Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga katika mtihani, Simba katikati ya giza

Dube X Awesuuuu Yanga katika mtihani, Simba katikati ya giza

Sun, 21 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kuna fikra nyingi zinaendelea wakati huu. Kila mtu anawaza mambo makubwa. Yapo yanayowezekana na yasiyowezekana.

Baada ya usajili wa nyota kadhaa, mashabiki wa Yanga wapo katika fikra kubwa. Wanaona Yanga ikitikisa Afrika katika msimu mpya wa mashindano.

Wapo mashabiki wa Yanga wanaoona timu yao ikifika fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Wapo wengine wanaoamini kuwa kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwao itakuwa jambo jepesi.

Kwanini wanawaza hivyo? Wamefanya usajili mkubwa. Wamemchukua aliyekuwa staa wa Simba, Clatous Chama. Wamemsajili aliyekua straika tegemeo wa Azam FC, Prince Dube. Kwanini wasitambe?

Wana nyongeza ya wachezaji wengine kama Duke Abuya. Fundi wa mpira kutoka pale Kenya. Aliweka ufalme wake pale Singida. Basi wamemsajili Jean Baleke. Straika aliyetamba pale Simba. Ni mashine ya mabao. Kazi ya kufunga haijawahi kuwa ngumu kwa Baleke.

Unadhani ni usajili huu tu unawapa kiburi mashabiki hao wa Yanga? Hapana. Wana sababu za kutamba zaidi. Wamewabakisha nyota wote muhimu. Wamefanya jitihada kubwa kuhakikisha Stephane Aziz Ki anabaki. Mfungaji bora wa msimu uliopita. Alifunga mabao 21 na kutoa asisti nane. Ni mchezaji hatari.

Djigui Diarra bado yupo. Kipa mahiri zaidi wa kigeni kuwahi kucheza Ligi Kuu ya Tanzania. Kwanini wasitambe?

Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli wanaingia katika msimu wao wa pili. Wachezaji muhimu sana. Wana uwezo mkubwa wa kuwavuruga wapinzani. Wanatosha kuwapa Yanga jeuri ya kuwaza makubwa.

Kwani unadhani yameishia hapo? Hapana. Bado kocha Miguel Gamondi yupo. Kocha aliyeweka rekodi ya kugawa vipigo vizito msimu uliopita. Kuna wakati Yanga kushinda mabao matano ilionekana jambo la kawaida. Bado yupo.

Anaingia kwenye msimu wa pili. Amelifahamu zaidi soka la Tanzania. Ameongezewa wachezaji ambao aliwahitaji. Anaweza kufanya makubwa zaidi.

Ila katika fikra hizo kubwa, mashabiki wa Yanga wakumbuke kuwa huu ni mpira wa miguu. Kuna wakati mambo yanaweza kukugomea hata uwe na timu nzuri kivipi. Mifano ni mingi.

Wale Mamelodi Sundowns pamoja na usajili wa kutisha. Ina miaka mingi sasa haijaonja fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Kwanini? Ndio mpira wa miguu.

Kuna Pyramids ya pale Misri. Inafanya usajili wa kutisha kila msimu lakini bado inajitafuta. Bado haijaweza kutwaa ubingwa CAF.

Wapo Petro de Luanda wa pale Angola. Wanatumia fedha za kufa mtu kila msimu, lakini bado hawajaweza kuvuka nusu fainali. Ndio soka. Linahitaji heshima yake.

Pamoja na yote, wakati Yanga wakiwa na fikra kubwa, mashabiki wa Simba hawajui cha kuwaza. Hawana uhakika kama wataweza kuwa na timu ya kurejesha taji la Ligi Kuu katika himaya yao.

Wamesajili wachezaji 13 wapya mpaka sasa. Wengi wanaonekana wanakwenda kuingia katika kikosi cha kwanza. Wataweza kuelewana haraka na kuleta ushindani kwa Yanga na Azam? Ni ngumu kusema.

Mashabiki wa Simba hawajui wawaze nini katika Kombe la Shirikisho Afrika. Wataweza kufika robo fainali au nusu fainali? Hawajui. Wanaona timu yao ni mpya na pengine wanahitaji muda kuwaza mambo makubwa.

Kocha wao Fadlu Davids hana mafanikio makubwa katika historia yake. Hajawahi kutwaa ubingwa au kuifikisha timu mbali kwenye mechi za CAF akiwa kocha mkuu.

Japo alikuwa msaidizi pale Raja Casablanca ikishinda taji la Ligi Kuu msimu uliopita. Ana wasifu mzuri zaidi kama kocha msaidizi. Ataweza kuwapa makubwa? Hawana uhakika. Wapo gizani.

Chama ameondoka. Wapo kwenye hisia mchanganyiko kama kweli alistahili kuondoka ama la. Wanasubiri kuona maingizo mapya.

Kibu Denis hayupo kambini mpaka sasa. Kwanini? Wenyewe hawajui kwanini mchezaji wao muhimu hayupo kikosini hadi sasa. Wapo gizani.

Huu ndio mtihani mkubwa zaidi kwao. Ila mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga inaweza kuwapa fikra mpya. Wanasubiri kuona wataingiaje hapo.

Chanzo: Mwanaspoti