Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga hatari zaidi ndani ya boksi CAF

YANGA 2 2t Yanga hatari zaidi ndani ya boksi CAF

Fri, 26 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kwa sasa ni Yanga pekee ndio inasubiriwa kutimiza ndoto ya kuwa klabu ya kwanza Tanzania kuleta Kombe la Afrika.

Hata hivyo wakati ikijiandaa na mechi hiyo ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuwakaribisha USM Alger kutoka Algeria, takwimu zinaonyesha mabao yao mengi wameyafunga ndani ya eneo la hatari, huku mastraika wao waliofunga mabao mengi kwenye michuano hiyo, Fiston Mayele na Kennedy Musonda pia wanaongoza kwa kutoa pasi za mwisho 'asisst.'

Takwimu za Yanga katika michuano hiyo zinaonyesha kati ya mabao 15 waliyofunga, mechi 10 ilizocheza tangu hatua za makundi, mabao 13 yamefungwa ndani ya eneo la hatari.

Ni mabao mawili pekee ambayo yamefungwa nje ya boksi, nayo ni lile alilofunga kiungo, Mudathir Yahaya Februari 19, mwaka huu walipocheza dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na kushinda 3-1 hapa Dar es Salaam.

Bao lingine la nje ya 18 lilifungwa na Mayele kwenye mechi dhidi ya Real Bamako ugenini Februari 26, mwaka huu huku timu hizo zikitoka sare goli 1-1.

Yanga inaonyesha haifungi sana mabao yake kwa vichwa, kwani ni mawili tu ambayo yamepachikwa kwa njia hiyo na mfungaji ni mmoja tu, Musonda.

Alifunga bao kwa njia hiyo kwenye mechi dhidi ya TP Mazembe hapa nyumbani na lingine akilifunga kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya US Monastir ya Tunisia, waking'ara kwa ushindi wa mabao 2-0.

Kati ya mabao 15 ya Yanga, 11 yamefungwa kwa mguu wa kulia, na manne kwa mguu wa kushoto.

Mabao ya mguu wa kushoto ya Yanga yalianza kufungwa na Mayele ugenini Yanga ikicheza dhidi ya Real Bamako katika sare ya bao 1-1, Stephane Aziz Ki akifanya hivyo timu yake ilipocheza dhidi ya Marumo Gallants Mei 10, mwaka huu nyumbani na kushinda mabao 2-0, Bernard Morrison akifunga bao kwa mguu wa kushoto kwenye mechi hiyo hiyo na Musonda akipachika bao, wakati wa mechi ya mkondo wa pili ya nusu fainali iliyochezwa Afrika Kusini, Yanga ilishinda mabao 2-1.

Takwimu zinaonyesha viungo wa Yanga hawatengenezi sana nafasi za kufunga, mastraika wao tegemeo, ndiyo wanaongoza kwa pasi za mwisho.

Kiungo pekee aliyetoa pasi ya mwisho ni Aziz Ki, akimlisha Mayele kwenye mechi ya ugenini dhidi ya Real Bamako.

Musonda ndiye kinara wa 'assist' kwenye timu hiyo, mechi za kimataifa akiwa ametoa pasi za mwisho nne, lakini pia akifunga mabao matatu mpaka sasa, hivyo kuchangia jumla ya mabao saba.

Mayele, mwenye mabao sita mpaka sasa anayeongoza katika ufungaji si kwa Yanga tu bali michuano yote, anashika nafasi ya pili kutoa pasi za mwisho, akiwa na 'assist' tatu, na kuchagia mabao tisa, na anayeshika nafasi ya tatu ni beki, nahodha wa timu hiyo, Bakari Mwamnyeto akiwa nazo mbili.

Mwamnyeto ni mchezaji pekee ya kizawa aliyetoa 'assist' kwenye michuano hiyo, nayo alizipata walipokuwa Nigeria kucheza dhidi ya Rivers United na kushinda mabao 2-0, ambapo alikuwa na kazi ya kumwekea Mayele na kutumbukiza wavuni.

Wengine waliotoa 'assist' ni Djuma Shaaban, Aziz Ki, Jesus Moloko na Tuisila Kisinda.

Hiyo inafikisha jumla ya wachezaji saba, waliochangia mabao mpaka sasa kwenye mechi 10 ilizocheza Yanga hadi kufikia mechi ya kwanza ya fainali itakayopigwa keshokutwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: