Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga, Simba zisiogope robo fainali

Simba X Yanga CAF Yanga, Simba zisiogope robo fainali

Sat, 9 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Hadi sasa, Yanga na Simba hazina baya kwa kuitoa kimasomaso nchi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuingia hatua ya robo fainali.

Kwa timu hizo mbili kuingia hatua hiyo, zimeifanya Tanzania itambe kwa msimu huu kwani ndio nchi pekee ambayo klabu zake mbili zimeweza kusogea hadi hapo na zitaungana na timu sita kutoka mataifa sita tofauti.

Mbali na Simba na Yanga, timu nyingine ambazo zimeingia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni Asec Mimosas, Al Ahly, Esperance, Petro Luanda, TP Mazembe na Mamelodi Sundowns.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), droo ya hatua hiyo ya robo fainali itachezeshwa jijini Cairo, Machi 12 na timu zilizoongoza makundi zitakutana na zile zilizoshika nafasi ya pili.

Kutokana na hilo, Simba iliyoshika nafasi ya pili katika kundi B, inaweza kukutana na mojawapo kati ya Al Ahly, Mamelodi Sundowns au Petro Luanda wakati Yanga iliyoshika nafasi ya pili kwenye kundi D inaweza kukutana na timu moja kati ya Asec Mimosas, Mamelodi au Petro Luanda.

Ukiangalia historia na hata ubora wa sasa wa hizo timu ambazo miongoni zinaweza kukutana na Simba na Yanga unaweza kutishika kwa vile sio nyepesi na zimestahili kuwepo hapo na hata matokeo ya mechi zilizopita yanatoa majibu ya wazi.

Hata hivyo, Yanga na Simba hazipaswi kuhofia timu yoyote katika hatua hiyo kwani mchezo wa soka matokeo yake yanategemea zaidi maandalizi na kiwango cha siku husika ya mchezo na sio historia au jina la timu.

Jambo la msingi kwa wawakilishi wetu ni kujipanga vyema kwa kufanya tathmini ya ubora na udhaifu wa wap-inzani na kisha kufanyia kazi katika viwanja vya mazoezi kisha kwenda kutekeleza katika mechi na sio kuamini haitowezekana.

Ukiangalia kwa sasa, Simba na Yanga zina vikosi vizuri vyenye wachezaji ambao wana uzoefu wa mashindano hayo na wengi wana viwango bora zikinufaika pia na uwepo wa makocha wa daraja la juu.

Chanzo: Mwanaspoti