Kuna wakati huwa hatupendi ukweli. Tunapenda kudanganyana kwa sababu tu ya ushabiki. Ni kama hili la Simba na Yanga kimataifa.
Nimeona tambo za Yanga katika michuano ya Kombe la Shirikisho. Wanatamba kuwa watafanya vizuri na kufika mbali.
Wanatamba kuwa wao ni bora kuliko timu yoyote nchini kwa sasa. Ni kweli. Matokeo ya Ligi ya ndani yanaonyesha hilo. Ni wazi kuwa Yanga iko katika kilele cha ubora wao.
Tangu msimu uliopita mpaka sasa wamepoteza mechi moja tu ya ligi. Ni rekodi bora sana. Hakuna timu nchini imewahi kufanya hivyo.
Yanga imekuwa vyema sana ndani na nje ya uwanja. Haipotezi mechi kizembe. Ni ngumu kutabiri inapoteza mchezo lini. Inapendeza sana.
Lakini ukweli ni kwamba pamoja na uimara ilionao Yanga sasa bado ina mengi ya kujifunza katika michuano ya kimataifa.
Huku kwenye mechi za CAF, Simba ina dunia yake. Imejenga ufalme ambao hautikisiki kirahisi. Ilianza ikiwa ovyo lakini imekwenda ikiimarika siku hadi siku. Sasa wamekuwa wababe hasa wakiwa nyumbani.
Baada ya miaka 15 bila kuingia hatua ya makundi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, miaka hii mitano iliyopita imebadilisha kila kitu.
Ilionekana kama imebahatisha ilipofuzu robo fainali mwaka 2019. Ni kweli haikuwa na timu imara sana kama sasa. Lakini ilikuwa na hesabu kali.
Pamoja na kufungwa 5-0 na AS Vita pale Kinshasa. Ikapigwa tena kipigo kama hicho na Al Ahly pale Cairo. Bado Simba iliweza kupenya. Iliweka hesabu kali na mipango ya kushinda nyumbani.
Tangu hapo Simba imeifanya Benjamin Mkapa kuwa ngome imara. Kila timu inayokwenda kucheza na Simba pale kwa Mkapa inakuwa na hofu. Si sehemu salama sana kucheza. Simba ikiwa kwa Mkapa inageuka Barcelona ama Bayern Munich.
Hii hesabu na uzoefu wa mashindano haya Ndio kitu ambacho Yanga inakikosa. Mpaka leo Yanga haifahamu kwanini inashindwa kutamba nyumbani inapokuja suala la mechi za kimataifa.
Imefanya kila kitu lakini bado kupata ushindi kwa Mkapa imekuwa ngumu. Haijaanza leo wala jana. Wakati Yanga imefuzu hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka 2017, ilishinda mechi moja tu nyumbani. Iliifunga MO Bejaia tu.
Licha ya Bilionea Yusuf Manji kusema mashabiki waingie bure kwenye mechi dhidi ya TP Mazembe bado Yanga ilipoteza 1-0.
Hesabu zake za nyumbani hazikuwa nzuri na ikamaliza mkiani kwenye kundi lao. Ilipofuzu tena hatua ya makundi mwaka 2018 bado hesabu zake zilikuwa vilevile. Ilishinda mechi moja tu nyumbani.
Tena huu ndio mwaka ambao ilionekana kama imepangwa katika kundi jepesi. Ilipangwa na Rayon Sports ya Rwanda, Gor Mahia ya Kenya na USM Alger ya Algeria. Lakini haikuwa na jipya. Ikaambulia matokeo yale yale.
Bahati mbaya ni kwamba mzimu huo bado unaifukuza mpaka sasa. Yanga haina uhakika wa kushinda nyumbani wala ugenini.
Ni tofauti kabisa na ilivyo Simba. Kila mtu anafahamu nguvu yao ilipo. Inashinda kwa Mkapa. Ikienda nje inatafuta sare. Inasonga mbele. Yanga inapaswa kujifunza hapo.