Dar es Salaam. Wakati Simba imepeleka wachezaji 11 wa kikosi cha kwanza Zanzibar, Yanga leo itacheza mchezo wa nusu fainali dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Amaan.
Yanga itaivaa Mtibwa huku jicho lake likiwa katika mchezo wa fainali ambapo ikishinda itaisubiri Simba ambayo kesho itacheza na Azam katika mechi ya nusu fainali ya pili.
Endapo timu hizo zitashinda zitavaana katika mchezo wa fainali utakaochezwa Jumatatu ijayo kwenye uwanja huo ikiwa ni siku chache tangu zilipotoka sare ya mabao 2-2 kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara Januari 4.
Katika kujiwinda na mchezo huo wachezaji wa Simba Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Tairone Santos, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Deo Kanda, Mzamiru Yassin, Medie Kagere, Clatous Chama, Francis Kahata na kocha wa viungo Adel Zrane waliwasili jana visiwani humo wakitokea Dar es Salaam.
Simba na Yanga zikishinda mechi za nusu fainali, zitacheza kwa mara ya kwanza fainali ya mashindano hayo.
Timu hizo zimekuwa zikikutana katika nusu fainali na mara ya mwisho ilikuwa Januari 11, 2017 ambapo Simba ilishinda kwa penalti 4-2 na kutinga fainali ambayo ilipoteza dhidi ya Azam.
Wakati watani hao wa jadi wakiwa na rekodi hiyo, Yanga na Mtibwa zimecheza nusu fainali mara moja mwaka 2011 na wakata miwa walifungwa mabao 2-1 kupitia kwa Kigi Makasi na Davis Mwape.
Awali, Mtibwa ilipenya kwa mbinde baada ya kuifunga Chipukizi penalti 4-2 baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90.
Yanga inaweza kuwatumia Kelvin Yondani, Lamine Moro, Juma Abdul na Abdulazizi Makame ambao hawakucheza mechi ya juzi walioshinda mabao 2-0 dhidi ya Jamhuri.
Kocha msaidizi wa Yanga, Said Maulid ‘SMG’ alisema wanaumpa umuhimu mchezo wa leo kutokana na ubora wa Mtibwa katika mechi za mashindano.
Kocha wa Mtibwa Zuberi Katwila alisema watacheza kufa au kupona kupata ushindi ili kufuzu fainali.
Wakati huohuo katika mechi za Ligi Kuu jana, Coastal Union iliilaza Kagera Sugar 1-0, Alliance ilichapwa 1-0 dhidi ya JKT Tanzania, KMC na Lipuli zilitoka sare ya bao 1-1.