Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga hatulali, Al Hilal ikiwasili

Yanga Bao Pasi Kikosi cha Yanga

Thu, 6 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati kiungo wa Yanga, Stephanie Aziz Ki, ameshajiunga na kikosi cha timu hiyo, Kocha Mkuu, Nesreddine Nabi amesema anaendelea na mkakati wa kuiimarisha safu yake ya kiungo, winga na ushambuliaji baada ya kuona ubora wa wapinzani wao katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Hilal ya Sudan.

Nyota wanaotajwa kupewa majukumu ya kuhakikisha Yanga inavuna matokeo chanya ni pamoja na Tuisila Kisinda, Bernard Morrison, Jesus Moloko, Yannick Bangala, Fiston Mayele na Aziz Ki ambaye yuko tayari kwa mchezo huo wa kwanza utakaochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Hata hivyo Aziz Ki anaonekana bado hajaimarika vizuri kutokana na changamoto ya kiafya iliyokuwa inamkabili na kupelekea kuchelewa kurejea nchini baada ya kukwama Morocco alipokuwa na Timu ya Taifa ya Burkina Faso mechi za kimataifa zinazotambuliwa na Kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Nabi aliliambia gazeti hili jana ameona ubora na madhaifu ya wapinzani wao na ameyaanza kuyafanyia kazi haraka kwa ajili ya kujiweka imara na tayari kwa mchezo huo.

"Tumeongeza mazoezi na kupata mbinu wachezaji wa nafasi ya kiungo na washambuliaji, hawa ndio roho ya timu, wakifanya vizuri, tutarajie matokeo chanya, hatutatulia kwa sababu tunakutana na timu yenye uzoefu pia," Nabi alisema.

Aliongeza kikubwa wanatakiwa kuongeza umakini hasa kwenye safu ya ushambuliaji ambayo inatakiwa kutumia vyema nafasi wanazotengeneza kuanzia kipindi cha kwanza.

"Tumemaliza mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting, sasa kazi iliyobaki ni kuona mwaka huu tunatinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya muda mrefu kutofika hatua hiyo, hili litafanikiwa endapo wachezaji watajituma na kujitoa kwa dakika 90 za mwanzo.

Nimeona baadhi ya mechi za Al Hilal, wako vizuri kuanzia kwa wachezaji hadi na benchi la ufundi, maandalizi yanaendelea vizuri kwa ajili ya kujipanga kuelekea mchezo huo, tunayafanyia kazi mapungufu yetu ikiwamo kuzidisha umakini wa kutumia nafasi tunazotengeneza hasa katika kipindi cha kwanza ili kujiwekea mazingira bora na si vinginevyo," Nabi alisema.

Alisema pia anaendelea kuwasisitiza wachezaji wake kila mmoja kuwajibika kutokana na majukumu waliyopewa kwa sababu kwa kufanya hivyo watafikia malengo yao ya kupata ushindi hapa nyumbani na kwenda ugenini kumalizia dakika 90 zilizobakia.

Naye Aziz Ki alisema amerejea nchini salama na anawashukuru viongozi wa Yanga kwa kumpa ushirikiano wakati wote tangu alipopata changamoto ya ugonjwa wa Uviko-19.

"Nina matumaini makubwa tutafanya vizuri (dhidi ya Al Hilal), tunachohitaji mashabiki ni kutuunga mkono kwa kufika uwanjani, uwepo wao utakuwa chachu kubwa kwetu kuongeza bidii," alisema Aziz Ki.

Aliongeza kurejea kikosini kwa Morrison kutaongeza nguvu katika timu yao na kila mchezaji yuko tayari kuonyesha uwezo wake.

"Tunashukuru changamnoto tuliyoipata dhidi ya Ruvu Shooting, ni kama ilikuwa kipimo kizuri kwenye benchi letu la ufundi kwa ajili ya mechi inayokuja, ilibidi tuonyeshe sanaa yetu ya kushambulia na wao kuonyesha sanaa yao ya kuzuia.

"Sasa akili na mawazo nguvu zote zipo kwenye mechi ya Jumamosi dhidi ya Al Hilal, tunataka tuvunje rekodi mbaya tuliyonayo ya Yanga kutocheza hatua ya makundi barani Afrika, wengi wanatubeza wakitutolea maneno ya hapa na pale, lakini ndiyo ukweli, " Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema.

Kamwe alisema pia kikosi cha Al Hilal kinatarajiwa kutua nchini leo tayari kwa mchezo huo ambao maandalizi yake yamekamilika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live