Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga, Simba zafunika rekodi zao

Simba Yanga Cafcl Yanga, Simba zafunika rekodi zao

Fri, 23 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ligi Kuu Bara inatarajiwa kuendelea wikiendi hii kwa mechi za raundi ya 17 baada ya kusimama kwa muda kupisha mechi za Kombe la Shirikisho (ASFC), huku Yanga ikiendelea kukaa kileleni ikicheza mechi 16 kama ilivyo kwa Azam inayoshika nafasi ya pili na alama zake 36 sawa na Simba ila zinatofautishwa na mabao ya kufunga na kufungwa tu.

Wakati ligi hiyo ikianza ngwe ya lala salama, rekodi zinaonyesha kwa mechi 15 za duru la kwanza za msimu huu, asilimia kubwa ya klabu shiriki zimeonyesha kunufaika zaidi kulinganisha na mechi kama hizo kwa msimu uliopita, huku mbio za ubingwa zikiwa bado zipo wazi kwa vigogo, Simba, Yanga na Azam tofauti na vita ya kuepuka kushuka daraja.

Kumbuka ligi hiyo inayoshirikisha timu 16, hutoa bingwa na mshindi wa pili wa kucheza mechi za Ligi ya Mabingwa, huku inayoshika nafasi ya tatu sambamba na bingwa wa ASFC zinashiriki Kombe la Shirikisho Afrika, huku timu mbili za mkiani mwishoni mwa msimu zinashuka moja kwa moja na mbili zinazomaliza nafasi ya 13 na 14 zinacheza play-off ya kuchujana zenyewe ili kubaki kwa msimu ujao na itakapofungwa itaumana na mshindi wa play-off wa Ligi ya Championship.

Mwanaspoti linakuletea namna rekodi zilivyo kwa kila klabu katika mechi 15 za duru la kwanza kwa msimu huu kulinganisha na zile za msimu uliopita zilizoshuhudiwa Ruvu Shooting na Polisi zilizokuwa mkiani zikishuka moja kwa moja kabla ya kufuatiwa na Mbeya City iliyoshindwa kufurukuta katika play-off na Mashujaa ikapanda daraja.

VITA YA POINTI Vita iliyopo sasa katika mzunguko wa lala salama ni timu zilizo katika nafasi za juu kusaka pointi tatu muhimu kwenye kila mchezo ili kukusanya pointi zitakazowapa ubingwa.

Yanga ambayo inaongoza ligi ikiwa na pointi 43 baada ya mechi 16, kwenye mechi 15 za kwanza msimu huu ilikusanya pointi 40, hizi ni pointi mbili zaidi ya zile pointi 38 ilizokusanya katika mechi 15 za kwanza msimu uliopita.

Simba ambayo ipo nafasi ya pili imekusanya pointi 36 baada ya mechi 15, imeachwa na kinara Yanga kwa pointi 7, lakini Mnyama ana mechi moja mkononi. Msimu uliopita baada ya mechi 15 za kwanza, Wekundu wa Msimbazi walikuwa na pointi 34 na walikuwa wakishika nafasi ya tatu hivyo wamevuna pointi mbili zaidi katika mechi 15 za kwanza msimu huu.

Azam FC ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 36 baada ya mechi 16, lakini kwenye mechi 15 za mzunguko wa kwanza msimu uliopita ilikusanya pointi 35, sawa na mechi 15 za msimu huu, ila msimu uliopita pointi zao 35 ziliwaweka katika nafasi ya pili.

Mambo yamekuwa magumu upande wa Singida Fountain Gate kwani msimu uliopita mzunguko wa kwanza walikuwa nafasi ya nne na pointi 27 mzunguko wa msimu huu wametupwa nafasi ya sita wakiwa na pointi 20, wamepoteza pointi saba.

Nafasi ya nne mzunguko wa kwanza msimu huu ilikwenda kwa KMC ambayo katika mechi 15 za kwanza ilikusanya pointi 22 ikiongeza pointi sita ukilinganisha na mzunguko wa kwanza msimu uliopita iliokusanya pointi 16 na kushika nafasi ya 10 kwenye msimamo.

Coastal Union katika mechi 15 za kwanza msimu ilikusanya pointi 20, wakati msimu uliopita ilimaliza mzunguko wa kwanza ikiwa na pointi 15.

KUSHUKA DARAJA Tanzania Prisons, Dodoma Jiji, Namungo Kagera Sugar, Ihefu FC, Geita Gold, JKT Tanzania, Tabora United, Mashujaa FC na Mtibwa Sugar ni timu ambazo zipo kwenye vita kubwa ya kupambana kubaki Ligi Kuu Bara msimu huu.

