Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga ina kazi kwa Kagera leo

F2e9a181c0bdd8fc8902a786eafd6300 Yanga ina kazi kwa Kagera leo

Thu, 18 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

VINARA wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara Yanga leo wanashuka dimbani kuwakabili Kagera Sugar katika mchezo wa mzunguko wa 20 utakaochezwa kwenye uwanja wa Mkapa.

Mara ya mwisho kukutana timu hizo ilikuwa mzunguko wa kwanza wa ligi kwenye uwanja wa Kaitaba ambapo Yanga ilishinda bao 1-0.

Kwa miaka ya karibuni bila kujali nani bora, timu hizi zinapokutana zimekuwa zikioneshana ushindani wa hali ya juu. Yanga haitasahau msimu uliopita iliposhangazwa na timu hiyo kwa kuchapwa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

Mzunguko wa pili timu hiyo ya mitaa ya Twiga na Jangwani Kariakoo imeanza vibaya kwa sare ya bao 1-1 katika mchezo uliopita dhidi ya Mbeya City uliochezwa ugenini kwenye Uwanja wa Sokoine.

Mchezo wa leo unaweza kuwa wenye presha kwa wenyeji Yanga wakitafuta ushindi kwa nguvu kwasababu zifuatazo.

Kwanza inajua wazi ikipoteza au kupata sare inaweza kupoteza mweleko wa uongozi kutokana na presha kubwa kutoka kwa watani zao wa jadi Simba ambao wakishinda mechi mbili za viporo wanawafikia na pengine kuwashusha kwenye msimamo wa ligi kwa uwiano mzuri wa mabao.

Kingine Yanga inataka kushinda kujiweka pazuri katika mbio za ubingwa baada ya kukosa misimu mitatu mfululizo.

Bado safu yake ya ushambuliaji licha ya kutengeneza nafasi imekosa utulivu na ufanisi katika umaliziaji. Huenda wakawa wamerekebisha mapungufu yao.

Kwa upande wa Kagera Sugar ni timu isiyotabirika kuna wakati wako vizuri na muda mwingine wamekuwa wakifanya vibaya pengine ni sehemu ya michezo.

Mchezo uliopita imetoka kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Gwambina kwenye Uwanja wa nyumbani Kaitaba.

Kagera ipo katika nafasi ya 10 kwa pointi 23 ikitofautiana pointi 22 dhidi ya Yanga ilioko kileleni kwa pointi 45 katika michezo 19 kwa kila mmoja.

Timu hiyo ina wachezaji wengi vijana na mshambuliaji wao tegemeo ambaye alilelewa Yanga ni Yusuph Mhilu amekuwa na mwenendo mzuri toka msimu uliopita.

Yanga au Kagera zote zina nafasi ya kushinda mchezo huu kutegemea na aliyejiandaa vizuri dhidi ya mpinzani wake.

Michezo mingine itakayochezwa ni Mtibwa Sugar dhidi ya Ihefu kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro na Dodoma Jiji dhidi ya Coastal Union katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Chanzo: habarileo.co.tz