Meneja wa Klabu ya Young Africans, Walter Harson, amezungumzia hali ya kikosi hicho baada ya kufika nchini Misri na kufanya mazoezi ya kwanza.
Young Africans SC ipo nchini Misri kwa ajili ya mchezo wa mwisho katika Kundi D la michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo itacheza dhidi ya Al Ahly, keshokutwa Ijumaa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo.
“Habari Mwananchi, hapa ni Cairo International Stadium, uwanja ambao utachezwa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Al Ahly dhidi ya Young Africans keshokutwa siku ya Ijumaa, tukiwa tunafanya mazoezi katika uwanja huu.
“Ikumbukwe, kikanuni tunatakiwa kufanya mazoezi siku moja kabla ya mchezo lakini leo tunafanya siku mbili kabla ya mchezo kutokana na kesho kutakuwepo na mchezo wa ligi ambapo Zamalek watacheza kwenye uwanja huu.
“Kikosi kimefanya mazoezi ya kwanza baada ya kufika hapa nchini Misri na kila kitu kinakwenda vizuri mpaka sasa hivi.
“Kesho tutafanya mazoezi kwenye uwanja mwingine ambayo yatakuwa ni mazoezi yetu ya mwisho kuelekea mchezo wetu wa siku ya Ijumaa mida ya saa 12 jioni kwa saa za hapa Misri, lakini kwa Tanzania itakuwa mida ya saa 1 usiku.
“Wananchi, timu yenu ipo hapa, kila kitu kinakwenda sawa mpapa sasa hivi , tunahitaji sapoti kama ambavyo imekuwa kawaida yenu kutupa sapoti hata mkiwa nyumbani.
“Sisi tupo hapa kuhakikisha tunakwenda kuwapa furaha, tupo tayari kwa mchezo dhidi ya Al Ahly na tunaamini kabisa kwa kikosi kilichokuja huku kwa maandalizi bora tuliyoyapata kutoka kwa uongozi, tupo kwenye hali nzuri ya kwenda kuwafurahisha Wananchi, endeleni kutupa sapoti, furaha inaendelea,” alisema Harson.
Ikumbukwe kwamba, Young Africans na Al Ahly, zote zimekata tiketi ya kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, hivyo mchezo huo ni wa kutafuta nani atamaliza kinara wa Kundi D.