Mashabiki wa Yanga, wamepata ubaridi baada ya jana kushuhudia chama lao likilala nyumbani kwa mara ya kwanza katika michuano ya CAF msimu huu, lakini timu hiyo bado ina nafasi ya kipindua meza kutokana na rekodi kuwabeba ugenini.
Kikosi cha Yanga kilikumbana na kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa USM Alger ya Algeria katika pambano la kwanza la fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, lililopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Aymen Mahious na Islam Merili katika dakika ya 32 na 84 yalitosha kuipa kazi ngumu Yanga kwa mchezo wa marudiano utakaopigwa Juni 3, 2023 jijini Algers, Algeria.
Bao la kufutia machozi la Yanga lilifungwa na Fiston Mayele dakika ya 82, likiwa la saba kwake kwenye michuano hiyo ya Shirikisho, akijiweka katika nafasi nzuri ya kubeba tuzo ya Mfungaji Bora.
Licha ya kipigo, rekodi ya mechi za ugenini ilizocheza Yanga katika michuano hiyo kwa msimu huu kuanzia play-off inawabeba.
Katika mechi sita ilizocheza Yanga ugenini kuanzia hatua hiyo imepoteza mchezo mmoja tu na kutoka sare moja pia, na zilizobakia zote ilitoka na ushindi.
Yanga ilianza kwa kuifunga Club Africain ya Tunisia kwa bao 1-0 katika play-off, kisha ikapoteza mechi ya kwanza ya makundi dhidi ya US Monastir pia ya Tunisia, ikatoka sare ya 1-1 na Real Bamako ya Mali na ikashinda 1-0 dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo, ikaifunga Rivers United kwa mabao 2-0 kwenye robo fainali, kisha ikaichapa Marumo Gallants ya Afrika Kusini pia 2-0 hatua ya nusu fainali.
Hata hivyo, Yanga itakuwa na kazi ya ziada kuitibulia USM Alger ambayo katika mechi saba za CAF msimu huu haijapoteza wala kupata sare nyumbani.
Wanafainali hao wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu wa 2015, katika mechi hizo saba za nyumbani imefunga mabao 16 na kuruhusu nyavu zao kuguswa mara mbili kuonyesha ilivyo ngumu kufungika kwao.
Hata hivyo, rekodi ya Yanga kufunga ugenini na ikiwa na Mayele, Kennedy Musonda na Stephane Aziz Ki inawabeba zaidi kwani katika mechi sita kuanzia play-off imefunga jumla ya mabao saba ikiwa na wastani wa kila mechi bao moja.
Pia imeruhusu mabao mawili tu, kuonyesha ukuta wao ugenini ni imara kama inapokuwa nyumbani.
Kwa dakika 90 ilizonazo Yanga katika mechi ya marudiano ya fainali dhidi ya USM Alger, Inahitaji ushindi wa mabao 2-0 au 3-2 ili ibebe taji au ishinde 2-1 ili mechi iende kwenye matuta, japo bado rekodi baina yao na wenyeji inawapa ugumu kwani ilipokutana nao katika makundi ya michuano hiyo mwaka 2018, Vijana wa Jangwani ilichapwa mabao 4-0 kabla ya kulipa kisasi jijini Dar kuwa kushinda 2-1 na jana ilikuwa mara ya kwanza kuchapwa nyumbani na timu hiyo na cha kwanza msimu huu. Ngoja tuone hiyo Jumamosi timu hizo zitakaporudiana.