BENCHI la ufundi la Yanga, limechungulia kasi ya wapinzani wao kwenye vita ya ubingwa, Simba, na kushtukia jambo, ambapo wameweka mkakati wa kuhakikisha hawapotezi pointi katika michezo yao ijayo, bali wanapambana kuongeza pengo la pointi kati yao.
Yanga ndio vinara wa msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi zao 39 walizokusanya katika michezo 15 waliyocheza mpaka sasa, ambapo juzi Jumatano waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar.
Msimu huu, Yanga imekuwa kwenye kiwango bora ambapo mpaka sasa ndiyo timu pekee ambayo bado haijapoteza mchezo kwenye Ligi Kuu.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedrick Kaze, alisema: “Ni kweli bado mapema sana kuzungumzia masuala ya ubingwa kwa sasa, lakini ni wazi kila mtu anajua kuwa msimu huu tuna malengo ya kuwa mabingwa wa Ligi Kuu.
“Tunajua kuwa katika malengo haya tunakumbana na upinzani mkubwa kutoka kwa wapinzani wetu, hususan Simba ambao wanatufuatia kwenye msimamo, hivyo hatupaswi kufanya makosa ya kupoteza tena pointi.
“Tunapaswa kuhakikisha tunashinda kwenye kila mchezo ulio mbele yetu, ili kuongeza ukubwa wa pengo la pointi kati yetu, nao wanaonekana kuzidi kuimarika.