Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga inavyotukumbusha zama za BBC, MSN

Aziz Chama Pacome Yanga Chama, Pacome na Aziz KI

Mon, 15 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Moja ya mijadala mikubwa nchini kwa sasa ni kitendo cha Yanga kumsajili aliyekuwa kiungo wa Simba raia wa Zambia, Clatous Chota Chama 'Triple C' aliyetua ndani ya timu hiyo baada ya kukitumikia kikosi cha wekundu kwa miaka sita.

Chama ameondoka ndani ya kikosi cha Simba alichojiunga nacho Julai Mosi, 2018 akitokea Klabu ya Lusaka Dynamos ya kwao Zambia, huku ukiwa ni uhamisho ambao haujatarajiwa licha ya mara kadhaa kuhusishwa kutua Yanga.

Alihusishwa na timu ya Wananchi mara nyingi hadi ikafikia kuzaa msemo kwamba "Chama ndiye mchezaji pekee ambaye husajiliwa na Yanga kila msimu, lakini daima anacheza Simba."

Uhamisho wa nyota huyo ni ishara tosha kwamba Yanga inataka kuendelea kufanya vizuri kuanzia michuano ya ndani na ile ya nje kwa maana ya kimataifa kwani uwepo wake na mastaa wengine waliopo kikosini unaonyesha wazi jinsi Wananchi wanavyojipanga imara.

Kitendo cha viongozi wa Yanga kumchukua Chama, ni wazi wanatukumbusha enzi za mastaa wakubwa waliochezea Real Madrid na Barcelona zote za Hispania ambazo zilitengeneza utatu maarufu ambao uliteka mashabiki wengi wa soka na kuwa kivutio.

Katika timu ya Real Madrid ilikuwa na wachezaji wengi na maarufu ndio maana kiliitwa kikosi cha 'The Galacticos' zama zile ilipowasajili kwa pamoja mastaa kama Roberto Carlos, David Beckham, Claude Makelele, Zinedine Zidane, Figo, Raul, Michael Owen na Ronaldo de Lima.

Baadaye Real Madrid ikaunda utatu maarufu ukiwa na mastaa wakubwa kama Karim Benzema, Gareth Bale na Cristiano Ronaldo uliotambulika kwa jina la utani la 'BBC'.

Kwa upande wa Barcelona nayo pia ilitengeneza kikosi imara ambacho kilizidi kutawala soka la Ulaya kwa miaka mingi japo miongoni mwa utatu maarufu uliokuwepo ni wa mastaa, Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar waliojulikana kwa jina la 'MSN'.

Achana na Real Madrid na Barcelona. Hapa Bongo tunayo Yanga, ambayo nayo usajili wake wa Chama unaifanya timu hiyo ambayo ni mabingwa mara tatu mfululizo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na mataji 30 ya ligi hiyo kwa ujumla tangu mwaka 1965, kutengeneza utatu wa 'CPA'.

CPA kitaalamu au kisomi zaidi unaweza kusema ni Certified Public Accountant au kwa ludha adhimu ya kiswahili ni Mhasibu wa Umma Aliyeidhinishwa, ila huku katika mpira wa miguu tuna maana ya Clatous Chama, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz Ki.

Uwepo wa nyota hao wakubwa katika kikosi cha Yanga, haina maana itakuwa timu isiyofungika isipokuwa ni kuonyesha jinsi gani viongozi wa kikosi hicho wanazidi kujiimarisha na kuleta ushindani kwenye michuano ya ndani na ile ya kimataifa.

Ubora wa wachezaji hao unatokana na namba ambazo wamezitengeneza katika michuano mbalimbali ambapo kwa mfano wa Chama hakuna asiyejua ubora wake na hata kitendo chake cha kwenda Yanga kimewauma hata wale waliokuwa wakisema "aondoke, amechoka ni mzee".

Katika kipindi cha miaka sita alichocheza Chama katika ardhi ya Tanzania na kikosi hicho cha Simba, amecheza jumla ya michezo 179 kwenye mashindano yote ambapo kati ya hiyo amehusika na mabao 102, akifunga 42 na kutoa asisti zilizozaa mabao 60 mengine.

Licha ya kuondoka Agosti 16, 2021 na kutimkia RS Berkane ya Morocco kisha kurejea tena Simba Januari 14, 2022 ila Chama katika Ligi Kuu Bara pekee amehusika kwenye jumla ya mabao 85 ambapo amefunga mabao 31 na kutoa asisti za mabao 54 mengine.

Rekodi zake tamu ni za msimu wa 2022/2023 alipohusika katika mabao 18, ambapo alifunga manne na kuasisti 14 na ile ya msimu wa 2020/2021 alipokuwa wa moto baada ya kuhusika na mabao 23, akifunga manane na kutoa asisti za mabao 15 mengine.

Mbali na Chama ila kuna Aziz KI ambaye amesaini mkataba mpya wa kuendelea kukitumikia kikosi hicho baada ya kutanda kwa wasiwasi kwa mashabiki wa Yanga ambao walikuwa hawajui kama nyota huyo angebakia kutokana timu kubwa zilizomuhitaji.

Aziz Ki aliyejiunga na Yanga msimu wa Julai 15, 2022 akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast, amekuwa ni mmoja wa wachezaji bora ndani ya kikosi hicho na namba zake katika miaka miwili aliyoitumikia ni wazi timu hiyo ilikuwa inamuhitaji zaidi.

Katika misimu yake miwili, Aziz Ki ameipa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo, Ngao ya Jamii mara moja, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) mara moja pia, jambo linaloonyesha ni mchezaji mkubwa ambaye ni msaada kikosini hapo.

Kiujumla amefunga jumla ya mabao 37 katika misimu yake miwili ambapo Ligi Kuu Bara amefunga 30, Kombe la Shirikisho la FA akifunga manne, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika akipachika moja wakati Kombe la Shirikisho Afrika amepachika mawili alipoipeleka hadi fainali.

Katika Ligi Kuu Bara, Aziz KI amechangia jumla ya mabao 41 katika mechi 51 alizocheza akifunga 30 na asisti 11, katika jumla ya dakika 3553 alizocheza, huku rekodi bora ikiwa ya msimu uliopita alipoibuka mfungaji bora wa Ligi.

Aziz KI aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita baada ya kufunga jumla ya mabao 21 na kutoa asisti saba na kuifikia rekodi ya aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga Mrundi, Amissi Tambwe aliyefunga idadi ya mabao kama hiyo aliyoiweka msimu wa 2015-2016.

CPA inahitimishwa na Pacome ambaye licha ya kucheza msimu wake wa kwanza tangu ajiunge na Yanga akitokea ASEC Mimosas ya kwao Ivory Coast, ila alihusika pia na jumla ya mabao 11 ya Ligi Kuu Bara, akifunga saba na kutoa asisti zilizozaa mabao manne mengine.

Uwepo wa wachezaji hao watatu ndio ambao unatengeneza utatu mtakatifu wa 'CPA' na kwa kuangalia namba za kila mmoja wao ni ishara tosha, mashabiki wa Yanga wanatamani Ligi ianze mapema kutokana na kiu ya kuwaona mastaa hao wakicheza pamoja na kina Maxi Nzengeli, Prince Dube, Jean Baleke, Mudathir Yahya, Khalid Aucho, Yao Kouassi, 'Afande' Ibrahim Bacca, Djigui Diarra na wengineo wengi.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: