Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga iliomba wachezaji watatu kutoka Simba

Yanga, Simba Kukipiga Siku Moja Klabu Bingwa.jpeg Yanga iliomba wachezaji watatu kutoka Simba

Tue, 28 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Novemba 24, 2023 ilikuwa siku ya kihistoria kwa klabu ya kihistoria kwenye mashindano ya kihistoria.

Ni siku ambayo klabu ya soka ya Yanga ya Tanzania ilikuwa ikirejea kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya miaka 25.

Miamba hao walikuwa mjini Algiers nchini Algeria kukabiliana na klabu ya Belouzdad ya huko na kuambulia kipigo cha mabao 3-0.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Yanga kucheza mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa ndani ya karne ya 21. Mara ya mwisho kwao ilikuwa mwaka 1998, wakati bado tukiwa katika karne ya 20.

Kutoka 1998 hadi sasa kuna mengi yamebadilika, lakini kupitia ukurasa huu nataka kukumbusha machache yaliyotkea wakati ule.

1. UTATA WA HATUA YA YANGA Miaka 25 iliyopita taarifa zilikuwa ngumu sana kupatikana. Baada ya Yanga kushinda 8-3 kwa matokeo ya jumla (2-2 ugenini na 6-1 nyumbani) dhidi ya Coffee United ya Ethiopia, haikujulikana walifuzu kucheza hatua gani.

FAT (ambayo sasa ni TFF) ilisema lake, vyombo vya habari vilisema lake na Yanga wenyewe walisema lao.

Katibu Mkuu wa FAT wa wakati ule, Ismail Aden Rage, alisema Yanga wametinga nusu fainali na wakivuka hapo wanakwenda fainali.

Vyombo vingi vya habari vya hapa nyumbani viliandika kwamba Yanga wametinga robo fainali. Ukipata nafasi ya kukutana na baadhi ya magazeti ya wakati ule, utaona yameandika hivyo.

Yanga wenyewe wakasema wametinga hatua ya makundi kwa sababu ndivyo barua yao kutoka CAF ilivyowaambia.

Kwa ufupi maneno yalikuwa mengi mno...leo hii miaka 25, baadaye unaweza kuona namna gani ufinyu wa taarifa ulivyopelekea mkanganyiko huu.

Wakati huo hata huko duniani intaneti kilikuwa bado kitu kigeni. Kumbuka intaneti imeanza kutumika duniani mwaka 1996, miaka miwili tu kabla ya Yanga kutinga hatua ya makundi...hata huko Ulaya kilikuwa bado kitu kigeni.

Lakini kupitia nguvu ya intaneti kwa sasa, utaweza kubaini kwamba waliotoa majibu tofauti walibabaishwa na mabadiliko ya mashindano huku wao wakikosa taarifa sahihi kwa wakati.

Kwa mfano, katibu mkuu wa FAT, Ismail Aden Rage, aliposema Yanga wameingia nusu fainali na wakitoka hapo wataenda fainali, alibababishwa na muundo wa hatua ile ya makundi.

Kulikuwa na makundi mawili, A na B huku Yanga wakiangukia kundi B, na baada ya mechi zote za hatua ya makundi...hali ilikuwa namna hii.

Kwa namna mashindano yalivyoendeshwa, hakukuwa na robo wala nusu bali ilikuwa kutoka hatua ya makundi hadi fainali moja kwa moja. Na kwa kawaida kabla ya fainali huwa kuna nusu fainali...na hiki ndicho kilichomchanganya Rage. Alipojua kwamba endapo Yanga wangeongoza kundi basi wangecheza fainali, akahitimisha kwamba ile ilikuwa nusu fainali.

Yale magazeti yaliyoandika kwamba Yanga imeingia robo, yalibabaishwa na mazoea ya zamani kwamba hatua ya nane bora ilikuwa robo fainali. Itakumbukwa kwamba mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika yalianza mwaka 1997 baada ya shirikisho la soka Afrika, CAF, kubadilisha mfumo na muundo wa mashindano ya awali ya Klabu Bingwa Afrika, yalivyoanza mwaka 1964/65.

Mabadiliko haya yalileta mfumo wa makundi tofauti na zamani ambapo mashindano yalikuwa ya mtoano kuanzia raundi za awali hadi fainali. Kwa hiyo kuanzia hapo ndiyo jina pia likabadilika kutoka Klabu Bingwa Afrika na kuwa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kutokana na kukosa taarifa sahihi na kwa wakati, vyombo vyetu vikabaki na mfumo na muundo wa zamani. Ndiyo vikaripoti kwamba Yanga wametinga robo fainali.

Ni Yanga wenyewe pekee ndiyo walikuwa sahihi kwa sababu walinukuu barua waliyopata kutoka CAF iliyosema wametinga hatua ya makundi.

2. MASLAHI YA TAIFA MBELE Baada ya Yanga kutinga hatua ya makundi, zikatoka taarifa za ruhusa ya kusajili wachezaji watatu ili kuboresha kikosi kwenye hatua ya makundi. Katibu Mkuu wa FAT, Ismail Aden Rage, akawashauri Yanga wakawaombe Simba nyota wao watatu ili wawasaidie kwa maslahi ya taifa.

Nyota hao walikuwa mshambuliaji Monja Liseki, beki wa kushoto Alphonce Modest na kiungo mshambuliaji Shaaban Ramadhan. Simba hawakuwa na kinyongo, wakawaruhusu wachezaji hao kwa maslahi ya taifa. Hili ni tukio la kizalendo zaidi kimpira baina ya watani hawa wa jadi.

3. KUSHINDWA  KUSOMA MUDA Baada ya kutinga hatua ya makundi, Yanga walianzia nyumbani dhidi ya Manning Rangers ya Afrika Kusini na kutoka sare ya 1-1, huku bao la Yanga likifungwa na Monja Liseki aliyeazimwa kutoka Simba. Baada ya mechi hii Yanga wakamfukuza kocha wao Tito Mwaluvanda, aliyewapeleka hatua ya makundi.

Wakaenda kumchukua kocha wa Rayon Sports ya Rwanda, Raoul Shungu, raia wa DRC ambaye alijipatia umaarufu mkubwa Tanzania kupitia mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, yaliyofanyika Zanzibar Januari 1998.

Kocha huyo aliiongoza Rayon Sports kucheza soka safi na kutwaa ubingwa kwa kuwafunga Mlandege ya Zanzibar 2-1 kwenye fainali. Kabla ya fainali Rayon Sports walikutana na Yanga kwenye nusu fainali na kushinda 3-1.

Kama haitoshi, mwezi Machi, Shungu akakutana tena na Yanga akiwa na Rayon Sports kwenye raundi ya kwanza ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa. Mechi zote mbili ziliisha kwa sare (2-2 Rwanda na 1-1  Tanzania) na Yanga kufuzu kwa sheria la bao la ugenini.

Mpira ambao Yanga walipigiwa mara zote tatu walizokutana na Rayon Sports ya Raoul Shungu, ndiyo uliokuja kuwashawishi baadaye kumchukua kocha huyo raia wa DRC.

Kazi yake ya kwanza ikawa dhidi ya Asec Mimosas mjini Abidjan, Septemba 6, 1998. Yanga ilipoteza mchezo huu 2-1 lakini iliupiga mwingi sana na kuleta matumaini kwa mashabiki wake. Mchezo uliofuata ulikuwa dhidi ya Raja Casablaanca huko Morocco, Septemba 20.

Yanga wakatakiwa kutoka Ivory Coast kuelekea Morocco, Jumatano ya Septemba 9, saa sita usiku. Lakini wakakosea kusoma tiketi za ndege...ile saa sita usiku ya Jumatano, wao wakadhani ni usiku wa Jumatano kuamkia Alhamisi, kumbe ni usiku wa Jumanne kuamkia Jumatano.

Walipofika uwanja wa ndege wakaambiwa ndege yenu ilikuwa saa sita usiku, yaani usiku wa kuamkia leo...wakachoka. Ndege nyingine ya kutoka Ivory Coast hadi Morocco ilikuwa Jumatano inayofuata, yaani Septemba 16. Ili kujistiri, wakaenda kuomba kwa wenyeji wao Asec wawape hifadhi kwenye akademi yao hadi ikifika siku ya safari.

Yanga wakapewa hosteli za Asec ambako walikaa na watoto wa akademi. Wakati huo watoto wenyewe ndiyo walikuwa kina Kolo Toure, Aruna Didande, Bonaventure Kalou na wengine wengi ambao baadaye walikuja kuwa nyota wakubwa duniani.

4. JEZI ZA ZA TIMU YA TAIFA Novemba 8, 1998, kwenye nyasi za Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru), Yanga walikuwa wanakamilisha safari yao ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Waliwakaribisha vinara wa kundi, Asec Mimosas kutoka Ivory Coast. Kwenye msafara wa wageni alikuwemo kijana mdogo wa kuitwa Kolo Toure, ambaye miaka michache baadaye akawa nyota mkubwa duniani.

Lakini hata hivyo, Kolo alikuja kupata uzoefu tu, hakuwemo hata kwenye orodha ya wachezaji wa akiba. Yanga walicheza mchezo huu wakivaa jezi za timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, baada ya zile walizoandaa kwa ajili ya mchezo kufanana na za wageni.

Yanga waliandaa jezi za njano, na Asec hutumia jezi za njano...kuonyesha uungwana, Yanga wakakubali kubadilisha. Lakini hawakuwa na jezi zingine hivyo wakavaa jezi za Taifa Stars.

Yanga wakapoteza mchezo huu kwa mabao 3-0 na kumaliza safari yao. Waliendelea kukaa nje ya hatua ya makundi hadi mwaka huu waliporudi tena. Na mechi yao ya kwanza ikawa ya kichapo cha 3-0, kama kile kile cha mwisho waliposhiriki.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live