhidi ya KMC ambayo yalitugharimu na kujikuta tukipoteza mchezo kwa mabao mengi, ninawaheshimu Yanga ni timu kubwa ambayo ndiyo kinara wa ligi lakini sitokuwa tayari kupoteza michezo miwili mfululizo,” alisema Badru.

Michezo mingine ya Ligi Kuu Tanzania utakaopigwa leo, KMC watawakaribisha Biashara United katika Uwanja wa Uhuru, Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ watakuwa nyumbani katika Uwanja wa Mkwakwani kupepetana na Mtibwa Sugar kutoka Manungu mkoani Morogoro.

Chanzo: www.habarileo.co.tz