Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga ishindwe yenyewe, Simba mmmh

Yanga Kikosi.jpeg Yanga ishindwe yenyewe, Simba mmmh

Sat, 8 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kitendo cha Yanga kupangwa kukutana na Rivers United katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ni jambo la kufurahisha kwa upande wao.

Mungu awape nini tena! Kingine wakati ameshaonyesha mkono wake kwa kuwagawia Rivers United ambayo kiuhalisia wanaimudu kirahisi kulinganisha na iwapo wangekutana na Pyramids FC au USM Alger.

Asikuambie mtu bwana, Yanga huwa wana aleji kweli na timu za kutoka Uarabuni. Sio kama huwa hawashindi dhidi ya hizo timu lakini mara nyingi huwa kama wamemwagiwa maji wakicheza na timu za Kiarabu.

Na timu zenyewe sasa ambazo wamezikwepa ni Pyramids na USM Alger ambazo kwenye hatua kama hizi ukienda kucheza nazo kwao zinakufunga mabao mengi haswa ili ukiwa kwako uwe na kazi ngumu ya kupindua matokeo.

Wale Rivers United wala sio timu ngumu na sidhani kama Yanga watakuwa na sababu ya msingi ya kujitetea ikiwa watashindwa kuwatoa.

Kivumbi kipo kwa watani wao Simba ambao wao kwenye robo fainali wamepangwa kukutana na Wydad Casablanca ya Morocco.

Simba wanakutana na timu dume hasa na wanatakiwa kujiandaa vilivyo ili kuhakikisha inafanya vizuri dhidi ya mabingwa hao wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.

Siikatishi tamaa Simba lakini ili iitoe Wydad, wachezaji wake wanapaswa kujitolea vilivyo ndani ya uwanja katika dakika 180 za mechi ili kufanya vizuri dhidi ya watemi hao wa Morocco.

Wajitahidi kucheza kitimu na wahakikishe wanapunguza kufanya makosa ili kutowapa mwanya wapinzani wao kuwaadhibu kama ambavyo wamekuwa wakifanya katika baadhi ya mechi kubwa.

Yale makosa ya kusababisha penalti za kizembe au kuacha kuokoa mpira katika eneo la hatari kwa kutegea mchezaji mwingine aokoe, hayatakiwi kufanyika dhidi ya Wydad kama kweli Simba inataka kwenda nusu fainali.

Chanzo: Mwanaspoti