Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga, Simba balaa lipo hapa

Yanga X Simba Balaa Yanga, Simba balaa lipo hapa

Sat, 9 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ukitaja timu ambayo imekuwa bora kwenye ufungaji wa mabao ndani ya boksi (ndani ya 18) hauwezi kuacha kuitaja Yanga kwani imeonyesha ufundi katika msimu huu hadi sasa katika mashindano yote ambayo imeshiriki.

Yanga hadi sasa imecheza mechi sita za mashindano huku mchezo mmoja pekee ndio haikufunga bao ni wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba.

Katika mechi tano za mashindano ambazo Yanga imecheza imefunga mabao 19 na kuruhusu bao moja tu.

Yanga imefunga mabao 12 ndani ya boksi huku saba yakiwa ya nje ya eneo hilo.

Katika mchezo wa kwanza ambao Yanga ilifunga ni dhidi ya Azam FC katika mechi ya Ngao ya Jamii na mabao yote yalikuwa ni nje ya boksi.

Stephen Aziz KI ndiye mchezaji wa kwanza kufunga bao katika mechi hiyo baada ya dakika ya 84 kuwatoka mabeki wa Azam FC na kufyatuka shuti lililokwenda wavuni na dakika ya 88, Clement Mzize alipigilia bao la pili na la mwisho.

Mechi ya pili Yanga ambayo ilifunga mabao ilikuwa kwenye mchezo wa hatua ya kwanza ya awali katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya ASAS ya Djibout na ilishinda mabao 2-0 yote yakiwa ndani ya boksi (18).

Kiungo mshambuliaji, Aziz KI alifunga dakika ya 22 akipokea pasi ya beki Joyce Lomalisa aliyepiga ndani ya boksi na KI alifunga huku bao la pili likifungwa dakika ya 52 na Kennedy Musonda ambaye alipigiwa pasi na Mudathir Yahya na yeye aliingia ndani ya boksi na kufunga.

Mechi ya tatu ilikuwa upande wa Ligi Kuu Bara Yanga ikiifunga KMC 5-0 huku mabao matatu yakiwa ndani ya boksi na mawili ni nje.

Bao la kwanza lililofungwa dakika ya 17 na beki Dickson Job lilitokana na piga nikupige langoni kwa KMC bao la pili likifungwa na Aziz Ki ndani ya boksi akipokea pasi ya Jesus Moloko.

Straika wa Yanga, Hafidh Konkon alifunga bao la tatu dakika ya 70 baada ya kutokea piga nikupige huku la nne likifungwa na Mudathiri dakika ya 76.

Wakati huo huo mshambuliaji, Pacome Zouazoua alifunga bao la tano dakika 81 akipokea pasi ya Maxi Nzengeli na yeye aliwatoka mabeki wa KMC na kuweka mpira wavuni.

Katika mchezo wa marudiano dhidi ya ASAS, Yanga ilishinda 5-1 huku mabao yake yote yakiwa ndani ya boksi.

Maxi Zengeli ndiye mchezaji wa kwanza kufunga akiweka wavuni dakika ya nane akiwa ndani ya boksi akipokea pasi ya Jesus Moloko huku bao la pili likifungwa dakika ya 45 na Konkon akipokea pasi ya Aziz KI ndani ya boksi na yeye aliweka wavuni.

Pacoume katika dakika ya 55 aliifungia Yanga bao la tatu akipokea pasi ya Maxi Zengeli ndani ya boksi akawachambua mabeki na kipa wa ASAS kisha aliweka mpira wavuni.

Dakika ya 69 mshambuliaji, Clement Mzize aliifunga bao la nne katika mechi hiyo akionganisha kwa kichwa krosi ya Nickson Kibabage akiwa ndani ya boksi na mpira ukaenda wavuni.

Chuma cha mwisho kilifungwa na Max Nzengeli dakika ya 90+ akipokea pasi ya Clement Mzize.

Mchezo wa mwisho Yanga kucheza kabla ya Ligi haijasimama ni dhidi ya JKT Tanzania ambao ilishinda 5-0 huku mabao mawili yakiwa nje na matatu ndani ya boksi.

Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Aziz KI ndiye aliyekuwa wa kwanza kufunga bao katika mchezo huu dakika 45+ kwa kupiga faulo nje ya boksi.

Bao la pili lilifungwa dakika ya 55 na Kennedy Musonda ndani ya boksi akionganisha pasi ya Nickson Kibabage huku bao la tatu likifungwa na Yao Attohoula nje ya boksi dakika ya 65.

Huku Nzengeli aliweka wavuni chuma cha mwisho dakika ya 88 akiwa ndani ya boksi akipokea pasi ya Yao na yeye alipiga mpira ulioenda wavuni.

SIMBA SASA

Simba imecheza mechi nne za mashindano, mbili za Ngao ya Jamii na mbili Ligi Kuu. Upande wa Ngao Simba haikufunga bao lolote lile ndani ya dakika 180 lakini kwenye Ligi Kuu mechi zote mbili ilifunga.

Dhidi ya Mtibwa Sugar, Simba ilishinda 4-2 huku mabao yote yakiwa yamefungwa ndani ya boksi.

Bao la kwanza lilifungwa na Jean Baleke dakika ya sita akipokea pasi ya Kibu Denis, bao la pili lilifungwa na Willy Onana dakika ya tisa baada ya kutokea piga nikupige langoni kwa Mtibwa.

Bao la tatu lilifungwa dakika ya 44 na Fabrice Ngoma baada ya kutengewa mpira ndani ya boksi kwa kichwa na Baleke kisha (Ngoma) aliweka wavuni kwa kichwa huku bao la nne likifungwa na Clatous Chama dakika ya 81 ambaye alipokea pasi ndefu kutoka kwa Luis Miqquisone iliyokwenda moja kwa moja kwa Chama aliyeweka mpira wavuni.

Mchezo wa pili Simba kwenye Ligi Kuu iliichapa Dodoma Jiji 2-0 huku bao la kwanza likifungwa dakika ya 44 na Jean Baleke ambaye alipokea pasi kutoka kwa Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na yeye aliuweka wavuni akiwa katikati ya mabeki akiwa ndani ya boksi. Bao la pili liliwekwa wavuni dakika ya 55 na Moses Phiri akiwa ndani ya boksi baada ya kupokea pasi ya Shomari Kapombe nje kidogo ya boksi na kuingia nao kisha aliweka mpira wavuni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: