Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga inachokifanya ni mpango mkakati wa muda mrefu

Senzoo Pic Data Kaimu Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mazingisa

Fri, 22 Oct 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yanga imerejea Dar es Salaam juzi ikitokea Songea ilikoshinda mechi yake ya tatu dhidi ya KMC na kukaa kileleni. Kaimu Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mazingisa amesisitiza kwamba hawabahatishi wana mpango kazi imara.

“Nafikiri waliokuwa na wasiwasi na Yanga hii watagundua kwamba kikosi chetu kipo katika ubora mkubwa, hatushindi kwa kubahatisha tunaonyesha ubora mkubwa ndani ya uwanja,” alisema Senzo ambaye ni raia wa Afrika Kusini aliyewahi kuwa Mtendaji Mkuu wa Simba.

Senzo amesema katika mechi zao tatu za Ligi Kuu Bara licha ya kushinda lakini idara ya ushambuliaji imefunga mabao, kiungo kina ubora wa kuzuia na kutengeneza mashambulizi.

“Timu imefunga mabao manne katika mechi tatu na mabao hayo yamefungwa na washambuliaji na viungo lakini ukiangalia hata safu ya kiungo inatengeneza nafasi vizuri bila presha hii ndio timu ambayo tunaitaka.

“Hatujaruhusu bao mpaka sasa, kuna ubora ambao wanao walinzi wetu, angalia kipa wetu Diarra (Djigui) na mabeki wote, nafikiri kuna heshima ambayo tunastahili kupewa mtu anapoizungumzia Yanga na sio kuona kama tunabahatisha,” alisema

“Tuna tofauti ukiangalia hata msimu uliopita tulianza ligi kwa kasi kubwa lakini baadaye mwishoni tukapungua kasi tukakosa ubingwa, msimu huu tofauti tumeanza taratibu kidogo na kulikuwa na sababu ila muda unavyosogea tunazidi kuwa bora zaidi,” alisema.

Nabi ataka mambo mazuri

Kocha Nesreddine Nabi amesema ana furaha na kiwango kinachoonyeshwa na wachezaji wake lakini bado anaamini wanaweza kufanya vizuri zaidi endapo vijana wake watazingatia maboresho wanayoyafanya.

Jana Nabi aliwatania akiwatisha wachezaji wake kwamba wanarudi kambini mara baada ya kutua jijini Dar es Salaam ghafla wachezaji wakaonekana wanyonge lakini baadaye akawabadilishia akiwambia amewapa mapumziko ya siku moja wakaone familia zao hatua ambayo iliwafanya wachezaji kumpigia makofi.

“Tunafanya vizuri sawa lakini naamini bado tunatakiwa kuwa bora zaidi, kuna mambo tunatakiwa kuyaboresha zaidi taratibu, tunatakiwa kuongeza umakini wa kutumia nafasi ni suala la muda tu,” amesema.

Kocha Edna Lema alisema ingawa Yanga inafanya vizuri lakini bado kuna maboresho yanatakiwa kuendelea kufanyika ya kiufundi ili iwe kwenye ubora zaidi.

“Nakubaliana kwamba Yanga iko katika ubora lakini hilo halina maana kwamba hawafanyi makosa kuna mambo ya kiufundi wanatakiwa makocha kuendelea kuyafanyia kazi zaidi,” alisema Lema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live