Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga kamili yatua Mtwara, yajigamba

60603146cf41b7c21fd93673b270538a.jpeg Yanga kamili yatua Mtwara, yajigamba

Thu, 13 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KIKOSI cha Yanga kimetua salama mjini Mtwara tayari kwa pambano lao la Jumamosi dhidi ya Namungo FC huku kocha wao, Nasreddine Nabi akisisitiza kuwa bado wanayo nafasi ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu, hivyo wanazipa uzito mkubwa mechi zilizobaki kabla ligi kumalizika.

Yanga ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 57, katika michezo 27 iliyocheza hadi sasa, watani zao Simba ndio vinara kwa sasa wakikusanya pointi 61 katika michezo 25 waliyocheza, miwili nyuma ya Yanga.

Akizungumza na gazeti hili muda mfupi kabla ya timu hiyo kwenda Mtwara kwa ndege, Nabi amewataka wachezaji wake kuweka mzaha pembeni na kupambana kadri wanavyoweza kuhakikisha wanaondoka na pointi zote tatu katika kila mchezo uliopo mbele yao.

“Najua tupo nyuma kwa pointi nne dhidi ya wanaoongoza ligi Simba, lakini hicho hakiwezi kuwa kikwazo cha kutukatisha tamaa ninachojua Yanga ni miongoni mwa timu tatu ambazo zina nafasi ya kutwaa ubingwa, hivyo lazima tupambane kwa uwezo wetu wote hadi mechi ya mwisho baada ya hapo ndio tutajua kitakachotokea,” alisema Nabi.

Kocha huyo raia wa Tunisia alisema baada ya kutofanyika kwa mchezo wao dhidi ya Simba, alifanya kikao kizito na wachezaji wake wote na kuwaleleza namna ambavyo wanatakiwa kutuliza akili na kucheza kwa hesabu mechi hizo ili kuweza kushinda na kutimiza malengo yao.

Alisema anatambua ugumu uliopo wakianza na mchezo wa Jumamosi dhidi ya Namungo na kuwataka wachezaji wake wahisi kama wanacheza mechi ya fainali ili kuhakikisha wanaondoka na pointi zote tatu, jambo ambalo alisema linawezekana kutokana na mbinu na maelekezo aliyowapa kwenye mazoezi yao.

Kocha huyo alisema anafurahi kuona kila kukicha kikosi chake kikizidi kuimarika kwa wachezaji kufuata maelekezo anayowapa mazoezini, jambo ambalo linampa matumaini ya kuiona timu hiyo ikicheza soka la kuvutia kama alivyo ahidi siku ya utambulisho wake.

Yanga inafukuzia taji la 28 msimu huu baada ya kulikosa misimu mitatu huku Simba wakilifukuzia kwa mara ya nne mfululizo baada ya hadi sasa kulitwaa taji hilo mara 21.

Chanzo: www.habarileo.co.tz