Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga ilinibania kwa Simba, TP Mazembe

Bahanuzi Pic Data Yanga ilinibania kwa Simba, TP Mazembe

Wed, 27 Jan 2021 Chanzo: mwanaspoti.co.tz

By Olipa AssaMore by this Author JANA tulianza makala ya mahojiano maalumu na nyota wa zamani wa Mtibwa Sugar, Polisi Moro na Yanga na kufunguka changamoto alizokutana nazo,  Leo anaendelea kuelezea mikasa yake, huku akifichua ndoto zake za kucheza Simba zilivyokatiliwa, sambamba na kubaniwa Jangwani kutua Tp Mazembe kwa dau kubwa walilotaka. Kivipi? Tiririka naye;  “Kuna siku wakati nipo kambini Yanga, nilikumbwa na tukio la ajabu, wakati nipo chumbani jioni hivi, ulikuja upepo mkali, ukaangusha dirisha, katika mazingira ambayo sikuyaelewa,” anasema na anaendelea.  “Nilienda kumwambia nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na kuniambia nikakae naye chumbani kwake. Nilifanya hivyo. Baadae wakati natoka mlangoni kwangu nikakuta soksi zilizokuwa zimepotea. Kifupi nilikumbana na mengi nisiyoweza kumaliza kuyasimulia. Ndio maana nasema wanaonisema vibaya, hawajui ukweli na wanaojua ukweli wamenyamaza kimya.”  Anasema kutokana na matukio mbalimbali ya kumtisha, yalimfanya atamani kucheza timu nyingine akakae kwa amani.  “Yanga niliifurahia mwanzoni, baadae nilikuwa naumia moyoni, mashabiki hawakujua undani wa maisha yangu zaidi ya kunituhumu kwa umalaya, ambao niliishia tu kushangaa, kiukweli hilo lilikuwa linanitesa sana,” anasema.

  ABANIWA SIMBA  Anasema wakati yupo Polisi Moro, uongozi wa Simba ulimfuata kuhitaji huduma yake, lakini tayari alikuwa ameongeza mkataba wa miaka miwili, hivyo akawa amebakiza mwaka mmoja na miezi sita, uliokuwa unamzuia kufanya mazungumzo na timu nyingine.  Anasema baada ya kuipokea ofa ya Simba, aliupigia uongozi wa Yanga kuuambia ana ofa aliyonayo bila kutaja ni timu gani, lakini alijibiwa bado yupo kwenye mipango yao.  “Waliniambia wana uhitaji na mimi, nikakataa ofa ya Simba, nikiwa likizo nikaona jina langu ni kati ya wachezaji wanaoachwa, wakavunja mkataba ambao hawajanilipa hadi leo wa mwaka mmoja na miezi sita,” anasema,  “Japokuwa Simba ilinipuuza kunisajili kabla ya kusaini Yanga kwa mara ya kwanza, alikuja kiongozi na alizungumza na mimi kwa dharau sana, ila nikashukuru Mungu kwa kila jambo,” anasema. 

AFICHUA LA MOYONI  Bahanunzi ambayee ni wa pili kuzaliwa kati ya watoto sita, anafichua siri ya moyoni mwake ndoto yake kubwa ilikuwa kucheza Simba inayoshabikiwa na wazazi wake, hivyo aliamini kupitia kipaji chake, angeweza kuwapa furaha wakati akifunga.  “Sina maana Yanga sikucheza kwa moyo, lakini nilikuwa nikirudi nyumbani nikimwambia mama hamia Yanga, alikuwa anasema nakujali sana kijana wangu na kukutakia mema ya kazi yako, ila siwezi kushabikia Yanga, hivyo mpaka leo mama yangu anakwenda uwanjani kuangalia mechi za Simba inapocheza,” anasema na anaongeza, sababu nyingine ni kucheza nje jambo ambalo kwa Simba ingewezekana tofauti na Yanga walikuwa hawaruhusu wachezaji wake kutoka.  SH600 MIL ZA TP MAZEMBE  Kuhusu dili la TP Mazembe kuyeyuka anasema.  “Wakati nipo Yanga, uongozi wa TP Mazembe ulinifuata, lakini walihitaji Sh600 milioni, kiukweli ilinishitua sana kwani wao walinisajili kwa Sh12 milioni, nikitokea Mtibwa Sugar, ni kweli nilikuwa na kipaji lakini sikucheza kwa muda mrefu wa kuhitaji kiasi kile,” anasema na anaongeza  “Zilikuja timu nyingi kutoka Misri na China, lakini ziligonga mwamba,” anasema. 

WATOTO KUCHEZA MTIBWA SUGAR  Bahanuzi ambaye ni baba wa watoto watatu aliowataja ni Samir (7), Sabra (5) na Azir (mwaka mmoja na miezi sita) anasema “Kijana wangu wa kwanza anapenda sana mpira, ninatamani siku akikua aje aanzie Mtibwa Sugar, ndipo aende timu nyingine,” anaeleza. 

KINACHOMUUMIZA  Anasema baada ya kuondoka Yanga, timu ya mwisho kuichezea ni Mtibwa Sugar msimu wa 2016/17 ambako aliumia goti la mguu wa kulia na mfupa umekaa pembeni, hivyo anajikuta goti linajaa maji.  Anasimulia kwa uchungu wa kutoa machozi, gharama za matibabu kwenda kufanya matibabu nchini Afrika Kusini zimemshinda, hivyo wakati mwingine akifanya kazi kwa muda mrefu goti linajaa maji na kumsababishia maumivu makali.  “Naumia kwasababu sijatimiza ndoto zangu kwenye soka, naishia kuwatazama wenzangu wakifanya kazi, nimehangaika sana hospitali jibu ninaloambiwa ni moja, unapaswa kwenda kufanyiwa upasuaji Afrika Kusini, najiuliza haya maji yanayojaa mguuni, itakuaje kufanya shuguli za kuendesha maisha yangu, sipati mwanga wa jibu,” anasema  Anasisitiza alichokizungumza ndio sababu ya yeye kuwa nje ya kazi ya soka na laiti kama angetibiwa angeendelea kucheza ama kwenda kusomea uchambuzi wa soka, huku akifurahishwa na umahili wa uchambuzi wa Ally Mayay na Mwalimu Alex Kashasha.  “Kama atatokea mtu mwema atanisaidia kuondoa tatizo langu ambalo nikilala na kuamka huwa nawaza sana, nashindwa kujua mwisho wangu, nitashukuru kwani natamani afya yangu kuiona inakuwa sawa,” anasema. 

STARS TATU, WATANI MOJA  Anasema kwa muda ambao alicheza Yanga aliitwa timu ya Taifa, Taifa Stars mara tatu na kucheza mechi ya watani wa jadi mara moja, huku nyingine akiwa anasugua benchi.  “Nakumbuka mechi ya watani wa jadi ambayo nilipewa nafasi ya kucheza msimu wa 2013/14 ilikuwa tafu sana, upande wa Simba golini alikaa Juma Kaseja, mabeki walikuwa Juma Nyoso, Shomary Kapombe na Masoud Nassor ‘Chollo’ hao watu walijua kukaba, lakini tulipambana iliisha sare ya bao 1-1,” anasema.  Anasema ndoto zake ilikuwa ni kuitumikia kwa muda mrefu Stars, lakini anaona haikuwa riziki aliyopangiwa na Mungu. 

Chanzo: mwanaspoti.co.tz