Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga hasira kwa Biashara leo

6796e2fff60752e43ec18cb08c0ac0ad.jpeg Yanga hasira kwa Biashara leo

Sat, 17 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KOCHA Mkuu wa Yanga, Juma Mwambusi amesema kuwa hasira zake wanazihamishia katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Biashara United kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam leo.

Vinara hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wanaingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu nzuri dhidi ya Biashara United, ambapo walishinda 1-0 katika mchezo wa kwanza katika Uwanja wa Karume, Musoma.

Akizungumza na gazeti hili, Mwambusi alisema kuwa maandalizi ya mchezo huo yamekamilika kikosi chake kiko vizuri wachezaji wake wanaendelea vizuri hata wale waliokosekana katika mchezo uliopita wameungana na wenzao kwaajili ya kuwakabili Biashara United.

Katika mchezo uliopita Yanga iliwakosa nyota sita , Farid Mussa, Bakari Nondo , Yasin Mustapha, Carlos Stenio Carlinhos, Haruna Niyonzima pamoja na majeruhi wa muda mrefu Mapinduzi Balama ambaye pia hivi sasa yuko katika programu maalum.

“Malengo yetu msimu huu ni ubingwa wa Ligi Kuu, hivyo tunaingia uwanjani tukiwa na lengo moja tu la kuondoka uwanjani na pointi tatu zitakazo tuwezesha kusogea zaidi kileleni mwa msimamo wa Ligi.

“Tumesahau yaliyopita hivi asa tunaangalia mbele tunaenda kufanya nini ili kurudisha imani yetu kwa mashabiki wetu ambao wana kiu ya ubingwa,” alisema Mwambusi.

Naye kaimu kocha mkuu wa Biashara United, Marwa Chamberi alisema wanaingia katika mchezo huo kwa tahadhari kubwa kutokana na matokeo waliyopata katika mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union ambao walifungwa 1-0, lakini lengo ni pointi tatu.

“Nawaheshimu Yanga ni timu kubwa yenye mashabiki wengi, lakini hilo haliwezi kutuzuia kupata pointi tatu ili tujiweke katika mazingira mazuri ya kusaka nafasi nne za juu katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, ” alisema Chamberi.

Mechi zingine leo, Coastal Union watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, huku Morogoro Mtibwa Sugar watawaalika Kagera Sugar.

Chanzo: www.habarileo.co.tz