Kambi za Simba na Yanga zimezidi kunoga baada ya mastaa wapya waliosajiliwa kwenye dirisha dogo kuungana na wale ambao hawakuitwa katika timu za taifa zilizoenda kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023, huku wakisubiri wale waliokuwa timu za taifa kuanza kuwasili kuanzia leo.
Lakini wakati kambi hizo zikiendelea kunoga, klabu hizo sasa zitakuwa kwenye kazi moja tu ya kula viporo, baada ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kutolewa mapema Afcon, hivyo mamlaka zinasoimamia soka nchini kuanza kutoa ratiba za mechi za viporo vya Ligi Kuu Bara.
Baada ya Yanga kumaliza kiporo chake cha Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Hausung ya Njombe kesho Januari 30, itaenda kagera kwaajili ya mechi ya Februari 2 na Kagera Sugar kisha Februari 5 kukipiga na Dodoma Jiji uwanja wa Azam Complex na kumalizia viporo vyake Februari 8 dhidi ya Mashujaa.
Keshokutwa Simba itaanza kiporo cha ASFC dhidi ya Tembo FC na kuendelea na Ligi dhidi ya Mashujaa katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, kabla ya kukutana na Tabora United ugenini Februari 6.
Simba itakutana na Azam kwenye Dabi ya Mzizima Februari 9 na kumaliza viporo vyake na Geita Gold Februari 12, Uwanja wa CCM kirumbu, Mwanza.