Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga imeisha hiyoo! akili yote kwa Mkapa Oktoba 23

Yanga Yatua Sudan Yanga wana kibarua mbele ya Simba Oktoba 23

Tue, 18 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mastaa wa zamani wa Yanga, wamedai matokeo ya juzi Jumapili usiku nchini Sudan hayana uhusiano wowote na mechi ya watani wa jadi Jumapili ijayo.

Wamesisitiza Yanga kwenye mechi za ndani wameiva hivyo; “Tukutane Kwa Mkapa.”

Yanga imetolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa bao 1-0 na Al Hilal nchini Sudan na muuaji akiwa ni yuleyule Mohammed Abdulrahman aliyewafunga bao katika sare ya 1-1 jijini Dar es Salaam.

Hiyo inamaanisha kwamba Yanga italazimika kusubiri zaidi kupata nafasi ya kucheza tena makundi la Ligi ya Mabingwa baada ya mara ya mwisho kushiriki mwaka 1998, miaka 24 iliyopita!

Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, sasa wataenda kucheza dhidi ya timu za Kombe la Shirikisho Afrika kuwania kutinga hatua ya makundi ya Shirikisho.

Lakini kabla ya hilo, wanaingia kwenye mchezo dhidi ya wapinzani Simba wikiendi ijayo wakiwa na kumbukumbu ya kuwafunga Wekundu wa Msimbazi kwa mabao 2-1, mara ya mwisho walipokutana kwenye mchezo wa ufunguzi wa ligi ‘Ngao ya Jamii’ Agosti 13, mwaka huu.

Kocha na mchezaji wa zamani wa Yanga, Kenny Mwaisabula akizungumzia mchezo huo alisema timu hiyo ina kikosi kizuri chenye muunganiko mzuri tofauti na Simba inayotegemea juhudi za wachezaji binafsi.

“Yanga kwa ujumla inacheza mpira wa kiufundi japo inapowakosa nyota wake kama, Djigui Diarra au Yannick Bangala ndipo pengo lao linakuwepo, kutokana na umuhimu wao kikosini, hivyo nawapa nafasi kubwa ya kushinda,” alisema na kuongeza;

“Maandalizi ya mechi za dabi yanakuwa tofauti na wanayofanya wanapojiandaa kucheza mechi nyingine hata wanapocheza michuano ya CAF, hivyo Yanga wana nafasi kubwa ya kushinda mechi hiyo kwa matokeo yoyote waliyoyapata jana huko Sudan,” alisema Mwaisabula ambaye ni kocha wa zamani wa Bandari ya Mtwara.

Mchezaji wa zamani wa Yanga na Simba, Mohamed Banka alisema michezo ya dabi siku zote haitabiriki na kwa jinsi ambavyo ameziangalia timu zote mbili anaona ushindani utaongezeka zaidi kwani kila mmoja anataka kulinda hadhi yake.

“Timu zote ni nzuri lakini Simba tunaweza kunufaika kuliko Yanga kwa sababu wataingia kawaida tu tofauti na wapinzani wao ambao wanajiamini kutokana na matokeo yao ya mwisho,” alisema. Banka aliongeza licha ya michezo hii kutotabirika ila bado hofu yake ipo kwa Yanga kwani eneo la ulinzi wanaonekana kufanya makosa mengi binafsi kitu kinachoweza kuwapa faida Simba.

Kwa upande wa Emmanuel Gabriel ‘Batigol’ aliyewika Simba alisema licha ya Simba kuonekana kubadilika kwa siku za hivi karibuni ila bado nafasi kubwa anaipa Yanga kwani wamekuwa wakifanya vizuri mbele yao.

“Simba mbele ya Yanga bado hawajajua watokeje, wasipokuwa makini hata hii mechi watafungwa, kwani hawajifunzi, matokeo mazuri kwao ni sare. Hata ukiangalia kipindi chote cha mafanikio yao hawana matokeo mazuri mbele ya watani, wanapaswa kutuliza akili,” alisema Batgol

Hii ni dabi ya 19 kwa timu hizi kupigwa mwezi Oktoba tangu Ligi Kuu Bara ilipoasisiwa mwaka 1965 ambako kila mmoja wao ameshinda michezo sita. huku mara saba zikiwa sare.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live