Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga isahau Ubingwa msimu huu

Try Again Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’

Mon, 24 Jan 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mashabiki wa Yanga wanatamba sana mitaani na mitandaoni kwa sasa wakiamini chama lao litabeba ndoo msimu huu, lakini watani wao wamewasikia na kuwajibu kwa kuwaambia ‘Msijidanganye, ubingwa unatua Msimbazi’.

Mabosi wa Msimbazi wamesisitiza licha ya kuzitema pointi 11, bado wanaamini timu yao itatetea taji kwa msimu wa tano na wapinzani wao Yanga wanaojipigia debe wasitarajie kabisa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ aliliambia Mwanaspoti, mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu bado mbichi na wale wanaoichukulia poa Simba wajiandae kushangazwa mwishoni.

Try Again alisema kipigo cha Mbeya City kilichowafanya wateme pointi tatu kwa mara ya kwanza msimu huu, kimewazindua na sasa kila mechi yao wanaishukia kwa tahadhari kubwa ili wasipoteze malengo yao ya kutetea ubingwa tena.

Simba kwa sasa inashikilia ubingwa kwa misimu minne mfululizo tangu 2018 na kama itabeba tena msimu huu itaandika rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutwaa taji la Ligi Kuu mara mbili kwa misimu mitano mfululizo.

Awali Yanga iliandika rekodi kwa kulibeba taji kwa idadi hiyo kati ya 1968-72 kisha Simba kujibu mapigo ikibeba mwaka 1976-80 na haijawahi kutokea tena timu yoyote kurudia rekodi hiyo, japo Simba kwa sasa ipo pazuri kuirudia tena.

Try Again alisema kupoteza kwao sio ishu sana kwani ndivyo soka lilivyo, lakini lengo lao bado lipo palepale kutetea taji kwa mara ya tano mfululizo na anaona nafasi hiyo wanayo kwani ligi bado mbichi kwa sasa ikiwa raundi ya 13.

“Kila timu bado ina nafasi ya kuchukua ubingwa msimu huu, hata Simba tumo kama watetezi na tumejipanga ili kuhakikisha tunabeba tena, achana na hao wanaojidanganya, misimu iliyopita kuna timu ziliongoza msimamo, ila sisi tulimaliza mabingwa,” alisema Try Again na kuongeza;

“Tumejipanga kuhakikisha hatupotezi ovyo pointi katika mechi zetu, ili kutimiza malengo, tunaamini kikosi tulichonacho tutatetea tena Inshallah.”

Simba iliyokuwa Uwanja wa Manungu jana kumalizana na Mtibwa Sugar, ipo nafasi ya pili nyuma ya Yanga, ikiwa na mechi moja ya kiporo dhidi ya Kagera Sugar itakayopigwa Jumatano ijayo kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.

Mbali na kiporo hicho, Simba imesaliwa na mechi nyingine mbili za kukamilisha duru la kwanza dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya Kwanza zote zikitarajiwa kupigwa mwezi ujao jijini Dar es Salaam.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz