Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga ilijichanganya hapa kwa CR Belouizdad

Yanga Cr Belouizdad M Yanga ilijichanganya hapa kwa CR Belouizdad

Sun, 26 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kikosi cha Yanga kimesharejea nyumbani alfajiri ya leo kutoka Algeria baada ya kuanza vibaya mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayoshiriki kwa mara ya kwanza baada ya miaka 25 kupita, kwa kufungwa na CR Belouidad kwa mabao 3-0 kwenye mechi kali iliyopigwa juzi usiku jijini Algiers.

Yanga ilikumbana na kichapo hicho kwenye mchezo wa Kundi D uliopigwa Uwanja wa Julai 5, 1962 , huku Yanga ikiupiga mwingi, lakini kuna mambo yaliwaangusha mbele ya wenyeji ambao walicheza kwa nidhamu kubwa ikiwaheshimu wawakilishi hao wa Tanzania waliocheza mra ya mwisho makundi 1998.

Kwa sasa Yanga imerejea ili kujiandaa na mchezo mwingine mgumu dhidi ya Al Ahly, lakini hapa chini ni mambo kadhaa yaliyochangia miamba hiyo kupoteza kwa idadi hiyo ya mabao tofauti na matarajio ya mashabiki wengi nchini kutokana kiwango ilichonacho katika michezo ya Ligi Kuu Bara.

MABADILIKO YA KIPA

Hakuna ubishi Yanga iliathiriwa kwa kiasi kikubwa na kukosekana kwa kipa wao namba moja wa kikosi hicho, Djigui Diarra, ndiye amekuwa mhimili mkubwa katika michezo mbalimbali msimu huu tofauti na Metacha Mnata aliyeanza kwenye mchezo huo.

Kuthibitisha hilo katika mchezo wa juzi, Metacha ndiye mchezaji pekee wa Yanga aliyecheza chini ya kiwango kwani kwenye ukadiriaji kuanzia 0-10, alipata 4.9 huku Pacome Zouzoua akifunika zaidi ndani ya kikosi hicho baada ya kukusanya 7.8.

Kocha Miguel Gamondi alilazimika kumuanzisha kipa huyo, huku benchini akimweka Aboutwalib Mshery kutokana na Diarra kusumbuliwa na maumivu wa bega ambayo yalimfanya kushindwa kucheza pia kwenye mchezo na Coastal Union uliopigwa Novemba 8 na hata kutoichezea timu ya taifa ya Mali.

Tofauti na Diarra anayezungumza na mabeki wake mra kwa mara na kusogea mbele kuongezea idadi ya wachezaji kwenye lango la wapinzani, huku akiwa na uwezo mkubwa wa kutumia miguu yake kujilinda kwa Metacha hali ilikuwa tofauti, japo safu nzima ya ulinzi inastahili lawama kwa kukosa umakini kwenye mchezo huo.

HESABU ZILIKATAA

Licha ya Yanga kumiliki mchezo kwa asilimia 58 na kupiga pasi sahihi 459 tofauti na wapinzani wao Belouizdad waliomiliki kwa asilimia 42 na kupiga pasi 323 ila ilishindwa kucheza kwa hesabu hivyo kujikuta ikianza vibaya kwenye michuano hiyo.

Katika mchezo huo Yanga ilipiga mashuti manne yaliyolenga lango (shots on target) ingawa jambo la kusikitisha hakuna hata moja lililoingia nyavuni tofauti na CR Belouizdad ambayo ilipata nafasi tatu tu zilizolenga bao na kuzitumia zote vizuri.

UKABAJI MBOVU

Moja ya jambo lililoiangusha Yanga ni kushindwa kukaba vizuri wakati ikiwa haina mpira kitu kilichokuwa kinaipa nguvu wapinzani wao hasa wakichagizwa na nyota, Abdelraouf Benguit aliyekuwa mwiba kwao akifunga bao moja na kusaidia pia moja (Assisti).

Nyota wa Belouizdad baada ya kuona ni ngumu kushindana na Yanga kwenye umiliki wa mchezo waliamua kutowapa nafasi kubwa za wazi za kuwashambulia na walifanikiwa jambo ambalo kwa sasa Gamondi anapaswa kulifanyia kazi katika michezo ijayo.

NAFASI BADO IPO

Mchezo unaofuata utakuwa ni dhidi ya mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Al Ahly ya Misri ambapo endapo Yanga inahitaji kuweka matumaini hai katika kundi hilo ni lazima ipambane iwezavyo kuhakikisha inapata pointi tatu na sio vinginevyo.

Katika mchezo huo utakaopigwa Desemba 2, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, utatoa taswira halisi ya kikosi hicho cha Muargentina, Miguel Gamondi katika kundi lenye timu ya Medeama ya Ghana iliyowahi kukutana nayo 2016.

KAULI ZA WADAU

Akizungumza na Mwanaspoti mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Said Maulid ‘SMG’ anasema licha ya Yanga kupoteza ila ukweli ni kwamba wana kikosi bora msimu huu huku akifananisha kipigo hicho ni kama ilivyoanza msimu uliopitana na Klabu ya US Monastir.

“Unapocheza ugenini na kuonyesha kiwango kama kile ni ishara tosha una timu bora, Yanga ilikosa bahati tu kwenye kufunga mabao hivyo naamini nafasi ya wao kufanya vizuri ipo kwa sababu bado kundi lipo wazi na wameonyesha ina kitu,” anasema.

Kwa upande wa Kocha Msaidizi wa Biashara United, Edna Lema anasema endapo ingekuwa ni mechi ya mtoano ingekuwa ngumu kwa Yanga ila kwa kuwa ni ya makundi anaiona ikifanya vizuri kutokana na wachezaji wazuri iliyonayo msimu huu kikosini hapo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: