Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga Zenji waitana kuijadili robo fainali

Yanga Tizi 135 1024x819 Yanga Zenji waitana kuijadili robo fainali

Fri, 1 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mashabiki wa Klabu ya Yanga visiwani Unguja kesho Jumamosi wanatarajia kukutana ili kuijadili timu na kuweka mipango mbalimbali ya ushiriki wa mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo timu hiyo imetinga msimu huu na usiku wa leo itakuwa uwanjani kusaka nafasi ya kumaliza kama kinara wa Kundi D mbele ya Al Ahly ya Misri.

Yanga iliyokuwa haijacheza makundi kwa miaka 25 tangu ilipofanya hivyo kwa mara ya kwanza mwaka 1998, imefuzu robo fainali baada ya kuifunga CR Belouizdad ya Algeria kwa mabao 4-0 na kufikisha pointi nane, moja pungufu na walizonazo watetezi, Al Ahly walioinyoa Medeama ya Ghana inayoburuza mkia wa kundi hilo ikiwa na pointi nne.

Kutokana na kutaka kuona timu hiyo ikiweka heshima kubwa zaidi msimu huu kwa kuvuka robo fainali, wanachama wa klabu hiyo wameitana kesho kwenye mkutano utakaofanyika Skuli ya Maungani Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi visiwani humo.

Katika mkutano huo utakaoanza asubuhi, wanachama na mashabiki wa klabu hiyo watajadili mambo mbalimbali ya kuisaidia timu kwenye mechi hizo za robo ambazo droo yake inatarajiwa kupangwa wiki ijayo.

Lengo ni kutaka kuona Yanga inavuka hatua hiyo na kusonga mbele ikiwezekana kufika hata fainali kama ilivyofanya msimu uliopita kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na kulikosa kidogo taji mbele ya USM Alger ya Algeria iliyonufaika na kanuni ya bao la ugenini, kwani matokeo ya mwisho yalikuwa sare ya mabao 2-2, Yanga ikipasuka nyumbani 2-1 na kushinda ugenini bao 1-0 kwa bao la penalti la beki Djuma Shaban ambaye hayupo na timu hiyo.

Katibu wa tawi la Yanga hilo la Maungani, Othman Mohammed, amesema katika mkutano huo pia watagawa kadi kwa wanachama waliojiandikisha mwezi uliopita na watawasajili wengine wapya.

"Kama tunavyojua timu yetu imeingia kwenye hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika, ni hatua muhimu kwetu kwa hiyo wanachama wana mchango pia wa kuipeleka timu yetu hatua nyingine," amesema Othman na kuongeza:

"Lengo ni kuisapoti timu yetu kama tunavyojua kwa sasa viongozi wanaopambana kwa hali na mali kutaka kujenga uwanja wa kisasa kama tulivoona ramani, hivyo hayo yatimie ni lazima tuungane."

Othman amesema ni vyema mashabiki wa klabu wajitokeze kwa wingi na kama kweli wanaipenda timu yao basi waende kujisajili kuwa wanachama rasmi.

Amesema baada ya zoezi hilo la kugawa kadi za wanachama na kusajili wanachama wapya, ndipo sasa watatumia muda mrefu wa kujadili mikakati mbalimbali kwa ajili ya mechi hizo za robo fainali, wakilenga kutaka kuvunja rekodi iliyofanywa kwa misimu minne kati ya mitano ikicheza hatua hiyo, lakini ikikwamia hapo hapo.

"Tunataka kuleta heshima na rekodi mpya, hatutaki kuishia wanapoishia wenzetu, tunataka twende mbali zaidi kwenye michuano hiyo, kwani tuna kikosi bora na kocha mwenye mbinu zinazotupa matumaini, ndio maana nasi tunataka tutoe mchangio wetu," amesema Othman.

Chanzo: Mwanaspoti