Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga imewasha moto, Simba iuchochee sasa

Simba X Yanga Robo Final Yanga imewasha moto, Simba iuchochee sasa

Mon, 1 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Inawezekana kabisa baadhi ya mashabiki wameshakata tamaa ya kuona moja ya timu zetu mbili zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa wa Afrika, ikisonga mbele hadi angalau hatua ya nusu fainali baada ya kumaliza mechi zao za kwanza za robo fainali zilizopigwa wikiendi iliyopita jijini Dar es Salaam.

Simba, ambayo imekuwa mzoefu katika mashindano hayo makubwa ya soka kwa ngazi ya klabu, ilikubali kipigo cha bao 1-0 nyumbani mbele ya vigogo wa Afrika, Al Ahly katika mechi iliyopigwa Ijumaa Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kwenye uwanja huo huo Jumamosi, Yanga ikalazimishwa sare ya bila kufungana na Mamelodi Sundowns, mabingwa wa mashindano mapya ya Ligi ya Afrika (African Football League, AFL).

Wakati Simba inahitaji ushindi wowote ule ili isonge mbele, Yanga inahitaji angalau sare ya mabao ili isonge mbele kwa sheria ya bao la ugenini, wakati ushindi utakuwa bonasi kwa vijana hao wa Jangwani kufika kwa mara ya kwanza nusu fainali baada ya kutofanya vizuri kimataifa kwa muda mrefu.

Kila ukiangalia mahitaji hayo kwa timu zetu unaona mlima ni mrefu kuweza kuuvuka kirahisi, hivyo kazi kubwa inatakiwa ifanywe na wahusika kabla ya mechi za marudiano zitakazofanyika Misri (dhidi ya Al Ahly) na Afrika Kusini (dhidi ya Mamelodi Sundowns).

Pamoja na hali kuwa ya kukatisha tamaa kuna mambo yaliyotokea kwenye mechi hizo mbili yanayoweza kuwajengea imani Watanzania, kuna uwezekano wa timu zetu, au moja ya timu zetu kusonga mbele.

Kwa muda mrefu wa mechi ya Ijumaa, Simba ilishinda ndani ya nusu ya Al Ahly ikisaka mbinu za kuipenya ngome na takriban mara tatu ilitengeneza nafasi za wazi, ambazo wamaliziaji hawakuzitumia vizuri. Hii inatia moyo kama uwezekano wa kutengeneza nafasi ulikuwepo, maana yake kuna uwezekano wa kutengeneza nafasi hata Cairo wakati wa mechi ya marudiano, ilimradi tu benchi la ufundi lifanyie kazi tatizo la ukosefu wa utulivu ulioonyeshwa na Saido Ntibazonkiza, Sadio Kanoute na Kibu Denis.

Ni muhimu pia Simba ijue kuna uwezekano mkubwa Al Ahly hawakucheza kwa kiwango chake kikamilifu na hivyo watataka kufunguka zaidi nyumbani, jambo linaloweza kuwa faida pia kwa Simba.

Lakini kikubwa zaidi ni saikolojia ya wachezaji kwenye mechi hiyo. Saikolojia inaweza kujengwa na benchi la ufundi katika muda wa takriban wiki watakayokuwa wakirekebisha makosa kabla ya mechi ya marudiano.

Lakini imani kwa timu wanayotakiwa kuwa nayo viongozi, wanachama na mashabiki ni kitu kikubwa kinachoweza kuwajenga vizuri wachezaji kisaikolojia na kwenda kwenye mechi ya pili wakiwa imara vichwani.

Hao mashabiki wanaohojiwa na kutoa maneno ya kukatisha tama na hata kukashifu timu, hawawezi kuweka hamasa yoyote kwa wachezaji zaidi ya kuwafanya wajione wameshamaliza kazi kwa kuwa hakuna mwenye matumaini nao.

Yanga inahitaji ushindi au angalau sare ya mabao ili iweze kuiondoa Mamelodi Sundowns, ambayo imekuwa na kiwango kizuri kimataifa katika miaka ya karibuni. Vigogo hao wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini wamekuwa wakipata ushindi nyumbani na ugenini, hivyo sare dhidi ya Yanga itakuwa imewashtua na kusababisha waanze kujipanga upya.

Kitu muhimu kinachoweza kujenga matumaini kwa Yanga ni jinsi walivyomudu kuvuruga mipango ya Mamelodi kila wakati walipotaka kupitisha mipira kwenye ukuta wa Yanga na hivyo kulazimika kutumia muda mwingi kurudisha mipira golini kwa ajili ya usalama.

Kama walijua kushambulia mfululizo kungekuwa na athari kwao, Mamelodi walitumia ujanja wa kutuliza kasi ya mpira kwa wachezaji wa kati kwenye ngome yao kutoachia mipira haraka na wakati mwingine kutembea kabisa wakisubiri washambuliaji wa Yanga wawafuate ili wafungue sehemu yao ya kiungo.

Hii haitaweza kufanyika Afrika Kusini kwa kuwa Mamelodi watataka kushinda, ingawa wakipata bao mapema wanaweza kurudia kwenye mbinu hiyo ya kupooza mpira na hasa kupoteza muda kama walivyowafanyia Al Ahly katika fainali ya AFL.

Kikubwa zaidi ni jinsi Yanga walivyopenyeza mipira na kufanikiwa kutengeneza takriban nafasi tatu za wazi zilizopotezwa na washambuliaji wake. Ngome ya Mamelodi inaruhusu mabao ndio maana hucheza kwa tahadhari kubwa wakati ikiwa na mpira, ikihofia kuwa timu ikipoteza mpira wakati ikijenga mashambulizi uwezo wa kuzuia wapinzani wasirudi kwa kasi ni mdogo.

Kingine kikubwa ni Yanga kuweza kuhimili mikiki ya Mamelodi bila ya kuwa na wachezaji wake watatu muhimu kwenye kikosi cha kwanza. Khalid Aucho, ambaye amejijengea sifa ya kuwa mtu anayeituliza timu, Pacome Zouzoua, ambaye amefunga mabao matatu muhimu kwenye mashindano hayo na Kouasi, beki imara wa kulia, hawakuwepo kwenye mechi ya Jumamosi kutokana na majeraha.

Uwezekano mkubwa ni watatu hao kuwepo kwenye kikosi kitakachoenda Afrika Kusini na kucheza mechi hiyo ya marudiano itakayofanyika Johannesburg, jambo ambalo litaongeza uimara wa Yanga.

Kwa kifupi, Yanga imeonyesha matumaini ya Tanzania kuivusha angalau timu moja hadi nusu fainali, kazi ya Simba ni kuongeza hiyo ari kwa kufanya vizuri dhidi ya Al Ahly, jambo litakaloweka hamasa kwa Yanga kufanya vizuri siku inayofuata au matokeo mazuri ya Simba ugenini baada ya kuona wenzao wakipata sare nyumbani, yatakuwa kichocheo cha Yanga kufanya vizuri zaidi.

Yanga ameuwasha moto, sasa ni kazi ya Simba kuuchochea ili mambo yawe matamu zaidi.

Chanzo: Mwanaspoti