Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga inavyopiga mkwanja matawini

Yanga Matawini Yanga inavyopiga mkwanja matawini

Tue, 12 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Ni Yanga yenye mipango. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya klabu hiyo hadi sasa kukusanya Sh170.2 milioni kutoka katika matawi 36.

Fedha hizo zinatokana na usajili na uhakiki wa wanachama wa klabu hiyo ambao unaendelea katika mikoa yote nchini na kama zoezi hilo lilikamilika klabu hiyo inaweza kuweka rekodi ya kuvuna mamilioni ya pesa.

Kila mwanachama wa klabu hiyo anatakiwa kujisajili Kidijitali ili kutambulika na uongozi wa klabu na kupata fursa ya kushiriki kikamilifu uchaguzi mkuu wa Yanga.

Uongozi wa Yanga, umeweka hadharani majina ya matawi 36 ambayo yamekidhi vigezo kwa kutimiza idadi ya wanachama 100 na kuendelea huku wakiyataka matawi mengine kufanya hivyo ili yatambulike ramsi.

Licha ya matawi hayo 36 kuwekwa hadharani baada ya kutimiza vigezo lakini bado idadiu ya wanachama inaweza kuongezeka ndani ya matawi hayo na hivyo kuzidi kupatia fedha klabu hiyo wakati matawi mengine mengi bado yanapambana kujisajili kidijitali ili kutimiza idadi ya wanachama kuanzia 100 na kuendelea kuiongezea kipato timu hiyo.

Kila mwanachama anayejisajili Kidijitali anachangia Sh31,000 hadi kukamilisha usajili wake ikiwa na mchanganuoa wa fomu Sh2,000 na Sh29,000 ya usajili.

Katika matawi hayo 36 yanayotambulika na klabu hiyo hadi sasa, tawi la Dodoma Makao Makuu linaongoza kwenye usajili baada ya wanachama 367 kujisajili kidijitali na kuchangia sh 11.3 milioni kwenye usajili huo likifuatiwa na tawi la Dhahabu Geita lililosajili wanachama 304 na kuchangia sh 9. 4 milioni wakati Mwanza Mjini inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na wanachama 289 na kuchangia sh 8.9 milioni.

Matawi mengine yaliyotimiza vigezo ni Kariakoo lenye wanachama 272 (sh 8.4 milioni), Morogoro mjini lina wanachama 209 (6.4 milioni), Whatsapp Makao Makuu lina wanachama 199( 6.1 milioni), Bukoba limesajili wanachama 193 (sh 5.9 milioni) wakati tawi la Viva Young International hadi sasa limesajili wanachama 192 na kuiingizia klabu hiyo fedha sh 5.9 milioni.

Tawi la Buguruni lenyewe lina wanachama 178 na kulipia usajili sh 5.5 milioni, Whatsapp Group Admins limesajli wanachama 171 sawa na sh 5.3 milioni, Airport Dodoma (wanachama 163 - sh 5 milioni , Kivule (wanachama 153 - sh 4.7 milioni), Yanga Facebook Fans (wanachama 146 - sh 4.5), Pamoja Mbezi Tanzania (wanachama 138 - sh 4.2 milioni sawa na Mwaloni Kirumba lenye wanachama 138 pia, Tunduma Momba (wanachama 131 - sh 4 milioni kama ilivyo kwa Iringa Manispaa yenye wanachama 131 pia.

Matawi mengine ni Yanga Empire Tabora lililosajli wanachama 129 na kuchangia Sh3.9 milioni, Wabishi Lindi(wanachama 127- sh 3.9 milioni), Iwawa(wanachama 123 - sh 3.8 milioni), Yanga Elite Fans (wanachama 121- sh 3.7 milioni), Yanga Kwanza Tabora(wanachama 120 - sh 3.7 milioni), Yanga Group Adimins(wanachama 118 - sh 3.6 milioni), Bunju Mweni Yanga Family (wanachama 115 - sh 3.6 milioni), Sumbawanga (wanachama 111 - sh 3.4 milioni), Mission Sengerema (wanachama 108 - sh 3.3 milioni sawa na Arusha Bus Terminal lenye wanachama 108 pia.

Tawi la Bungeni limesajili wanachama 107 na kuchangia sh 3.3 milioni kama ilivyo kwa tawi la Mafia na Mlandizi lenye wanachama 108 kila mmoja. Tawi la Ilala( wanachama 106 - sh 3.2 milioni), Uhuru Kariakoo(wanachama 105 - sh 3.2 milioni), NHIF(wanachama 103- sh 3.1 milioni), CCM mkoa(wanachama 101 - sh 3.1 milioni sawa na Bunju A lenye wanachama 101 wakati tawi la Warriors limesajili wanachama 100 na kuchangia sh 3.1 milioni.

MFIKIRWA AFUNGUKA

Mkurugenzi wa Fedha na Utawala Yanga, Haji Mfikirwa anasema muundo wa kidijitali kwa wanachama ni mzuri kwa sababu unasaidia kujua wana wanachama wangapi tofauti na ilivyo sasa.

“Hata huko nyuma klabu ilikuwa na wanachama lakini mfumo huu unakuja kuipa faida kwa kujua tuna wanachama kiasi gani wakati wowote. Kwenye mabadiliko yetu kuna kipengele cha uhusiano mzuri na wanachama,” anasema Mfikirwa.

“Kipindi cha nyuma tukiwa na La Liga (Ligi Kuu ya Hispania) na klabu ya Sevila tuliulizwa tuna wanachama kiasi gani, lakini hatukuwa na jibu kamili. Kila mtu alikuwa na jibu lake, sasa kitendo tunachofanya ni kuwa na kumbukumbu ya wanachama ambao wataweka kila kitu chao kwenye fomu.”

WANACHAMA KUNUFAIKA

Mfikirwa anasema faida ambayo wanachama wataipata ni kununua bidhaa zao moja kwa moja kutoka Yanga kwa sababu rekodi zao zitakuwapo.

“Wakijisajili na kujulikana ni rahisi kwao kupata vitu harisi vilivyo na nembo ya klabu na watakuwa na punguzo la bei wakiagiza bidhaa zao kupitia matawi ya timu,” anasema.

“Wanachama watakuwa hawapati tena jezi feki kwa sababu watakuwa wanaweka oda ya mapema kwenye jezi moja kwa moja Yanga na hii itasaidia kupata pesa,” anasema.

MATAWI KIBAO

“Matawi zaidi ya 500 yamejisajili mpaka sasa na kwenye kila tawi kunatakiwa kuwe na wanachama 100 na kwa upande wa juu ni wanachama 500. Mwitikio ni mkubwa na tunafanya hili kwa nguvu kubwa na mwisho wa siku tuje kupata viongozi,” anasema.

“Katiba inasema sio wanachama wote wanakuja kwenye uchaguzi, lakini kupitia matawi wao ndio watachagua watu wa kwenda katika uchaguzi mkubwa na mwezi wa saba tunatakiwa tuwe na viongozi wapya kwa mujibu wa katiba.”

“Tumeanza kusajili wanachama wetu na namba zinaenda vizuri. Mpaka sasa tunaona mabadiliko yanaenda vizuri na kutakuwa na mabadiliko ya kimuundo kwenye uongozi wa Yanga na lengo likiwa ni kupata muundo wa timu,” anasema Mfikirwa.

BILA ADA INAKULA KWAKO

Zamani ilikuwa ni kawaida kwa mwanachama wa Yanga kutolipia kadi yake mpaka muda wa uchaguzi mkuu ndio wengi hulipa, lakini kupitia mabadiliko suala hilo limeondolewa.

Mfikirwa anasema katiba mpya inasema mwanachama hai ni yule ambaye analipia kadi na kupitia matawi ndio itasaidia kujua uhai wa wanachama.

“Haya matawi tunataka yawe hai muda wote. Tunataka kuona uhai wa mwanachama na usipolipa ada kwa muda wa miezi sita sifa yako inaondoka. Fomu ya mwanachama kujaza gharama yake ni Sh2,000 na pesa hiyo inabaki katika tawi ili kusaidia hapohapo,” anasema Mfikirwa.

“Wanachama ambao wapo kwenye matawi watakuwa na bei punguzo ya kununua vitu halisi kutoka Yanga kwa sababu watakuwa wanapata moja kwa moja kutoka kwenye klabu. Hii itakuwa rahisi kupitia matawi kwa sababu tutakuwa tunawasiliana.”

Upande wake Senzo anasema kitendo cha kuweka rekodi ya wanachama ni sehemu ya Yanga kupata pesa kwa sababu hata wakienda kwa wafadhili wakitaja wingi wa wanachama watawapata wengi na thamani halisi ya klabu itajulikana.

THAMANI YA KLABU

Senzo anasema baada ya kukamilika kwa usajili wa wanachama watageukia upande wa thamani halisi ya klabu ili wawekezaji wapate picha kamili ya Yanga kabla ya kuweka pesa zao.

“Tutaweka thamani halisi ya Yanga na tutaita watu ambao watakuja kutusaidia kwenye kuweka sawa. Katika mchakato huu moja kwa moja kutakuwa na mabadiliko makubwa kwenye upande wa uongozi.”

Senzo anasema hakutakuwa na mwenyekiti wala makamu tena, badala yake kutakuwa na rais wa timu na hakutakuwa na cheo hicho bila kuwapo kwa uchaguzi huru ndani ya klabu.

“Kupitia matawi tutakuwa na viongozi wa matawi ambao watatoka kwa ajili ya kwenda kwenye uchaguzi huu na hili linatakiwa lifanyike ndani ya miezi sita kuanzia sasa. Jambo la kushukuru ni mabadiliko yanaendelea vizuri na lengo kuifanya timu kuwa kwenye levo nyingine,” anasema Senzo.

“Hauwezi kuwa mwanachama wa timu kama haupo kwenye tawi. Ukiwa nje ya nchi unatakiwa kuhakikisha unajisajili kwenye tawi na ukiwa huko utapokea meseji ambayo inakupa taarifa na hii imetokana na kuwekeza kwenye upande wa dijitali.”

Mtendaji huyo anafunguka zaidi na kusema mambo yote ya mabadiliko yatazidi kwenda vizuri kupitia matokeo ya uwanjani yakiwa mazuri kwa sababu vitu hivyo vinakwenda pamoja.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz