Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

"Yanga haitobadili gia" -Nabi

Nabi Pc Data Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi

Sat, 6 Nov 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha Mkuu wa kikosi cha Yanga anafanya kazi usiku na mcha ili kuhakikisha kuwa kile walichookianza katika msimu huu wa Ligi Kuu Bara 2012/2022 hakiishii njiani.

Yanga imecheza michezo mitano mpaka sasa na imeibuka na ushindi katika michezo yote huku ikitandaza soka safi la burudani kwa wapenda kandanda nchini.

Nabi alisema anawapongeza wachezaji wake kwa kupambana na kupata ushindi katika mechi zote tano walizocheza, ikiwa ndio timu pekee iliyoshinda michezo yote mpaka sasa.

Nabi alisema matokeo ni mazuri ingawa amekiri haikuwa kazi rahisi kwa nyota wake kuvuna pointi 15 ambazo zimewaweka katika kilele cha msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 16 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini.

"Nina furaha, unapocheza mechi tano na zote ukapata ushindi, wote tunajua ligi ni ngumu, ina ushindani, timu zote zimejipanga kusaka pointi, kwa sababu hiyo hatutazubaa, tunahitaji kuona tunazidi kuimarika,” amesema Nabi.

Kocha huyo aliongeza ligi bado iko katika hatua za mwanzo, hivyo wanahitaji kuendelea kufanya vizuri kwa ajili ya kutimiza malengo yao kama ambavyo timu nyingine zilivyojipanga.

"Kila timu imejipanga, tumeanza msimu vizuri, tunahitaji kuendelea hivi hivi, tunakutana na changamoto ya kucheza kwenye viwanja tofauti, lakini hili tunakutana nalo wote, huwezi kulizungumzia, kikubwa ni kuendelea kupambana ili kupata kile tunachokitarajia," Nabi amesema.

Aliongeza ushindani wa namba kwenye kikosi chake unasaidia kuimarisha ubora wa timu na licha ya kupata ushindi kwenye mechi walizocheza, bado hakuna mchezaji mwenye uhakika wa namba kwenye kikosi cha kwanza.

"Kila mchezaji ana ubora wake, kupata nafasi ya kucheza au kutopata ni suala la wakati, kikosi kitakachoanza kinatokana na mfumo na aina ya mpinzani tunayekutana naye, kuna mchezaji mwingine anakuwa bora anapokutana na timu A, lakini huyo huyo anakaa nje unapocheza na timu B," Nabi ameongeza.

Naye Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh amesema kikosi chao kinatarajia kurejea mazoezini kwa ajili ya kujiandaa kuwafuata Namungo FC baada ya kumaliza mapumziko ya siku mbili.

"Tutaendelea na mazoezi kwa wale wachezaji ambao hawajaitwa katika timu za Taifa, tunahitaji kuwa na mwendelezo ule ule mara ligi itakaporejea, kila mchezaji anatakiwa kuwa tayari kupambana kwa ajili ya timu," alisema meneja huyo.

Namungo FC itaikaribisha Yanga katika mchezo wa raundi ya sita utakaochezwa Novemba 20, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi.

Yanga inaongoza katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara ikiwa na pointi 15, ikifuatiwa na mabingwa watetezi, Simba yenye pointi 11, Polisi Tanzania na Dodoma Jijin FC wanafuatia wakiwa na pointi 10 kila moja huku Kagera Sugar yenye pointi nane ikikamilisha 'Tano Bora'.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live