Hata kama huipendi Yanga itakapofika saa 1:00 usiku kuna utulivu utautengeneza kufuatilia hata kwa siri kipi kinaendelea pale Uwanja wa Benjamin Mkapa wakati watakapokuwa wanamaliza na wageni wao Rivers United ya Nigeria kwenye mchezo wa marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mashabiki wa Yanga watakaokuwa uwanjani huenda wakawa na bahati ya kuwa uwanjani wanaweza kuingia kwenye kitabu cha kumbukumbu kuishuhudia timu yao ikitinga hatua ya nusu fainali ya kwanza kwenye uhai wa wa klabu hiyo.
Yanga inahitaji ushindi wowote au hata sare kutinga nusu fainali baada ya kuwafunga Rivers kwao kwenye mchezo wa kwanza ka mabao 2-0 wakilipa kisasi cha kwanza dhidi ya Wanaigeria hao.
Wenyewe Yanga wanasema bado kisasi hicho hakijakamilika wakitaka kuwafunga wapinzani wao na hapa pia baada ya Rivers kuwafunga Yanga miaka miwili iliyopita hatua ya mtoano wa awali wa Ligi ya Mabingwa mecho zote mbili matokeo yakimalizika kwa Yanga kupoteza kwa bao 1-0.
Wananchi wanataka kushinda mechi hii ya leo kupeleka kilio kikubwa kwa Rivers kuwa tuliwaondoa katika hatua kubwa na pia mkapokea kipigo zaidi ya kile chenu, hayo yataonekana uiwanjani baadaye.
Baada ya kurudi kutoka Nigeria Jumanne alfajiri kikosi kamili kiliingia kambini haraka siku moja baadaye kuanza kujiandaa na mchezo huo kwa takribani siku nne huku viongozi wao na hata makocha wakisisitiza kwamba wamefuta matokeo ya ushindi a ugenini ili usiwaondoe kwenye utulivu wa kutotaka kushinda nyumbani.
Yanga inaonekana kuchukua tahadhari zote kuhakikisha wapinzani wao hawapindui meza hapa nyumbani ambapo kambini kwao wamekuwa wakijiandaa kusaka uimara wa safu yao ya ulinzi lakini pia kule mbele kunoa makali yao ya kusaka mabao yatayowapa ushindi.
Habari njema kw mashabiki wa Yanga ni kwamba ukiondoa kipa wao Aboutwalib Mshery ambaye ni majeruhi wa muda mrefu wachezaji wao wengine wote wako salama ni uamuzi wa benchi la ufundi watachagua mastaa gani watakaoikamilisha historia yao.
Tayari tajiri wao namba moja Ghalib Said Mohamed 'GSM' hakutaka kuchelewa ameshatangaza kuwa kuna sh 300 milioni mezani wakimaliza kwa ushindi mchezo huo huku pia zile fedha za hapo kwa hapo kutoka wa Rais Samia Suluhu Hassan zikiendelea ni uamuzi wao Yanga kushinda ngapi.
Shirikisho la Soka Afrika CAF wao kupitia idara yao ya mashindano imeshaweka bayana kuwa mchezo huo utasimamiwa na waamuzi wote kutoka Morocco akiwemo mwamuzi wa kati Redouane Jiyed akisaidia na msaidizi wake wa kwanza Lahsen Azgaouna wa pili ni Mostafa Akarkad huku mwamuzi wa akiba akiwa Jalal Jayed.
Takwimu zinaonyesha Jiyed ambaye amecheza jumla ya mechi 17 za kimashindano hana historia ya kutoa kadi nyekundu kwa timu mwenyeji akiwa amecheza mchezo mmoja wa shirikisho msimu huu wa hatua ya makundi kati ya Marumo Gallats ya Afrika Kusini dhidi ya FC Lupopo na wenyeji kushinda kwa mabao 3-2.
Kocha wa Yanga Nabi akizungumzia mchezo huo alisema wamekuwa katika msisitizo mkubwa wa kuondoa ushindi wao wa kwanza kwenye akili za wachezaji wao na kufanikiwa ambapo sasa wanakwenda kutafuta ushindi mwingine nyumbani.
Nabi alisema licha wao kushinda ugenini lakini bado Rivers sio timu nyepesi na kwamba makosa ya kubaki na matokeo ya kwanza ni kujaribu kuondoa sapraizi wanayoweza kukutana nayo kwa kupoteza wakiwa nyumbani.
"Kuna wakati mchezo wa soka unakuwa na maajabu yake, unapoamini sana umeshinda utakutana na mshtuko ambao utakuondoa kwenye malengo yako, unajua tulishinda kweli ugenini lakini sisi makocha tunajua kwamba Rivers bado ina kitu ambacho inaweza kufanya hapa kwetu na wakashinda,"alisema Nabi.
"Tunawaheshimu Rivers na tutaingia uwanjani kutaka kushinda kwa dhamira kubwa, nimefurahia mazoezi yetu tangu turejee nchini,kambini kumekuwa na morali kubwa, tutakuwa mbele ya mashabiki wetu bora tunakwenda kupambana kushinda hiki ndicho naweza kusema."
Staa wa Yanga mshambuliaji Fiston Mayele mwenye mabao manne msimu huu Afrika, akiwa katika kiwango chake bora anarudi uwanja wa nyumbani akiwatisha Rivers kufuatia kuwatungua mabao mawili katika kipigo chao cha kwanza Mkongomani huyo akisaka rekodi nyingine ya kuendelea kuibeba timu yake.
Rivers wao kuna akili ni kama wamekata tamaa wakidai safari yao ya kutua nchini imekubwa na mazingira ya ukata maneno ya kocha wao Stanley Eguma kauli ambayo Yanga hawataki kuamini wakidai 'anacheza na akili zetu'.
Yanga inajua kuwa Rivers haikuwatumia wachezaji wao watatu muhimu wakieleza walikuwa majeruhi na kama mshambuliaji wao Paul Acquah atakuwa tayari kwa mchezo huo anaweza kurudisha uhai wa safu yao ya ushambuliaji.
Acquah raia wa Ghana amefanikiwa kufunga mabao manne katika mechi 6 za hatua ya makundi yakiwemo mabao matatu Hat trick aliyoipiga nyumbani aliyowapiga Motema Pembe wakishinda kwa mabao 3-1 endapo atacheza leo safu ya ulinzi ya Yanga itatakiwa kuwa naye makini asije watibulia shughuli.