Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga katikati ya mtego dili la Aziz Ki

Video Archive
Wed, 10 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kumbakisha Stephane Aziz Ki kunaweza kuwa habari kubwa na muhimu kwa Yanga licha ya kufanikiwa kuongeza mikataba ya wachezaji nane na pia kusaini nyota kadhaa wapya katika dirisha kubwa la usajili linaloendelea.

Kiwango bora kilichoonyeshwa na mchezaji huyo msimu uliopita, ofa zilizopo mezani kutoka kwa timu mbalimbali, historia ya kuamua matokeo ya mechi kubwa pamoja na ushawishi mkubwa alionao kwa vigogo wa timu hiyo ni mambo manne ambayo yanaishaiwishi Yanga kuhakikisha inambakisha mchezaji huyo raia wa Burkina Faso mwenye umri wa miaka 28.

Katika msimu uliomalizika, Aziz Ki alifunga mabao 21 kwenye Ligi Kuu na kupiga pasi za mwisho nane na kuiwezesha Yanga kutwaa ubingwa huku yeye akiibuka mfungaji bora na katika Ligi ya Mabingwa Afrika alihusika na mabao manne katika mechi 12, akifunga mabao mawili na kupiga pasi mbili za mwisho na kuisaidia timu yake kutinga hatua ya robo fainali.

Kiwango hicho bora kimeonekana kuzivutia timu nyingi ndani na nje ya bara la Afrika ambazo zimeonekana kuhitaji huduma yake na miongoni mwa hizo ni tatu kubwa zinazoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini, Kaizer Chiefs, Mamelodi Sundowns na Orlando Pirates ambazo kwa nyakati tofauti zimewasilisha ofa za kumhitaji Aziz Ki.

Mbali na hayo, shauku imekuwa kubwa kwa Yanga kumbakisha Aziz Ki kutokana na kumbukumbu ya kuiweka timu hiyo mgongoni katika michezo mingi dhidi ya timu kubwa tangu ilipomsajili mwaka 2022 kulinganisha na wachezaji wengine.

Kiungo huyo amefunga katika mechi tatu tofauti za watani wa jadi dhidi ya Simba ambapo kati ya hizo, mbili Yanga iliibuka na ushindi, amefunga katika mechi tatu kati ya nne za ligi dhidi ya Azam FC.

Katika msimu ambao Yanga ilitinga hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Aziz Ki ndiyo alifunga bao pekee ugenini dhidi ya Club Africain ambalo liliivusha Yanga na kuiingiza hatua ya makundi huku akifunga bao moja katika mechi ya nusu fainali dhidi ya Marumo Gallants.

Kiungo huyo pia amekuwa kipenzi kikubwa cha viongozi wengi na mashabiki wengi wa timu hiyo na miongoni mwa vigogo wa Yanga ambao wanamhusudu ni waziri wa madini, Anthony Mavunde ambaye mchezaji huyo amekuwa akimtaja kama meneja wake.

Mambo hayo manne hapana shaka ndio yanafanya mashabiki na wanachama wengi wa Yanga kuwa na hamu ya kuona mchezaji huyo anabakia klabuni hapo kwa msimu ujao na kupiga chini ofa mbalimbali ambazo zipo mezani kwake.

Kumekuwa na hisia tofauti juu ya hatima ya mchezaji huyo licha ya jana Rais wa Yanga, Hersi Said kudai kwamba bado hajasaini mkataba mpya na wanapambana kuhakikisha anabakia klabuni hapo.

"“Ni mkakati wa klabu kuhakikisha mchezaji anabaki na majadiliano yanaendelea vizuri na hapana shaka tutarudi kufanya utambulisho ingawa kuna klabu nyingi zinamhitaji mchezaji.

Hivyo majadiliano yanaendelea na ninaweza kusema kuna nafasi kubwa kwa mchezaji kubakia lakini hatujakamilisha.

“Aliweka wazi kuwa anataka kubaki unajua nilimsaini miaka miwili iliyopita na nilimsajili kutoka Asec Mimosas na nikamueleza kuhusu ‘project’ yangu na nani nataka waipeleke klabu katika ngazi za juu na akawa sehemu muhimu ya program na mpango ambao upo hi vyo majadiliano yakawa yaleyale na alisema wazi kuwa nahitaji kubaki hapa na kuipeleka Yanga katika ngazi ambazo unataka ifike.

“Lakini mpira ni biashara sasa unaweza kusema unataka kubaki lakini hali ya kifedha ikabadilisha mawazo kwa hiyo naweza kusema ni 60/40 (uwezekano wa kubaki),” alisema Hersi.

Hata hivyo kwa nyakati tofauti hivi karibuni, Aziz Ki alitoa kauli zinazoashiria kuwa atabakia klabuni hapo kwa msimu ujao.

“Dube anakuja, (Joseph) Guede yupo, nisikilize, mimi ni kiungo, nitafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanakuwa wafungaji bora. Mimi ni kiungo kwa nini niwanie ufungaji bora, kwa nini ununue straika halafu utake kiungo awe mfungaji bora.

“Mimi ahadi yangu, nina matumaini straika wa Yanga atakuwa mfungaji bora msimu ujao Mungu akipenda, lakini sio Aziz, sahau kuhusu Aziz, mimi nitatoa asisti na siyo kuwa mfungaji bora,” alinukuliwa Aziz Ki katika moja ya mazungumzo yake.

Jana kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisisitiza kuwa anahitaji kumkuta kiungo huyo kambini pindi atakapojiunga nayo na sio vinginevyo.

Kumekuwa na hisia kwamba uongozi wa Yanga umeshamalizana na mchezjai huyo na unachokifanya kwa sasa kutangaza kuwa hajasaini mkataba mpya ni kujaribu kutengeneza thamani ya tukio la utambulisho wa mkataba mpya wa mchezaji huyo.

Hisia hizo zinaweza kuthibitishwa na mmoja wa wajumbe katika uongozi wa Yanga ambaye hakupenda jina lake kutajwa ambaye alifichua kuwa Aziz Ki atakuwa kwenye kambi ya timu hiyo Afrika Kusini.

"Kambi ya maandalizi ya msimu mpya tutafanya Afrika Kusini na Aziz Ki atajiunga na timu huko hatuna wasiwasi wowote," alisema kiongozi huyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live