Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga ‘chovu’ ina kibarua ugenini

Yanga Chovu Yanga ‘chovu’ ina kibarua ugenini

Fri, 4 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Yanga imeendeleza mzimu wa kutokuwa sawa katika mashindano ya Afrika baada ya kulazimishwa kichovu suluhu dhidi ya Club Africain ya Tunisia katika mchezo wa hatua ya mtoano wa Kombe la Shirikisho.

Matokeo hayo yanakuja ikiwa timu hiyo ikitoka kutupwa nje ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal ya Sudan ikitoa sare ya bao 1-1 nyumbani kisha kupoteza ugenini kwa bao 1-0.

Uchovu ulionekana

Yanga imecheza mechi nne ndani ya muda wa siku 10, hii ni ratiba ngumu kuanzia Oktoba 23 walipocheza na Simba kisha siku tatu baadaye wakacheza mechi ya ligi nyingine dhidi ya KMC,wakasafiri tena mpaka jijini Mwanza kucheza na Geita ndani ya siku tatu na ndani ya muda kama huo ikashuka kucheza mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Club Africain.

Hii ni ratiba ngumu ambayo ni vigumu kwa klabu yoyote kucheza kwa ubora na kupata matokeo bora katika mlundikano wa namna hiyo.

Yanga ilionekana kuathirika na uchovu mapema tu baada ya wapinzani wao kucheza soka la kujihami na kujilinda na ilikosa ubora wa kufungua ukuta na kupata mabao kama ambavyo walikuwa wanatamani.

Ukiangalia winga Bernard Morrison, Stephane Aziz KI, Feisal Salum, Fiston Mayele walijieleza wazi jinsi ya mchoko ulivyowaathiri katika mchezo huo wa juzi, hawakuwa na utulivu kichwani wa ubunifu wa kupenya ngome ya Club Africain.

Tuisila Kisinda bado

Winga Tuisila Kisinda alistahili kutolewa mapema katika mchezo huo ni bahati kwake kumaliza dakika 45 za kwanza kutokana na kutokuwa na jipya, mtaji wake mkubwa ulikuwa na mbio na hakukuwa na nafasi ya kufanikisha hilo kutokana na wapinzani wao kutotoa nafasi.

Kisinda hakuwa na mbinu nyingine za kupenya na hata alipopata nafasi ya kutaka kukimbia mbio zake alijikuta ameshaumaliza uwanja na kuonekana wa kawaida.

Club Africain haikucheza

Club Africain ilitumia mfumo wa 4-5-1, hawakuwa na ubora kabisa wa kutaka kushambulia walicheza nyuma muda mwingi wa mchezo, walipoteza muda wanavyotaka na bahati njema kwao hawakuwa na wakati mgumu kutoka kwa mwamuzi Celso Alvacao kutoka Msumbiji ambaye alionekana kuwalea badala ya kuwaadhibu.

Nabi kwenye presha

Katika mazingira magumu kama ambayo Yanga inapitia sasa hasa katika kukosa matokeo bora lazima mtu wa kwanza kumulikwa ni kocha mkuu wa timu hiyo Nasreddine Nabi kwa kuwa Yanga inategemea ubinifu wake katika kutengeneza mbinu za kupenya katika mazingira kama hayo.

Bado wana nafasi

Ukiacha kupoteza dhidi ya Al Hilal lakini rekodi inaonyesha Yanga inacheza vizuri ugenini na hata kama itapoteza huwa wanabadilika zaidi kuliko wanavyocheza nyumbani.

Suluhu hiyo ni matokeo bora kwa Yanga kwani kama Waarabu hao watafunguka ugenini na Yanga kupata nafasi wanaweza kupata bao kwa kuwa sio timu ngumu sana itategemea na mbinu za kocha wao Nabi katika mchezo huo wa ugenini.

Kocha Nabi

Baada ya mchezo hu, kocha Nabi aliutaja uchovu kuwaathiri akisema ilikuwa vigumu kwao kupata matokeo katika mzingira magumu kama hayo, huku pia akiwataja Club Africain kuwa haikucheza kama ambavyo huwa wanacheza ugenini.

“Nilisema wiki nzima hii tuko katika mazingira magumu katika mechi zetu kutokana na ratiba hii ambayo tumeipitia ndani ya siku 11, hii ni ratiba ambayo nimeiona kwa Yanga pekee tangu nimefika hapa, nawashukuru viongozi wangu walipambana kuomba lakini imekuwa vigumu kukubaliwa, hatukuchukuliwa kama tunaliwakilisha taifa.

“Nawajua Club Africain hii ni mechi ambayo hawakucheza kabisa walikuwa wengi nyuma ya mpira walichotaka ni kuzuia tu kwa uchovu wetu kuna ubora wa ubunifu tuliukosa, tutakwenda kupambana nao ugenini.

“Mimi si kocha wa kukata tamaa wala wa mbinu za kujilinda, tutakwenda kushambulia huko huko kwao,” alisema Nabi.

Chanzo: Mwanaspoti