Kwa sasa kwenye timu 16 ni timu tatu za juu, kinara Yanga, Simba na Azam FC ndizo zenye uhakika wa kubaki Ligi Kuu msimu ujao, timu nyingine zote haziko salama na hasa timu kuanzia inayoshika nafasi ya saba hadi mwisho ya 16.

Mtibwa Sugar ambayo inaburuza mkia ikikusanya pointi nane tu mzunguko wa kwanza, msimu uliopita ilikuwa nafasi ya sita ikikusanya pointi 22, yaani pungufu pointi 16 msimu huu ikiwa inapumulia mashine sawa na ilivyokuwa kwa Polisi Tanzania iliyoshuka daraja msimu uliopita kwa pointi tisa, ikiwa ni moja zaidi na ilizonazo wanaManungu.

Ruvu Shooting ambayo pia ilishuka daraja msimu uliopita mzunguko wa kwanza ilikusanya pointi tisa, wakati msimu huu nafasi hiyo inashikiliwa na Mashujaa iliyovuna pointi 10 katika mechi 15 za kwanza, ikifuatiwa na Geita Gold iliyovuna pointi 16 katika mechi 15 za kwanza, huku Tabora United na JKT Tanzania zikifuata juu yake zivuna pointi 17 nusu ya kwanza ya msimu huu.

Kagera Sugar ambayo msimu uliopita mechi 15 ilikuwa nafasi ya saba ikikusanya pointi 21 msimu huu mzunguko wa kwanza ilivuna pointi 17, Namungo FC imevuna pointi 18 katika mechi 15 za kwanza, msimu uliopita ilikuwa na pointi 18 hivyo inaenda sawa wakati Dodoma Jiji mechi 15 za kwanza ilivuna pointi 19, msimu uliopita ilikuwa na pointi 15. MBIO ZAUFUNGAJI Msimu uliopita Yanga ikiwa na aliyekuwa mshambuliaji wake Fiston Mayele ambaye aliibuka kinara akifunga mabao 17, kwenye mechi kama hizo za duru la kwanza ilifunga mabao 27, lakini msimu huu imekuwa bora zaidi kwa kutupia kambani mabao 39, huku Stephane Aziz KI akifunika na mabao 10 katika mechi hizo 15 za awali.

Wakati Yanga ikifunga idadi hiyo kubwa ya mabao msimu huu, Simba mzunguko wa kwanza msimu huu imetupia mabao sawa na msimu uliopita ilipofunga mabao 31, Azam FC safu yao ya ushambuliaji imeimarika hivyo ndio unaweza kusema baada ya msimu uliopita kufunga mabao 22 katika mechi 15 za kwanza na msimu huu ilitupia mabao 36 katika mechi 15 za kwanza, sawa na Yanga.

Coastal Union msimu uliopita ilifunga mabao 14 mzunguko wa kwanza na msimu huu 12, KMC ilifunga 12 na msimu huu ilifunga mabao 15 katika mechi 15 za kwanza, Singida Fountain Gate ilifunga 16 na msimu huu ilifunga mabao 18, Tanzania Prisons 11 msimu huu ilifunga 17, Dodoma Jiji 10 msimu huu 13, Namungo 11 msimu huu 12, Kagera Sugar 15 msimu huu kumi, Ihefu FC ilifunga 11 na nusu ya msimu huu 13.

Wakati JKT Tanzania, Tabora United na Mashujaa zimepanda daraja msimu huu, Geita Gold wao walifunga mabao 17 na msimu huu wakafunga tisa, Mtibwa Sugar ambao wanaburuza mkia walifunga mabao 16 mzunguko wa kwanza na nusu ya msimu uliopita walifunga 21.

VIPIGO VIKUBWA Msimu huu hadi mzunguko wa 15 kulikuwa na vipigo vikubwa 10 huku kati ya hivyo Yanga na Azam FC wanafungana kwenye idadi ya kutoa vipigo wakivitoa kwa timu nne kila moja na Simba ikitoa vipigo viwili.

Yanga alianza dhidi ya KMC (5-0), JKT Tanzania (5-0), Simba (5-1), Mtibwa Sugar (4-1) kwa upande wa Azam FC dhidi ya Tabora United (4-1), Mtibwa Sugar (5-0), Geita Gold (4-1) na KMC (5-0) na Simba wao wakiwanyuka Mtibwa Sugar (4-1) na Tabora United (4-0).

Msimu uliopita kwenye mizunguko 15 ya kwanza kulikuwa na vipigo vitano tu Simba akitoa viwili dhidi ya Ruvu Shooting (4-0), Mtibwa Sugar (5-0) huku Azam FC akishinda (4-2) dhidi ya Mtibwa na Geita Gold akiifunga Mtibwa 4-2.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live