Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga hii jaeni kwenye boksi, mnakufa

Yanga Jaeni Box Yanga hii jaeni kwenye boksi, mnakufa

Fri, 1 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Baharini mashambulizi ya papa ndiyo ya hatari zaidi, lakini kwenye viwanja vya soka, mashambulizi ya Yanga msimu huu yameonekana kuwapa matatizo mengi wapinzani wao.

Timu nyingi msimu huu zimekutana na vipigo vikubwa vikiwamo vya 5G, ambavyo Yanga imevitoa kwa timu saba tofauti katika michuano minne tofauti kuanzia Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la ASFC na Kombe la Mapinduzi.

Kwenye Ligi Kuu Bara, timu tatu tofauti zilipigwa 5G (Simba 5-1, KMC 5-0, na JKT Tanzania 5-0), kwenye Ligi ya Mabingwa hatua ya mchujo wa kuwania kuingia makundi iliipiga ASAS Djibouti Telecom 5-1 na kwenye Kombe la Mapinduzi iliifunga Jamhuri 5-0, huku kwenye Kombe la ASFC iliifunga Hausung 5-1 na Polisi Tanzania walikula 5-0.

Kati ya vipigo vikubwa vingine ni kile cha Mtibwa Sugar waliokula 4-1, Geita Gold 3-0, KMC 3-0, Medeama 3-0 (Makundi Ligi ya Mabingwa Afrika) na kile cha kujivunia cha 2-0 ugenini dhidi ya El Merrikh katika kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kati ya vyote, kipigo kilichostua zaidi ni cha mabao 4-0 dhidi ya mabingwa mara nne mfululizo wa Ligi Kuu ya Algeria, CR Belouizdad katika mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi iliyopita Februari 24, 2024.

Yanga ilikuwa imelala 3-0 kule Algeria katika mechi yao ya kwanza ya Kundi D, ambayo timu ya Wananchi ilitawala kila kitu ugenini lakini haikuweza kufunga bao hata moja. Inaonekana kuna mbinu haikukaa sawa. Yanga ilionekana kuvurugwa na staili ya kujilinda ya CR Belouizdad. Ndio maana timu hizo ziliporudiana Kwa Mkapa, kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alionekana kurekebisha jambo katika umaliziaji. Timu ikatawala kwa staili ileile iliyofanya kule Algeria, lakini mara hii ilikuwa ikiweka mpira wavuni.

Kabla ya kwenda kuikabili Belouizdad katika mechi ya kwanza, safu ya ushambuliaji ya Yanga inayoundwa na viungo watatu, Stephane Aziz Ki, Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli na mastraika wao Kennedy Musonda na Clement Mzize, tayari ilikuwa imeshajijengea heshima ya kuwa safu hatari ya kufunga mabao mengi, ikisaidiwa na mabeki wanaopandisha mashambulizi Yao Kouassi na Lomalisa Mutambala.

Lakini kule Algeria, Yanga ilionekana kuchanganywa na staili ya CRB ya kujaza watu wengi katika kujilinda ikajikuta ifungwa mabao matatu mepesi kila wenyeji walipofanya mashambulizi ya kushtukiza.

Belouizdad walipokuja Dar wakayatimba. Kwa kutegemea staili ile ile ya kujaza watu nyuma, hakuna walichopata Kwa Mkapa zaidi ya aibu iliyowafanya wabaki kupigana wenyewe kwa wenyewe kwenye benchi lao la wachezaji wa akiba.

Safu ya ushambuliaji ya Yanga, mara hii ikiongezwa nguvu na kiungo Mudathir Yahya aliye katika ubora wa juu na usajili mpya wa straika Joseph Guede, ilionyesha kuwa imepata dawa ya staili ya Belouizdad ya kujaza watu nyuma.

Katika mabao yote manne, ambayo Yanga ilifunga Kwa Mkapa, ndani ya boksi kulikuwa na wachezaji wa Belouizdad saba! Yaani ni bao moja tu ambalo ndani ya boksi walikuwa watano. Mengine matatu yote walikuwa saba-saba ndani ya boksi.

BAO LA 1 (CRB WALIKUWA 7)

Wakati Mudathir anafunga bao la kwanza kwa kuunganisha krosi ya Lomalisa, ndani ya boksi kulikuwa na wachezaji saba wa Belouizdad, wakati wachezaji wa Yanga walikuwa watatu – Maxi Nzengeli, Musonda na mfungaji Mudathir.

BAO LA 2 (CRB WALIKUWA WATANO)

Bao hili ndilo ambalo ndani ya boksi kulikuwa na wachezaji wachache zaidi wa Belouizdad. Walikuwa watano! Ndio watano! Na wachezaji wa Yanga walikuwa watatu ndani ya boksi hilo la wapinzani, Maxi, Musonda na mfungaji Aziz Ki.

BAO LA 3 (CRB WALIKUWA 7)

Hili ni moja ya mabao bora ya wiki ya CAF yaliyotolewa na shirikisho hilo la soka Afrika. Ni bao bora kwa mashabiki wa Yanga pia. Le’ Professeur Pacome Zouzoua, aliingia kwa kasi na mpira ndani ya boksi, akamuacha beki mmoja akiogelea sakafuni, akamfuata kipa wa CRB, Alexis Guendouz, akamlambisha nyasi, akamsubiri ainuke, akamlambisha nyasi tena kasha akatoa asisti iliyowapita wachezaji kadhaa wa CRB mpira ukamkuta Musonda aliyefunga katika lango tupu. Unaweza usiamini ukiambiwa ndani ya boksi kulikuwa na wachezaji saba wa Belouizdad na watatu wa Yanga, Pacome mwenyewe, Maxi Nzengeli na mfungaji Musonda.

