Saa chache zijazo Yanga itakuwa kule jijini Pretoria, Afrika Kusini ikipepetana na Mamelodi Sundowns ya huko katika mechi ya marudiano ya hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ni mechi hasa na inayosubiriwa kwa hamu na wengi kutokana na matokeo ya mechi ya kwanza iliyochezwa Dar es Salaam, Jumamosi iliyopita ambapo timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana.
Matokeo ya mechi ya kwanza ambayo ilichezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, yanaiweka Yanga katika nafasi nzuri ya kusonga mbele na kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo labda yenyewe tu ishindwe kuchanga karata zake.
Katika mchezo wa leo, Yanga inaweza kubebwa na matokeo ya aina nyingi jambo ambalo linawafanya wasiwe katika presha kubwa kulinganisha na wenyeji wao Mamelodi Sundowns.
Yanga itasonga mbele ikiwa itaibuka na ushindi lakini pia hilo linaweza kutokea ikiwa itatoka sare ya mabao na miamba hiyo ya Afrika Kusini lakini kama itapata matokeo ya sare tasa, maana yake mechi hiyo itaamuliwa kwa mikwaju ya penalti.
Hali ni tofauti kwa Mamelodi Sundowns ambayo yenyewe leo ili isonge mbele itahitaji kupata ushindi ama kusubiria kupita kwa mikwaju ya penalti ikiwa mechi itamalizika bila timu hizo kufungana.
Jambo jema zaidi kwa Yanga ni kupona kwa Khalid Aucho, Pacome Zouzoua na Yao Attohoula ambao walikosa mechi ya kwanza kutokana na majeraha tofauti ambayo walipata kabla ya mechi ya kwanza.
Hata hivyo, wanapaswa kucheza kwa nidhamu kubwa katika mechi ya leo ili watimize lengo lao la kusonga mbele kwani Mamelodi ni timu nzuri na itakuwa na faida ya kucheza nyumbani.
Yanga iitumie vyema presha ya Mamelodi kupata matokeo mazuri ambayo yataifanya isonge mbele na kutinga nusu fainali ambapo itakuwa inafanya hivyo kwa mara ya kwanza kwenye mashindano hayo.