Simba na Yanga zimehitimisha safari katika michuano ya kimataifa msimu huu baada ya kutolewa katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Al Ahly na Mamelodi Sundowns.
Yanga ilianza mapema kushuka uwanjani saa 3:00 juzi usiku kukabiliana na Mamelodi kwenye Uwanja wa Luftus Versfeld, Pretoria, Afrika Kusini na dakika 90 zikaisha kwa kutofungana kama ilivyokuwa wiki iliyopita katika mchezo wa kwanza uliopigwa Kwa Mkapa.
Ikaamuliwa mikwaju ya penalti na Yanga kupoteza mitatu kupitia Stephane Aziz KI, Dickson Job na Ibrahim Bacca, wakati wenyeji walipoteza wa Gastón Sirino, huku mitatu ikiingia kambani na kuivusha Mamelodi kwenda nusu fainali kwa ushindi wa penalti 3-2.
Kwa upande wa Simba ikitoka kufungwa bao 1-0 nyumbani na watetezi wa taji, Al Ahly, ilishuka uwanjani kuanzia saa 5:00 usiku kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, Misri na kuchapwa mabao 2-0 na wenyeji hao, hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 3-0. Hii ikiwa ni mara ya tano kati ya misimu sita ambayo Mnyama amefika robo fainali ya michuano ya CAF ikishindwa kuvuka salama kwenda nusu fainali.
Timu hizo zinarudi nyumbani kuendelea na michuano ya Kombe la Shirikisho na Ligi Kuu kusaka tiketi za CAF kwa msimu ujao, lakini zikiacha alama flani hususan kwa Yanga katika michuano hiyo kwamba miaka michache ijayo timu za Tanzania zinaweza kuandika rekodi ya kubeba ubingwa Afrika.
Kwa namna klabu hizo zinavyoendelea kufanya uwekezaji katika timu na aina ya wachezaji na makocha wanaoajiriwa, Simba na Yanga zikikaza kidogo zitaanza kuzoea michuano hiyo na kubanana na vigogo vya soka vinavyopokezana mataji ya CAF kila msimu.
Hata makocha waliowahi kuzinoa timu hizo na ambao walizifuatilia katika michuano hiyo wamefunguka na kueleza namna wanavyoziona siku za usoni zikifanya maajabu Afrika.
Makocha wa zamani wa timu hizo, wanaona hatua kubwa ikipigwa na klabu hizo kiasi kwa sasa kuwa tishio Afrika tofauti na namna ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo Simba na Yanga zilikuwa zikiishia katika hatua za awali.
Kwa sasa ni jambo la kawaida klabu za Tanzania kufika robo fainali, na zikipambania ni nusu na hata fainali jambo ambalo makocha hao wanaamini linawezekana kikubwa ni kuendelea kusukuma gurudumu la kujenga vikosi ili kuwa bora zaidi.
Hans van der Pluijm ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa makocha bora wa kigeni kufundisha soka Tanzania, anasema Yanga imepiga hatua kwa kasi misimu miwili iliyopita huku Simba ikionekana kujipambanua.
“Nafurahi kukua kwa soka la Tanzania kwa sababu nimekuwa sehemu ya hili. Huu ni msimu wa kipekee kwangu sijali hata kama watatolewa robo (fainali) nilichokiona ni mmea ambao tayari umechipua na suala na robo au nusu fainali ni la muda tu kwa sababu tayari wameshajua nini wanapaswa kufanya ili kushinda ubingwa wa Afrika,” anasema.
“Kukosea huimarisha na hufanya timu kupata uzoefu ambao utawafanya siku moja lengo la kuchukua ubingwa kufanikishwa. Kwangu kukosea ni sehemu ya mafanikio. Unaweza kukosea mara tatu, nne hadi tano na ya sita ukafanikiwa. Kuacha kujaribu ndio kufeli kwenyewe. Naziona mbali sana Simba na Yanga.”
Kwa upande wake, Dylan Kerr amesema: “Hata Mamelodi ambayo kwa sasa inatazamwa kama moja ya klabu kubwa Afrika iliwachukua muda wa kukijenga kikosi chao, Simba na Yanga zipo katika mwelekeo mzuri, wanachotakiwa ni kuendelea kuamini katika mipango yao wasitolewe kwenye mstari kwa sababu mpango ukikamilika wanaweza kuishangaza Afrika kwa kiwango kikubwa.”
Kocha huyo Muingereza ambaye aliinoa Simba, Gor Mahia ya Kenya kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki anaamini kufanya vizuri kwa Simba na Yanga kwa miaka ya hivi karibuni katika michuano ya kimataifa ni kivutio tosha cha kupata wachezaji wenye malengo makubwa na ubora wa aina yake.
“Wachezaji wakubwa huhitaji uhakika wa karibu kila msimu kucheza michuano ya kimataifa, tumeona hilo likifanikishwa kwa Simba na Yanga kwa misimu ya hivi karibuni, kama wataendelea hivi basi kuna uwezekano mkubwa mbeleni tukashuhudia mmoja kati yao au wote kwa vipindi tofauti wakacheza fainali.”
BATO NA VIGOGO
Kwa misimu ya hivi karibuni Simba na Yanga zimeonyesha kuwa sio wanyonge tena mbele ya vigogo wa soka la Afrika katika michuano hiyo ya kimataifa tofauti na miaka ya nyuma ambapo walionekana kuwa ni timu dhaifu.
Safari za Simba na Yanga zilikuwa zikishiia katika hatua za awali tu hasa wanapopangwa na timu kutoka ukanda Magharibi na Kaskazini mwa Afrika lakini kwa sasa wanaweza kutunishiana misuri na timu hizo.
Msimu uliopita wa Kombe la Shirikisho Afrika ambapo Yanga ilifika hadi fainali na kupoteza kwa kanuni dhidi ya USM Alger, iliitolea uvivu Club Africain ya Tunisia katika hatua ya mchujo kuwania nafasi ya kutinga makundi.
Ikiwa nyumbani Yanga ilitoka suluhu, wakati ambao Club Africain ikiamini itamaliza kazi kwenye uwanja wake wa nyumbani, Hammadi Agrebi, Tunis ndipo Stephane Aziz KI alipowafunga mdomo katika dakika ya 79 na Wananchi wakatinga kibabe kwenye hatua ya makundi.
Sio dhidi ya Club Africain pekee, Yanga imeshindana na kuonyesha ushindani mkubwa dhidi ya vigogo wengine wengi katika soka la Afrika kama vile Al Ahly, Mamelodi Sundowns na hata CR Belouizdad ambao waliktandikwa maba 4-0 kwenye uwanja wa Mkapa.
Simba huku ndio kama nyumbani kwani ndani ya msimu minne mfululizo wametinga robo fainali huku moja ambayo ni ya msimu wa 2021-22 ikiwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Kama kubato na vigogo, Simba ndio zake na wameonyesha ushindani wa aina yake kwa awamu tofauti mbele ya Al Ahly, Raja Casablanca, Wydad Casablanca na timu nyingine kubwa na zenye historia ya kutisha katika michano ya kimataifa.
UWEZO UGENINI
Miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakizipa wakati mgumu klabu nyingi za Afrika ni juu ya namna ya kupata matokeo mazuri ugenini, kitu ambacho kwa Simba na Yanga wameonakana kukimudu kwa miaka ya hivi karibuni.
Msimu huu katika hatua ya makundi, Simba ambayo ilikuwa kundi B ilipoteza mara moja tu ikiwa ugenini na ilikuwa Morocco tena kwa bao 1-0 dhidi ya Wydad Casablanca katika michezi mingine ilivuna pointi moja moja ambapo ni dhidi ya Jwaneng Galaxy (Botswana) na ASEC Mimosas (Ivory Coast).
Msimu uliopita 2022-23 katika raundi ya kwanza, Simba iliitandika Nyasa Big Bullets mabao 2-0 ikiwa ugenini na katika raundi ya kwanza wakiwa Angola waliendeleza dozi ya ugenini kwa kuwafunga C.D. Primeiro de Agosto mabao 3-1 na kumalizia kazi nyumbani kwa kushinda bao 1-0 na kutinga hatua ya makundi.
Kwa upande wa Yanga msimu uliopita walikuwa bora zaidi katika michezo ya ugenini katika kombe la shirikisho Afrika kwani ukiachana na Club Africain, walipata pointi ugenini dhidi ya Real Bamako na TP Mazembe katika hatua ya makundi.
Katika michezo ya mtoano, Yanga iliendeleza ubabe wa kufanya vizuri ugenini kwa kuifunga Rivers United ya Nigeria mabao 2-0, nusu waliifunga Marumo Gallants ya Afrika Kusini kwa mabao 2-1 na hata katika fainali USM Alger iliyokuwa ikinolewa na Abdelhak Benchikha ilifungwa bao 1-0 huko Algeria.
UBORA WA VIKOSI
Tofauti na miaka ya nyuma kwa sasa mastaa wa kigeni wa Simba na Yanga wamekuwa wakipata nafasi ya kuitwa na kucheza katika timu zao za taifa, na sio wachezaji kutoka mataifa ya kawaida hivyo hiyo inaonyesha kuwa vigogo hao vikosi vyao vinaundwa na wachezaji wenye ubora wa aina yake.
Kitendo cha kuwa na wachezaji wa daraja hilo, ni kiashiria tosha kuwa Simba na Yanga zipo katika mwelekeo mzuri ambao unaweza kuleta matunda tofauti na miaka ya nyuma ambapo wachezaji kutoka mataifa ya Mali, Nigeria, Ivory Coast walikuwa wakisikia tu kuhusu kuitwa kuzichezea timu zao za taifa.
Kwa sasa wachezaji kama Clatous Chama (Zambia), Henock Inonga (DR Congo), Saido Ntibazonkiza (Burundi) kwa Simba wamekuwa wakiitwa upande wa timu zao za taifa huku kwa Yanga ikiwa Aziz KI (Burkinafso), Djigui Diarra (Mali), Pacôme Zouzoua (Ivory Coast), Kennedy Musonda (Zambia).
Nyota hao wa kigeni wamekuwa wakiongeza ubora wa aina yake katika vikosi vyao ukichanganya na wazawa ambao nao wamekuwa wakijisukuma ili kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara mbele ya nyota hao na wengine.
NGUVU KIUCHUMI
Uwepo wa Mohammed ‘Mo’ Dewji na Ghalib Said Mohamed ‘GSM’ umezifanya Simba na Yanga kuwa na jeuri ya kujaribu hata kutunishiana misuri na vigogo wa soka la Afrika.
Nguvu ya fedha katika soka la Afrika na hata duniani kwa ujumla ni kubwa na ndio maana Al Ahly na Mamelodi Sundowns zinaonekana kusumbua kutokana na uwekezaji ambao umefanywa na matajiri katika klabu hizo.
Mbali na mikakati mizuri ambayo Mamelodi imekuwa nayo, Patrice Motsepe, mmiliki wa Masandawana ambaye pia ni rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) amekuwa akimwaga fedha kwa ajili ya shughuli za uendeshaji ikiwemo usajili. Japo hatuwezi kulinganisha nguvu ya kiuchumi kwa Simba na Yanga dhidi ya Mamelodi au Al Ahly, lakini kwa sasa angalau bajeti za watani hao zimekuwa zikiongezeka kulingana na mahitaji ya soka kiasi cha kumudu kusajili wachezaji kutoka mataifa makubwa zaidi kisoka Afrika na kuwalipa makocha wa daraja la kati na juu katika mpira wa Afrika, na ndio maana imeshahudia kina Miguel Gamondi na Benchikha wakifanya yao katika vikosi hivyo.
MSIKIE MOKWENA
“Siwezi kupata maneno mazuri ya kumtuliza (Gamondi), bila shaka hisia ya kuibiwa kwa kocha mwi-ngine yeyote si nzuri,” anasema Mokwena alipoulizwa kuhusu matamshi ya Gamondi kwa mwamuzi ambaye alionyesha wazi kutoku-baliana na uamuzi wa kunyimwa bao la Stephane Aziz KI.
“Kulikuwa na hali nyingine nyingi kama vile kumpiga kiwiko Devine Lunga ndani ya boksi, na hiyo inaweza kuwa penalti Lakini sitaki kuzungumzia mambo hayo. Labda kama ningepoteza, pia ningechukua mwelekeo huo, lakini wacha niwe na neema na heshima katika ushindi. (Yanga) walikuwa wapinzani wanaostahili. Timu nzuri ambayo tulifurahi kucheza dhidi yao nyumbani na ugenini.”