Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga hii, hamtaamini, Nabi amwaga mbinu zote

Nabi Nasreddine Prof Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi

Fri, 14 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yanga tayari iko kambini na kocha wao, Nasreddine Nabi ametamka liwalo na liwe, kwani ameshajua walipojikwaa, anajifungia na wachezaji wake na kufanya kikao kizito wakichora ramani ya jinsi ya kuwavamia wapinzani wao, Al Hilal ilimradi wafuzu hatua ya makundi Afrika.

Nabi amekaa na wachezaji wake wakakosomana jinsi walivyocheza mechi ya kwanza ya michuano hiyo iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 na kocha huyo amekubaliana na mastaa wake kwamba bado wana nafasi ya kufanya vizuri.

Kocha huyo alisema atafanya mabadiliko kwenye kikosi chake kitakachoshuka uwanjani Jumapili Oktoba 16 kuanzia saa 2:00 usiku na wala hana wasiwasi na mastaa wake.

“Sisi ni familia, kuna wakati tunakutana kama familia na kuzungumza, nimefurahi kuona hata wachezaji wameniambia bado wanaiona nafasi ya kufanya vizuri Sudan na wameumizwa na matokeo ya hapa,”alisema Nabi ambaye mtihani wake mkubwa msimu huu ni kufuzu hatua ya makundi.

“Nilisema kabla tunakwenda kukutana na timu bora, lakini tulicheza kwa ubora bahati mbaya hatukutumia nafasi zetu, tunaweza kufanya mabadiliko ya baadhi ya wachezaji lakini sio kwa kiwango kikubwa.

“Tutaingia kwa nguvu ya kuipigania Yanga, wachezaji wanatambua waliwaangusha mashabiki wao, ingawa tutakuwa ugenini lakini tunaweza kufanya kitu tofauti huu ni mpira wa miguu,” alisema Nabi ambaye amewahi kuinoa El Merrekh ya Sudan ambayo ni mpinzani mkubwa wa Al Hilal.

IBENGE NA MAYELE

Kocha wa Al Hilal, Mkongomani Florent Ibenge amesema anakuna kichwa jinsi ya kumzuia straika wa Yanga, Fiston Mayele asicheze kwa ubora katika mechi ya wikiendi hii.

Ibenge alisema Mayele ambaye aliifungia Yanga bao katika sare ya kwanza, ameonyesha yuko katika kiwango bora kufunga katika mechi hiyo ya kuamua inayosubiriwa na mashabiki wengi.

“Hatujamaliza mechi, watu wanaona kama kila kitu kimekwisha, sipo huko, natafuta akili ya jinsi gani tutapunguza au kuzuia kasi ya Mayele, huyu ni mshambuliaji ambaye yuko katika kiwango bora,” alisema Ibenge ambaye aliwahi kufanya kazi na mshambuliaji huyo katika klabu ya AS Vita.

“Ukiangalia katika mchezo uliopita tulifanya makosa kidogo tu akatuadhibu, angalia maamuzi ambayo aliyafanya alizungukwa na wachezaji wangapi mpaka anafikia kufunga bao lile, hii inatosha kuwaambia mashabiki kuwa mechi bado haijaisha kila timu ina nafasi ya kwenda hatua inayofuata lakini tutapigania ushindi kwa kupambana na Yanga nzima na sio Mayele peke yake,”alisema Ibenge ambaye ana uzoefu na soka la Afrika huku akiwa amecheza fainali kadhaa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live