Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga kuanza na Namungo kampeni ya Ubingwa

Yanga Lomalisa Okrah Maxi Yanga kuwafuata Namungo kesho

Wed, 6 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kikosi cha Timu ya Soka ya Young Africans SC, kinatarajiwa kuondoka Dar es Salaam kesho saa 1:00 asubuhi kwa usafiri wa ndege kuelekea mkoani Lindi.

Young Africans SC inakwenda Ruangwa kupambana na Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC utakaochezwa keshokutwa Ijumaa kwenye Uwanja wa Majaliwa uliopo mkoani Lindi.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Young Africans SC, Ally Kamwe, amesema kutokana na kikosi hicho kuwa na ratiba ngumu mwezi huu Machi, ikiwemo kukabiliwa na mechi nne za Ligi Kuu ya NBC, safari ya kukusanya pointi 12 inaanzia mkoani Lindi dhidi ya Namungo.

“Habari Mwananchi, mwezi huu wa tatu kila mmoja nafikiri anafahamu ratiba ngumu inayotukabili, tuna michezo minne ya Ligi Kuu ya NBC na mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo ratiba yake inapangwa tarehe 12 mwezi huu.

“Lakini kwenye ligi hapa tuna michezo minne, tuna mechi dhidi ya Namungo ambayo tutacheza ugenini, tuna mechi dhidi ya Ihefu, tuna mechi dhidi ya Geita Gold, halafu tuna mechi dhidi ya Azam.

“Michezo hii minne jumla yake ina pointi 12, ni pointi muhimu kabisa ambazo sisi Wananchi kuanzia viongozi, benchi la ufundi, wachezaji hadi mashabiki tuna hamu kubwa ya kuzipata kwa sababu zitatuweka kwenye nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wetu msimu huu.

“Safari ya pointi hizi 12 inaanzia siku ya Ijumaa pale Ruangwa, Lindi dhidi ya Namungo, haitakuwa mechi nyepesi kwa sababu nakumbuka mzunguko wa kwanza mechi ilikuwa ngumu sana tukicheza uwanja wa nyumbani pale Azam Complex, tulibahatika kushinda goli 1-0.

“Sasa tunaenda kwenye uwanja wao na Namungo wametoka kufanya vizuri katika mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar kwa hiyo tunaamini watakuwa wamejiandaa vizuri kwenda kupata matokeo mazuri.

“Kwa hiyo sisi kama Young Africans tunataka tuingie kwa nguvu kubwa katika mchezo huo, tuingie na umoja na mshikamano na ari ya kwenda kuchukua alama tatu za ugenini.

“Kikosi cha Young Africans kinatarajiwa kuondoka Dar es Salaam siku ya kesho asubuhi majira ya saa 1:00, tutaondoka kwa njia ya ndege kutoka hapa Dar es Salaam na kwenda kushukia Nachingwea, tukishukia Nachingwea pale tutaondoka kwa basi kuingia Ruangwa.

“Kwa wale mashabiki na wanachama wa Young Africans ambao wangependa kufuatana na timu kwenda kuisapoti kitu ambacho ni kawaida kwao kutoka mikoa mbalimbali kufanya hivyo, kuna leo na kesho, panapo majaaliwa ya Mwenyezi Mungu kama mnaanza safari basi tuanze safari kwa umakini mkubwa sana kwani taarifa tulizonazo njia kidogo zimekuwa na changamoto.

“Kwa hiyo tujaribu kuwasihi madereva waendeshe kwa umakini na abiria muwe watulivu kwenye magari kwa sababu tunatamani wote mfike salama na mkifka kwa wingi wenu mnatupa ari na nguvu kubwa wachezaji wetu katika kupambana kupata matokeo mazuri,” alisema Kamwe.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live