Kocha msaidizi wa Yanga Princess, Fred Mbuna amesema kikosi kinajinoa kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Wanawake na mashindano ya Get International, huku akisisitiza kuwa wanataka ubingwa.
Wiki iliyopita Yanga Princess iliachana na wachezaji 13 na tayari imeshatambulisha watatu akiwemo Madina Traore kiungo kutoka Burkina Faso, Faiza Sedu straika raia wa Ghana na Adejoke Ejalonibu kiungo mshambuliaji kutoka Raja Casablanca ya Morocco.
Mbuna alisema viongozi wa timu hiyo waliona haja ya kuondoa wachezaji 13 ili kusafisha kikosi kwa ajili ya msimu ujao na anaamini wapya waliosajiliwa watasaidia kutwaa ubingwa.
Msimu uliopita Yanga Princess ilimaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi.
Aliongeza kuwa timu hiyo ilicheza mechi mbili za kirafiki wiki iliyopita - ile ya kwanza ikishinda mabao 7-0 dhidi ya Sports Academy na 2-0 dhidi ya Ilala Queens ikiwa ni kipimo cha maandalizi ya michuano ya Get International yatakayofanyika mjini Dodoma kuanzia Septemba 9 hadi 23.
Mashindano hayo yanajumuisha timu 12 zikiwamo Get Program, Fountain Gate Princess, Yanga, Simba, Bunda Queens, New Generation, JKT Queens, Alliance Girls, CFC Aman FC, Polisi Queens, Kampala Queens na Ceasia Queens.