Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga imefuzu, ila ina kibarua

Gamondi Chama Boka Yanga imefuzu, ila ina kibarua

Mon, 26 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yanga imetinga kibabe hatua ya kwanza ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kuwang'oa Vital'O ya Burundi kwa jumla ya mabao 10-0.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga kwenda kukutana na CBE ya Ethiopia ambayo nayo imewatupa nje ya mashindano SC Villa ya Uganda kwa jumla ya mabao 3-2. CBE ilishinda ugenini kwa mabao 2-1 kisha juzi kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Jogoo ya Kampala.

YANGA NZITO

Baada ya kushinda mchezo wa mkondo wa kwanza kwa mabao 4-0, kisha juzi kufanya kweli tena kwa ushindi wa 6-0, tafsiri fupi inayowezwa kusemwa ni kwamba Vital'O ilikuwa nyepesi kwa mziki wa Yanga ambao umesheheni wachezaji wenye vipaji vikubwa na uzoefu.

Kocha wa Yanga Miguel Gamondi ameonyesha ana kikosi kipana akibadilisha sehemu kubwa ya kikosi chake kwenye mechi hizo mbili lakini bado haikuwa kitu rahisi kwa Vital'O kufanya chochote mbele ya mabingwa hao wa soka Tanzania.

CHAMA MMOJA TU

Hakuna atakayethubutu tena kusema kiungo, Clatous Chama amezeeka, Mwamba ni yuleyule, akicheza mechi nne za mashindano akitoa asisti tano akifunga mabao mawili akiwa na mwanzo mzuri ndani ya timu yake hiyo mpya.

Chama katika mechi mbili za Ngao ya Hisani ametoa asisti moja na aliporudi katika Ligi ya Mabingwa wakati akionekana kama hataweza kuonyesha makali, lakini akafunga bao moja kila mchezo huku akitoa asisti nne.

Ilikuwa ni suala la muda tu, kwa Chama kwani alikuwa anajiunga na timu mpya ambayo ni wazi alihitaji muda ili kuweza kuingia kwenye mifumo ya kikosi hicho lakini pia kuzoeana na wenzake hatua ambayo imeimarika na ameendelea alipoishia tangu alipohama kutoka Simba.

AMADEE KIPA MZURI TU

Vital'O mafuriko ya mabao sita iliyokubali safari hiyo ilianzia dakika ya 13 baada ya beki wake Amedee Ndavyutse kupewa kadi nyekundu ya moja kwa moja kufuatia kuudaka mpira kama kipa wake wakati akiokoa shuti la kiungo wa Yanga Pacome Zouzoua akitaka kufunga.

Amadee aliiumiza timu yake kwa kuwa ni bora angeacha mpira huo uingie wavuni ili timu yake ibaki kamili uwanjani lakini maamuzi aliyoyafanya bado hayakusaidian kitu kwani Yanga ilipata bao huku Vital'O ikipungua uwanjani.

Kabla ya hapo Vital'O ilikuwa ikicheza sana nyuma lakini baada ya kadi hiyo mambo yalizidi kuwa magumu kisha baadaye tena kucheza pungufu kutokana na beki mwingine kupewa kadi ya pili ya njano iliyozaa nyekundu.

YANGA NA FEDHA ZA MAMA

Mechi mbili dhidi ya Vital'O mabosi wa Yanga wakafunga pochi zao wakitaka kuona makali ya timu yao na wakavuna sh 20 milioni kwa mechi ya kwanza ambapo kila bao likawa na thamani ya sh 5 milioni kutoka kwa ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Mchezo wa pili wakaambiwa tena hakuna bonasi kama uliona kila bao liliopokuwa linaingia wachezaji wa Yanga walikuwa wanahimizana kuwahisha mpira kati ili wavune mabao mengi na wakatengeneza mabao sita ambayo yaliwapa sh 30 milioni na kuifanya timu hiyo kuvuna jumla ya sh 50 milioni.

Wachezaji wa Yanga wanatakiwa kuendeleza njaa hiyo ya mabao isiwe tu kwa sababu ya mzuka wa fedha kwani timu yao ina nguvu ya kutengeneza ushindi mkubwa zaidi kuliko huo wa mabao sita.

KAZI IPO HAPA

Yanga isonga mbele kwa kishindo hicho lakini bado kuna eneo inatakiwa kujipanga sawasawa, hasa kwenye ukuta wao kuna makosa machache inayafanya kwa mabeki wake kushindwa kujipanga kwa kujisahau.

Yanga inapokuwa inamiliki mpira kwa muda mrefu mabeki wake wanakuwa wanapoteza umakini kumbuka bao ambalo ililiruhusu mbele ya Azam na nafasi chache za juzi ambazo zilikaribia kuwapa mabao Vital'O.

Timu hiyo sasa inakwenda kukutana na CBE ambayo inaweza isiwe na makosa kama Vital'O kama Yanga ikiendelea kufanya makosa hayo yanaweza kuiweka timu hiyo kwenye wakati mgumu kwa kuruhusu mabao ni vyema kuanzia sasa wakajipanga sawasawa.

Pia ni lazima yake ikumbuke kuwa, imekuwa na matokeo yasiyovutia mbele ya timu za Ethiopia hasa ikicheza ugenini kazi inayotakiwa kufanywa sasa kabla ya mechi hizo za kuwania kwenda makundi.

MSIKIE GAMONDI

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alichekelea timu kufuzu kwa kishindo hicho ambapo sasa anataka kurudisha hesabu zake kwenye mechi za ligi huku wakianza kuwatafuta CBE watakao kutana nao Septemba 13-15.

"Tumevuka kwa kishindo, nina furaha na namna wachezaji wangu walivyojituma kwenye mechi hizi mbili na sasa tutalazimika kusahau ushindi huu tuna mchezo wa ligi na zaidi ya hapo tunatakiwa kuanza kujipanga na mchezo dhidi ya CBE," alisema Gamondi.

Mbali na Yanga, wawakilishi wengine wa Tanzania waliosalia katika michuano hiyo ni Simba inayoanzia raundi ya pili kwa kuvaana na Al Ahli Tripoli ya Libya iliyowang'oa Uhamiaji ya zanzibar kwa ushindi wa jumla ya mabao 5-1, ikishinda awali mabao 2-0 na majuzi ikisindilia tena mabao 3-1.

Mechi hizo za raundi ya pili zitapigwa kati ya Septemba 14- 21 na washindi watafuzu hatua ya makundi ambayo Simba na Yanga msimu uliopita kila moja ilifuzu na kwenda kutolewa robo fainali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live