BAO LA 4 (CRB WALIKUWA 7)

Wakati mtokeabenchini, Guede anafunga bao la nne la Yanga, ndani ya boksi la Belouizdad kulikuwa na wachezaji saba, wakati wa Yanga walikuwa wawili tu, Aziz Ki aliyetoa asisti ya bao lile na Guede mwenyewe aliyefunga. Kiujumla Belouizdad walikiona cha moto na itakuwa vigumu kuisahau mechi ile katika maisha yao ya soka. Walitafuta mpira kwa tochi na walikula mabao ya kutosha na zaidi walikuwa na bahati kutofungwa mabao mengi zaidi ukizingatia nafasi ambazo Aziz Ki alipoteza, za Musonda na ile ya Pacome ambayo mpira ulishampita kipa lakini beki wao aliwahi na kuuosha mpira juu ya mstari wa goli kabla haujaingia nyavuni.

SIMBA 1-5 YANGA

Yaliyotokea kwa Belouizdad, hayatofautiani sana na yaliyowakuta Simba walipopigwa 5-1 Novemba 11, 2023 Kwa Mkapa. Wakati Musonda akifunga kwa kichwa bao la kwanza akimalizia krosi ya Yao Kouassi, ndani ya boksi la Simba kulikuwa na wachezaji sita wa Simba na watatu wa Yanga; Aziz Ki, Maxi na Musonda. Bao la kusawazisha la Simba lilikuwa la kona na lilifungwa kwa kichwa na Kibu. Bao la pili la Yanga lilifungwa na Maxi, lilikuwa shuti la nje ya boksi. Bao la tatu la Yanga lilifungwa na Aziz Ki akiwa peke yake wakati wachezaji wa Simba walikuwa watano ndani ya boksi. Bao la nne Maxi alifunga kwa asisti ya Mzize na walikuwa Yanga wawili tu ndani ya boksi na Simba walikuwa wanne. Bao la tano lilifungwa na Pacome kwa penalti iliyotokana na beki Henock Inonga kumwangusha Maxi Nzengeli wakati huo ndani ya boksi kukiwa na wachezaji wanne wa Simba dhidi ya wawili wa Yanga yaani Maxi na Mzize.

Takwimu za mechi Yanga v CRB

Yanga 4 – 0 Belouizdad

53.7% Kumiliki mpira 46.3%

16 Mashuti jumla 10

8 Yaliyolenga lango 2

383 Pasi sahihi 319

83.6% Usahihi wa pasi 80.6%

2 Kona 2

2 Kuotea 1

18 Madhambi 10

2 Kadi njano 1

0 Kadi nyekundu 0

Baada ya kulikosa taji la Ligi Kuu Bara kwa misimu minne mfululizo iliyokwenda kwa Simba, Yanga ilit-waa ubingwa wake wa kwanza katika miaka minne msimu wa 2021–22 bila ya kupoteza mechi hata mo-ja ikikusanya pointi 74, ilifunga mabao 49 na kuruhusu mabao manane tu. Ilitoka sare mara nane. Simba ilimaliza ya pili ikiwa na pointi 61, ilifunga mabao 41, iliruhusu mabao 14, ilishinda mechi 17, ilipoteza mechi 3 na kutoa sare 10 katika mechi 30 za ligi hiyo.

Timu ya Wananchi ilitwaa ubingwa wa pili mfululizo chini ya kocha Nasreddine Nabi msimu wa 2022-23, ikikusanya jumla ya pointi 78, ikifunga mabao 61 na kuruhusu mabao 18. Ilishinda mechi 25, sare 3 na vipigo viwili katika mechi 30 za ligi hiyo. Wapinzani wao Simba, walimaliza wa pili kwa mara ya pili mfulu-lizo wakiwa na pointi 73, baada ya kushinda mechi 22, sare 7 na kipigo kimoja tu. Na Simba hii ilikuwa inatoa vipigo vikubwa vikubwa, ilifunga mabao 75 ikiruhusu mabao 17. Yaani Simba ilikosa ubingwa wa licha ya kupoteza mechi moja tu na huku ikifunga mabao 14 zaidi ya yale waliyofunga Yanga.

Msimu huu, Yanga kama itaendelea na mwendo huu, inaonyesha dalili za kufunga mabao mengi zaidi katika michuano yote ukilinganisha ya Yanga ya misimu miwili iliyopita ambayo ilitawala soka la ndani na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kufikia sasa msimu huu, Yanga ambayo imeandika historia kwa kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza tangu mfumo wa sasa uanze kutumika 1998, inaongoza Ligi Kuu Bara baada ya mechi 16 ikiwa na pointi 43 na imefunga mabao 39, imeruhusu mabao 8, imepoteza mechi moja na kutoka sare mara moja. Inafuatiwa na Azam FC yenye pointi 37 ikiwa imecheza mechi 17 na imefunga mabao 39, sawa na Yanga, lakini Wanalambalamba wameruhusu mabao 13. Simba iko katika nafasi ya tatu ikiwa imecheza mechi 15, ina pointi 36, imeshinda mechi 11, sare tatu na imepoteza moja. Ime-funga mabao 31 na kuruhusu mabao 14.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: