Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga, Simba SC mchezo umekwisha mapema tu

98359 Mechi+pic Yanga, Simba SC mchezo umekwisha mapema tu

Mon, 9 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

UKIONA imefika sehemu matajiri wameamua kuingia jikoni wenyewe ujue kazi imeisha. Vigogo wote unaowajua wa Yanga wale wenyewe wenyewe sambamba na GSM juzi na jana walikuwa na vikao mara kadhaa vya kupanga mikakati mizito ya kumuua Mnyama leo jioni Taifa. Lakini hatari kubwa zaidi ni kwamba Bilionea wa Simba, Mohammed ‘Mo’ Dewjishoo ya leo ameisimamia na miguu yote. Mo huwa ni mara chache sana kujitokeza na kuzungumza na wachezaji au kuingilia mipango ya hamasa ndani ya timu, lakini amekutana na wazito wenzie na tayari wametoa ahadi za kufa mtu kwa wachezaji. Jana usiku kabla ya mechi ya Burnley na Spurs ya huko England, alipanga kuwa na kikao cha mwisho na wachezaji kambini.

MECHI YA FEDHA Achana na mamilioni ya fedha ambayo wametumia katika kusuka vikosi, mechi ya Yanga na Simba leo pekee ina thamani ya zaidi ya Shilingi 1.55 bilioni jambo linaloashiria ukubwa wa klabu hizo mbili kongwe nchini. Thamani hiyo ya fedha ya mechi hiyo itakayochezwa kuanza saa 11 jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini, inahusu ahadi ambazo zimetolewa kwa kila timu, mgawo wa fedha kutoka kwa wadhamini na mapato yatokanayo na viingilio. Kutokana na fedha za viingilio vilivyotangazwa, makadirio ya mapato ambayo huenda yakapatikana kutoka milangoni ni kiasi cha Sh 600 milioni. Katika mchezo uliopita baina ya timu hizo mbili uliochezwa Januari 4 na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2, kiasi cha mapato yaliyotokana na fedha za viingilio kilikuwa ni Sh 539 milioni. Lakini pia kuna fedha kiasi cha Sh 500 milioni ambacho timu hizo zimepata kutoka kwa mdhamini wao mkuu, Kampuni ya ubashiri wa matokeo ya michezo ya SportPesa ambapo kila moja itapata mgawo wa Shilingi 250 milioni. Ukiondoa fedha hizo, kuna fedha takribani Shilingi 400 milioni ambazo zinatokana na ahadi ambayo imetolewa kwa kila timu ikiwa itapata ushindi katika mchezo huo. Yanga ambao ni wenyeji, wametoa ahadi ya Sh 300 milioni kwa wachezaji na benchi la ufundi ikiwa tu wataibuka na ushindi wa aina yoyote ile mbele ya Simba leo. Kila mchezaji ameahidiwa Sh.10 milioni. Simba wameweka ahadi ya takribani Sh 150 milioni kwa nyota wao na benchi la ufundi ikiwa watawatia adabu Yanga. Kiwango hicho cha fedha kwa pamoja ambacho huenda kikaongezeka kulingana na matajiri watakavyofurahi leo kinazidi Sh 1.45 bilioni ambacho kinafanya mechi hiyo kuwa na thamani kubwa zaidi nchini kuliko nyingine yoyote iliyowahi kuchezwa siku za nyuma.

MO, GSM NA VIGOGO Katika kuhakikisha kila upande unaibuka na ushindi, vigogo wa pande zote mbili wamekuwa na vikao visivyokwisha na wachezaji ili kuwahamasisha wafanye vizuri katika mchezo huo. Chagizo kubwa kwa upande wa Yanga limekuwa likifanywa na mmoja wa wadhamini wao, Kampuni ya GSM ambaye mbali ya kutoa ahadi ya fedha kwa timu, pia amewaunganisha wadau wote wakubwa wa timu hiyo kuhakikisha wanakuwa na umoja kuelekea mechi hiyo. Taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti linazo ni kuwa kambi hasimu ndani ya Yanga zimepatanishwa na wote wameungana kuhakikisha Mnyama anakufa leo. Lakini pia viongozi wa zamani wa Yanga kama Hussein Nyika, Abdallah Bin Kleb, Seif Magari na wengineo, wamerudishwa kundini tayari kwa mechi hiyo na wengi wao juzi na jana walitembelea kambini na mazoezini kuwapa hamasa wachezaji na wameahidi Sh10milioni kwa kila mchezaji. Hilo halijaishia kwa Yanga tu kwani hata Simba nao, vigogo maarufu wa klabu hiyo  hawakulala usiku na mchana kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo. Vigogo hao ambao wengi wao ni wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa klabu hiyo wamekuwa wakijitokeza mazoezini na kambini huko Bunju ili kuweka mambo sawa ambapo wamewawekea wachezaji na benchi la ufundi Sh150milioni wagawane wakishinda leo. Na katika kuongeza hamasa zaidi, mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa klabu hiyo, Mfanyabiashara Mohamed Dewji, juzi alikutana na kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck na jana alikwenda kambini kuzungumza na wachezaji huku akiahidi leo kujitokeza uwanjani kuwasapoti nyota wake.

