Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga isione soo, waiige tu Simba

Kuiga Pic Data Yanga isione soo, waiige tu Simba

Sat, 17 Apr 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

YANGA mambo yao bado na nafsi zao hazijakunjuka, hasa wanapoona watani zao, Simba yanazidi kuwanyookea, lakini wamepewa mchongo wa maana kwa kuambiwa kama vipi waige tu njia wanazopita watani zao ili kila kitu chao kiwe freshi.

Mchongo huo umetolewa na aliyekuwa Kocha wa Mtibwa Sugar, Thierry Hitimana aliyesema kufanya vizuri sasa kwa Simba kunatokana na usajili mzuri jambo ambalo hata Yanga wanaweza kufanya ili kuongeza ufanisi kwenye michuano ya kimataifa.

Simba kwa sasa inapeperusha vyema bendera ya Tanzania na pia Afrika Mashariki katika Ligi ya Mabingwa Afrika, jambo ambalo limemfanya Hitimana kuliambia Mwanaspoti kuwa, kwa vile soka la Tanzania limetawaliwa na klabu hizo mbili ni lazima zote ziwe na ushindani sawa.

Alisema Simba na Yanga zikiwa bora ushindani unasaidia kuchangamsha ligi na hata zikiwakilisha kimataifa zitaleta mafanikio kwa nchi kama ambavyo Simba msimu huu imefanya.

Hitimana alisema amebaini timu hizo moja ikiwa haipo vizuri kama Yanga ilivyo kwa sasa, ushindani na mvuto wa soka unapungua na kuwafanya mashabiki kukosekana viwanjani, hivyo ni lazima Jangwani wachangamke na kufuata inachofanya Simba.

“Simba na Yanga zote zikiwa zinafanya vizuri ushindani unakuwa mkubwa, lakini Simba ikiwa bora kama sasa halafu Yanga inakuwa dhaifu unakosekana kabisa na ili iwe bora kama wenzao ni lazima ifanye usajili mkubwa na mzuri ambao utakuwa na manufaa.

“Kwa kuangalia Yanga ya msimu huu ina wakati mgumu, wajipange kwa msimu ujao ili kuhakikisha wanaendana na kasi ya wapinzani wao na kuifanya ligi ichangamke,” alisema Hitimana aliyeipandisha Ligi Kuu timu ya Namungo, akitokea Biashara United.

Kuhusu soka la Tanzania kwa ujumla, kocha huyo raia wa Rwanda alisema lina mambo mengi hasa mwingiliano wa majukumu kwa viongozi. “Safari ni ndefu kama wakiendelea na mambo hayo, tofauti kabisa na huku kwetu, sisi hakuna hivi vitu kila mtu anafanya majukumu yake katika anga yake kama kiongozi anafanya yake na kama kocha anafanya yake,” alisema.

Alisema kwa sasa yupo kwao mpaka msimu ujao ndipo atatafuta timu ya kufundisha licha ya kupata ofa tatu tofauti hapa nchini ambazo hajazitaja.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz