Ni yule yule Fiston Mayele ambaye alitoka kuiadhibu Singida BS ndiye aliyezamisha jahazi la Dodoma Jiji kwenye uwanja wa Liti na kuifanya Yanga irejee kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara huku wakiishusha Azam kwenye nafasi hiyo wote wakiwa na pointi 29, wametenganishwa na mabao.
Yanga ambayo ilitembeza boli na kuwaacha na furaha mashabiki zao ambao walijitokeza kwa wingi uwanjani hapo, imerejea kileleni huku wakiwa na mchezo mmoja mkononi tofauti na wenzao, Azam FC.
Hizi ni dondoo muhimu kuhusu mchezo huo wa Ligi ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 yote yakifungwa na Mayele.
Ulikuwa ushindi wa nne mfululizo kwa Yanga tangu mara ya mwisho kutoka sare ya bao 1-1 kwenye mchezo wa watani wa jadi.
Ulikuwa mchezo wa pili mfululizo kwenye ligi kwa Abutwalib Mshery kuanza kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga.
Mabao mawili ambayo alifunga Mayele yanamfanya kuwa kinara wa mabao Ligi Kuu Bara akiwa na mabao manane.
Kilikuwa kipigo cha nne kwa Dodoma Jiji kutoka kwa Yanga ndani ya michezo mitano tangu kupanda kwao ligi kuu, wamekuwa vibonde kwa mabingwa hao wa Kihistoria.
Yanga imeendeleza rekodi yao ya kucheza michezo mfululizo (48) kwenye ligi bila ya kupoteza, anayefuata kwenye ratiba yao ni Mbeya City.