SHOO YA MORRISON NA LUIS Yanga wana Bernard Morrison na Simba wanaye Luis Miquissone. Uwezo wa kumiliki mpira, kasi, chenga, kutengeneza nafasi na kufunga mabao ambao wanao, umewafanya wawe gumzo katika siku za hivi karibuni. Morrison tayari ameshaifungia Yanga mabao mawili katika Ligi Kuu wakati Miquissone yeye ameifungia Simba mabao matatu.

VIUNGO Timu itakayokamata idara ya kiungo inaweza kuwa na nafasi kubwa ya kupata ushindi katika mechi hiyo. Simba inaonekana itaendelea na mfumo wake wa 4-4-2 ambao imekuwa ikianza na vingo wanne lakini Yanga kuna uwezekano ikapanga wachezaji watano katika safu ya kiungo ikitumia mfumo wa 4-2-3-1.

VIKOSI Kikosi cha Yanga huenda kikaundwa na Metacha Mnata, Juma Abdul, Jafari Mohamed, Lamine Moro, Kelvin Yondani, Feisal Salum, Papy Tshishimbi, Bernard Morrison, Mapinduzi Balama, Haruna Niyonzima na Ditram Nchimbi.

Kwa Simba kinaweza kuwa hivi, Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohamed Hussein, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Luis Miquissone, Clatous Chama, Meddie Kagere, John Bocco na Francis Kahata.

MAREFA SITA Mwamuzi Martin Saanya kutoka Morogoro ndiye atakayeshika kipenga cha kuamua mchezo huo akisaidiwa na washika vibendera Mohamed Mkono na Frank Komba huku mezani akiwepo Elly Sasii. Marefa Abdallah Mwinyimkuu (Singida) na Ramadhan Kayoko (Dar es Salaam)  watasimama nyuma ya magoli.

DAKIKA HIZI Ingawa kila timu inahitajika kucheza kwa umakini katika dakika zote 90 za mechi, tahadhali kubwa zaidi zinapaswa kuichukua katika kipindi cha pili hasa kuanzia dakika ya 46 hadi ya 70. Muda huo ndio ambao timu hizo zimekuwa zikifunga idadi kubwa ya mabao lakini pia ndio ambao zimekuwa zikiruhusu nyavu zao kutikiswa mara kwa mara. Katika mabao 29 ambayo Yanga imefunga katika Ligi Kuu hadi sasa, 16 imefunga kipindi cha pili na 13 kipindi cha kwanza wakati kwa Simba iliyofunga mabao 55, dakika 45 za kwanza imefumania nyavu mara 21 wakati kipindi cha pili imefunga mabao 34. Kuanzia dakika ya 46 hadi 75, Yanga imefunga mabao 16 wakati Simba imefunga mabao 24. Katika kipindi cha pili, Yanga imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 10 wakati Simba imefungwa mabao saba (7).

MAKOCHA WATAMBA Kocha wa Yanga, Luc Eymael alisema; “Ni kweli Simba kwa ubora wa mchezaji mmoja mmoja imetuzidi, lakini ukweli ulivyo katika mechi hizi kubwa mara nyingi jambo hilo halipo isipokuwa timu inayocheza kwa pamoja kwa maana ya kushambulia na kukaba kwa nidhamu ndio inafanikiwa.” “Nina uzoefu wa kutosha na mechi kama hizi tangu nikiwa nafundisha Sudan, DR Congo na Kenya. Mchezo huu ili upate matokeo mazuri ni kuandaa mbinu si kuangalia rekodi au matokeo ya nyuma,” alisema Eymael Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck alisema; “Ni mechi ngumu kama zilivyo znyingine na lengo letu ni kupata ushindi katika kila mchezo. Tunafahamu, umuhimu wa kupata ushindi katika mechi hiyo na naamini wachezaji wakicheza kwa kujitolea na weledi basi tutapata ushindi.”

Chanzo: mwananchi.co.tz